Lowassa Ataka Wanaomchukia Ndani ya CCM Wahame Chama

Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari, nyumbani kwake, Dodoma jana.

Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari, nyumbani kwake, Dodoma jana.


WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa hana mpango wa kuhama Chama Cha Mapinduzi (CCM) na iwapo kuna mtu anamchukia ndani ya chama hicho, ni vyema akahama kwa sababu yeye hana mpango huo. Lowassa alitoa kauli hiyo alipozungumza na wahariri wa vyombo vya habari nyumbani kwake mjini Dodoma jana ambako alieleza mambo mbalimbali kuhusu afya yake, suala la Richmond, elimu, ajira, utajiri wake na hali ya kisiasa kwa ujumla.

Hata hivyo, Mbunge huyo wa Monduli hakutaka kujibu maswali mengi kwa madai kuwa atazungumza Jumamosi mjini Arusha atakapotangaza nia yake ya kugombea urais.

Kuhama CCM
Alipoulizwa iwapo yupo tayari kuhama CCM na kwenda upinzani asipopitishwa na chama hicho kuwania urais alisema: “Sina mpango wa kuhama chama changu, sina plan B, mimi ni plan A tu, tangu nimemaliza Chuo Kikuu mwaka 1977 nimekuwa mwana-CCM, sijafanya kazi nje ya CCM ukiondoa miaka ambayo nilikuwa vitani Uganda na nilipohamishiwa Kituo cha Mikutano cha Arusha (AICC). Maisha yangu yote yapo CCM.

“Kama kuna mtu ambaye hanitaki ndani ya CCM, yeye ndiye ahame, siyo mimi,” alisema.

Kimya miaka saba
Lowassa aliyejiuzulu uwaziri mkuu mwaka 2008 kutokana na kashfa ya mtambo wa kufua umeme wa Richmond, alisema kimya chake baada ya tukio hilo kilitokana na siasa nyingi za uhasama na kutishiana.

“Kwa miaka saba, niliona ni hekima kunyamaza, askofu mmoja alinifundisha kuwa ukimya ni hekima kutoka kwa Mungu. Nilichagua kuwa kimya. Nilinyamaza kwa sababu ilikuwa salama kunyamaza, ningezungumza ningeweza kutibua mambo kwenye nchi na kusababisha mambo ambayo hayapo.

“Nilinyamaza ili kuipa muda Serikali ifanye kazi yake…. sikupenda kuzungumza kwa sababu ya siasa nyingi za uhasama na kutishiana kwingi, kuna kusingiziana kwingi, kufitiniana kwingi. Kukaa kimya ni jambo gumu sana kwa mwanasiasa, lakini nashukuru Mungu niliweza hilo,” alisema Lowassa ambaye Jumamosi atatangaza nia ya kuwania urais mjini Arusha.

Wagombea wapime afya
Alipoulizwa kuhusu madai kuwa afya yake inaterereka, alisema anaamini yupo fiti na akashauri wagombea urais wote wakapimwe.

“Hata nikikimbia kilomita 100 watasema mimi mgonjwa. Hivi karibuni nilitembea kilomita tano na albino jijini Dar es Salaam, kuna watu wakasema nimechoka sana, nimepata ‘stroke’ na nimekimbizwa Ujerumani kutibiwa, huo ni upuuzi mtupu. Kuna chuki imeingia katika siasa zetu na kutakiana mabaya. Afya ni neema kutoka kwa Mungu tu. Napenda kuwahakikishia kuwa nipo fiti na nipo fiti na kwa lolote. Nadhani ni wakati sasa kwa chama chetu waweke utaratibu wanaogombea nafasi hii ambayo nitaitangaza Jumamosi, tukapime wote afya na mimi nitakuwa wa kwanza kujitokeza kwenda kupima.

“Twendeni tukapime tuone nani mgonjwa. Tuonane kwenye uwanja wa mapambano katika mchakamchaka wa maendeleo, ninajua nitawashinda kwa mbali,” alisema.

Sakata la Richmond
Kuhusu sakata la Richmond, ambalo lilimfanya ajiuzulu uwaziri mkuu, Lowassa alisema tatizo kubwa halikuwa kuhusu mitambo hiyo ya umeme ila uwaziri mkuu.

“Ajenda haikuwa kuhusu Richmond, ila uwaziri mkuu ndiyo maana niliwaachia. Tunajifunza nini katika hilo, wakubwa wawili wa Marekani, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje (Hillary) Clinton na Rais wake (Barack) Obama, wote wamekuja Tanzania na wamethibitisha kuwa ile mitambo ni mizuri. Lakini jingine tulilojifunza katika ubishi ule umeisababisha nchi hasara ya Dola 120 milioni,” alisema Lowassa.

“Moja ya ushauri wangu wakati ule ilikuwa ni kutaka kuvunja mkataba wa Richmond nikaita wataalamu, nikawaelezea kuhusu habari za magazeti kuwa zinasema hawa jamaa (Richmond) hawana fedha, hebu angalieni, nikaita wataalamu na mwanasheria mkuu, nikawaambia kuna hii habari kuweni makini, pamoja na hayo nikaweka kwa maandishi kwa mwanasheria mkuu, pia kulikuwa na timu ya mashauriano ya Serikali iliyokuwa chini ya makatibu wakuu nao walikuwa na vikao vyao, ilikuwa inaongozwa na (Katibu Mkuu Wizara ya Fedha (Gray Mgonja) nao wakakutana chini ya Katibu Mkuu Kiongozi na baada ya kukutana wakatoa uamuzi ambao sina haja ya kuujadili. Lakini ubishi ule umetugharimu Dola 120 milioni.

“Nilipotaka mkataba uvunjwe nilikuwa nimetoa uzoefu wangu kwani kabla ya kuwa waziri mkuu nilikuwa nimekuwa waziri wa maji na mifugo ambako nilivunja mkataba wa kampuni ya Kiingereza iliyokuwa imewekeza katika mradi wa maji Dar es Salaam ya City Water.

“Chini ya uongozi wa Rais (Benjamin) Mkapa tukagundua hawa jamaa (City Water) ni matapeli…tulifanya kikao saa tisa alasiri, tukachukua kibali cha kumkamata yule Mzungu wa City Water na tukamfukuza akaondoka siku hiyohiyo kwa ndege kurudi kwao, tulifanya saa tisa alasiri ili asiende mahakamani kupata zuio, kwa hiyo tulivizia muda huo ili asije kwenda kupata zuio.

Nini tofauti ya Lowassa nje ya Serikali na ambaye angeendelea kuwa waziri mkuu na kisha kugombea urais? “…Naamini kuwa kama tungeanza kwa kasi ile tuliyoanza nayo nikiwa waziri mkuu, sasa ningepita napunga mkono ningepata kura zote… lakini kinachonisikitisha tumekuwa hatufanyi maamuzi magumu au rahisi, kila kitu kinakwenda legelege. Rais amefanya jitihada kubwa, lakini kuna mambo katika nchi hayaendi, matokeo yake Uganda, Kenya na Rwanda zinatupita sasa, haifai, lakini nawaachia uhondo nitaelezea vizuri Jumamosi, Arusha.”

Elimu au kilimo kwanza?
Akizungumzia kuhusu kupingana na kaulimbiu ya Serikali ya ‘Kilimo Kwanza’, Lowassa alisema ataendelea kushikilia msimamo huo kwa sababu elimu ndiyo kila kitu katika maisha ya mwanadamu.

“Mimi sikubaliani na wenzangu wanajua, sikubaliani na kilimo kwanza, naamini ‘elimu kabla, kilimo kwanza baadaye’. Tukitaka nchi yetu ipige hatua ni lazima tuwekeze katika elimu… Nchi zote za mashariki ya mbali waliwekeza katika elimu, kuna shule za kata hazina walimu, lazima tuwekeze kwenye elimu ili tujikomboe,” alisisitiza.

-KUSOMA ZAIDI HABARI HII:- http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Lowassa–Asiyenipenda-CCM-ahame/-/1597296/2729628/-/item/1/-/632sxdz/-/index.html