Na Mwandishi Wetu, Igunga
MCHAKATO wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa kura za maoni kuteua majina ambayo yatawasilishwa katika kikao cha Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Igunga ili kuteua jina la mgombea wa ubunge kwa tiketi ya chama hicho Jimbo la Igunga, umeingia dosari baada ya baadhi ya wanachama kunaswa na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) eneo hilo wakipeana rushwa.
Taarifa kutoka eneo ambalo uchaguzi huo ulikuwa ukifanyika katika Ukumbi wa St. Leo zinasema TAKUKURU waliwatia mbaroni wanachama watatu wa CCM ambao walidaiwa kukutwa wakigawana mlugula uliotolewa na mmoja wa wagombea katika kinyang’anyiro hicho.
Vyanzo vya habari vinaeleza TAKUKURU walishtukia mchezo huo baada ya kubaini kulikuwa na baadhi ya wapigakura wakitaarifiana mmoja baada ya mwingine na kutoka nje kugawiwa fedha na kurudi ukumbini, ndipo maofisa hao walipofanikiwa kuwatia mtegoni wanachama watatu na kuwashikilia.
Hata hivyo Kamanda wa TAKUKURU wilaya ya Igunga, John Ngunangwa alipotakiwa kutoa ufafanuzi juu ya suala hilo aliomba apewe muda ili waweze kulifanyia kazi kabla ya kutoa taarifa kamili hapo baadaye.
Taarifa kutoka kwa wajumbea wazalendo wameudokeza mtandao huu kuwa uchaguzi huo ulitawaliwa na mazingira ya rushwa kwa baadhi ya wagombea nafasi hiyo kuwatongoza wajumbe tangu juzi usiku wakitaka kuwagharamia masuala mbalimbali kinyemela.
Mbali na tuhuma hizo Wajumbe hao wa Mkutano Mkuu Wilaya (CCM) walifanikiwa kuendelea na mchakato wa kuwapata wagombea wake, ambapo ilipata majina matatu kati ya wagombea wagombea 13 waliojitokeza kuomba ridhaa ya kupitishwa ili kuwa wagombea wa nafasi hiyo.
Akisoma matokeo ya kura hizo, Katibu wa CCM Wilaya ya Igunga, Neema Adamu alisema mgombea aliyeongoza kwa kura nyingi katika uchaguzi huo alikuwa ni Dk. Peter Kafumu ambaye alijizolea kura 588. Aidha alisema alifuatiwa na Japhary Omary aliyejinyakulia kura 193 na kufuatiwa na Shamus Brahamu aliyepata kura 38.
Tayari Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimewapitisha Joseph Mwandu, Isabela Maselemo pamoja na Juma Chacha kama wagombea wake, ambao watachujwa na vikao vya juu kabla ya kupitishwa jina moja kugombea jimbo hilo.