Rais Kikwete Ataja Changamoto za Rais Mpya Ajaye
RAIS mpya wa Tanzania anakabiliwa na changamoto kubwa ya kuhakikisha Tanzania itaendelea kubakia kuwa moja kwa kudumisha Umoja wetu na Amani kwani Tanzania inatokana na muungano wa nchi mbili.
Rais Jakaya Kikwete ameyasema hayo jijini Stockholm – Sweden ambapo alikuwa akizungumza na watanzania waishio Sweden mara baada ya kuwasili na kuanza ziara ya kikazi ya siku 3, kuanzia tarehe 3 – 5 Juni,2015.
“Hapa tulipofikia lazima kuhakikisha Taifa linakuwa moja, kuna vyama, na makabila mbalimbali, lazima uhakikishe Nchi inabaki moja”. Rais amesisitiza.
Watanzania mbalimbali walioko nchini Sweden kwa ajili ya shughuli za kikazi, kimasomo na ambao wanaishi nchini Sweden, walifika kumpokea na kumsalimia Rais Kikwete ambapo pia wamemsomea risala ambayo pamoja na vitu vingine wametaka kujua kuhusu haki yao ya kupiga kura katika uchaguzi Mkuu ujao.
“Swala hili linategemea Tume ya Uchaguzi, likiwekewa utaratibu linawezekana. Taratibu zake hazijawekwa, lakini ninaamini kuwa uchaguzi ujao unakuwa uchaguzi wa mwisho ambao watanzania wanaoishi nje hawapigi kura”. Rais amesema.
Rais Kikwete pia ameelezea matumaini yake kuwa Tanzania itapata kiongozi mzuri na kuelezea mafanikio ambayo serikali yake imeyapata na kutumaini kuwa yatadumishwa na kuendelezwa na Rais ajaye.
Mapema akisoma risala ya watanzania, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania Nchini Sweden Bw. Tengo Kilumanga, amempongeza Rais Kikwete kwa kuridhia na kuonesha nia ya dhati ya kumaliza kipindi cha uongozi wake na kuwa mfano bora katika ukanda wa Afrika Mashariki.
“Tunakupongeza mheshimiwa Rais, viongozi wengi katika Bara la Afrika huwa hawaagi, umefanya kitendo cha kishujaa sana. Viongozi wa Afrika huwa hawaagi kwa sababu siku ya kuondoka madarakani huwa haijulikani”. Amesema Bwana Kilumanga. “Hii inaonesha wewe sio Mtu wa kupenda madaraka”. Ameongeza.
Hii ni ziara ya kwanza ya Rais Kikwete ya kuaga Nchi wahisani na wenza katika maendeleo na Rais ameanzia Nchi za Nordic kwa sababu ya historia na uhusiano wa Nchi hizi kwa Tanzania tangu kupata Uhuru wake.
Rais Kikwete anaendelea na ziara yake nchini Sweden ambapo anatarajia kufanya mazungumzo na wafanyabiashara na wawekezaji mbalimbali kwa lengo la kuwahamasisha kuja kuwekeza nchini Tanzania.