Longo longo za upatikanaji umeme nchini zaendelea

Waziri wa Nishati na Madini

TAARIFA YA SERIKALI KUHUSU HALI YA UMEME NCHINI, WIKI HII

Taarifa hii imewasilishwa jana bungeni Dodoma

Mheshimiwa Spika, jana asubuhi, baada ya kipindi cha maswali na majibu kumalizika, Mheshimiwa Ezekiah Dibogo Wenje, Mbunge wa Nyamagana, alisimama kuomba Mwongozo wako, na akatoa taarifa kwamba kuna ukosefu mkubwa wa umeme katika Jiji la Mwanza kwa muda wa siku nne. Pia alieleza kuwa hali hiyo inahusu Miji ya Kigoma, Arusha, Mbeya na maeneo mengineyo ya Jiji la Dar es Salaam. Kwa kuzingatia tatizo hili Mheshimiwa Mbunge aliomba jambo hili lijadiliwe, na wewe Mheshimiwa Spika katika kutoa mwongozo wako ukaiagiza Serikali itoe maelezo hapa Bungeni.
Mheshimiwa Spika, naomba kwa niaba ya Serikali nitoe taarifa hiyo kama ulivyoagiza. Napenda kuthibitisha kwamba ni kweli kumekuwa na upungufu wa umeme katika miji hiyo kama ilivyoelezwa na Mheshimiwa Mbunge. Kiini cha tatizo hili ni kupungua kwa Megawati zisizopungua 200 kwa sababu nitakazozitaja hapa chini:
Mheshimiwa Spika, Mfumo wa gridi ya Taifa umekumbwa na matatizo kadhaa, yaliyopelekea uzalishaji wa umeme kuwa mdogo kuliko ilivyotarajiwa hususan tarehe 14 Agosti, 2011 hadi hivi sasa. Kama tunavyofahamu gridi ya Taifa inapata umeme wake kutoka kwenye vyanzo ya maji, gesi asili na mafuta mazito. Vyanzo vya umeme unaotokana na nguvu za maji ni Mtera (MW 80), Kihansi (MW 180), Kidatu (MW 204) New Pangani Falls (MW 68), Hale (MW 21) na Nyumba ya Mungu (MW 2). Vyanzo vya umeme unaotokana na gesi asili ya Songo Songo ni TANESCO Ubungo (MW 100), TANESCO Tegeta (MW 45), Songas (MW 180) na Symbion Power (MW 75). Umeme unaozalishwa kwa kutumia mafuta mazito ni MW 100 kutoka mitambo ya IPTL iliyopo Tegeta, Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, hadi tarehe 12 Agosti, 2011 uwezo wa uzalishaji wa umeme katika gridi ya Taifa ulikuwa ni MW 612, lakini kutokana na hitilafu mbalimbali zilizojitokeza katika kipindi hiki uzalishashi ulipungua kwa MW zisizopungua 200.

Mheshimiwa Spika, Kiini cha tatizo ni kupungua hizo MW 200 kwa pamoja zilizotokana na sababu zifuatazo:-
(i) Umeme unaozalishwa na gesi asili ulipungua kutokana na matatizo ya kiufundi kwenye mitambo ya kuchakata gesi na hivyo kusababisha kiasi cha gesi kilichokuwa kinapatikana kwa ajili ya kuzalisha umeme kupungua. Kiasi cha MW 80 hadi MW 125 hazikuweza kuzalishwa kutokana na matatizo haya.

(ii) Matatizo ya upatikanaji wa mafuta katika kipindi cha mgogoro wa wasambazaji wa mafuta, yalipelekea uzalishaji wa umeme katika mitambo ya IPTL upungue kutoka MW 100 hadi MW 20. Kwa mitambo hiyo ya IPTL, matatizo ya kiufundi katika mitambo miwili pia yalichangia kupunguza uzalishaji kwa MW 20.

(iii) Mwisho kwa sababu ya ukame unaoendelea, uzalishaji wa umeme kutokana na vyanzo vya maji haujaboreka, hususan mabwawa yote, yaani Mtera, Kihansi na New Pangani Falls, imelazimu kusimamisha au kupunguza uzalishaji kwa baadhi ya vituo hivi ili kufanya ponding yaani zoezi la kukinga maji kwa muda ili kuwezesha mitambo kufanya kazi kwa ufanisi. Zoezi hili liliathiri uzalishaji wa umeme katika kipindi hiki kifupi kwa wastani wa uzalishaji kama wa MW 20.

Mheshimiwa Spika, Shirika la TANESCO limeendelea kufanya juhudi za kukabiliana na matatizo haya ili kuhakikisha hali ya upatikanaji wa umeme inaimarika na unafuu unaanza kupatikana kwa kuchukua hatua zifuatazo:

(i) Kwa upande wa IPTL, kufuatia kuboreka kwa upatikanaji wa mafuta, ufuaji wa umeme katika mitambo hiyo umeongezeka hadi kufikia MW 80 jana mchana kutoka zile MW 20 nilizozitaja awali. Aidha, kutokana na matengenezo ya mitambo yenye hitilafu yanayoendelea hivi sasa matarajio ni kuwa ifikapo Jumapili, tarehe 21 Agosti, 2011, kazi ya kurekebisha hiyo mitambo miwili itakuwa imekamilika na MW 20 zilizosalia kwenye mitambo ya IPTL zitakuwa zimepatikana.

(ii) Kwa upande wa umeme unaotokana na gesi asili, mafundi wa Pan African Energy wameendelea na ukarabati wa mitambo ya kuchakata gesi kule kisiwani Songo Songo hadi jana usiku na matengenezo yanaendelea hadi hivi sasa. Ukarabati wa mitambo hiyo kwa hatua iliyofikiwa hadi jana usiku imeongeza upatikanaji wa gesi ambao umeweza kuongeza uzalishaji wa umeme kwa MW 80 hadi sasa. Umeme kwa kile kiwango cha MW 125 zilizokuwa zimetoka unatarajiwa kurejea katika mfumo wa gridi ya Taifa wakati wowote leo.

(iii) Kwa upande wa umeme unaotokana na vyanzo vya maji, hakuna maelezo ya ziada. Hali ya maji yanayoingia kwenye mabwawa bado siyo ya kuridhisha, jitihada za kukinga maji kwa maanda ya ponding ili kupanga umeme wa kuzalisha kwa kiwango cha juu zaidi zinaendelea. Hivyo basi, vyanzo vya maji kwa kipindi kijacho vinatazamiwa kuzalisha umeme kwa kiwango kidogo cha wastani wa asilimia 20 kwa uwezo wa mitambo yetu yote vituo vyetu vyote vya maji. Kwa kipindi hiki hadi hapo Mwenyezi Mungu atakapojalia mvua ya kutosha kuongeza kina cha maji kwa kiwnago cha kuridhisha zoezi hili la ponding litakuwa linaendelea mara kwa mara.

Mheshimiwa Spika, kama tulivyoeleza wakati wa kuhitimisha mjadala wa makadirio na matumizi ya Wizara tarehe 13 Agosti, 2011, kulingana na mpango wa dharura uliowasilishwa humu Bungeni, katika kipindi hiki cha Agosti, tunatarajia kupata nyongeza ya uzalishaji kwenye gridi ya Taifa kama ifuatavyo:

(i) Kwa upande wa Symbion, kampuni hiyo inakamilisha taratibu za kuzalisha Megawati 37 za ziada kwa kutumia mafuta ya ndege. Symbion imetuhakikishia kuwa ifikapo Jumapili hii keshokutwa tarehe 21 Agosti, 2011 kiasi hicho cha umeme kitakuwa kimepatikana ndani ya gridi ya Taifa.

(ii) Kampuni ya Aggreko nayo inaendelea na kazi ya ufungaji wa mitambo, pamoja na kazi ya kuunganisha mitambo hiyo kwenye mfumo wa kupeleka mafuta kutoka kwenye matanki ya kuhifadhia, (storage tanks). Matarajio yetu ni kwamba kabla ya mwisho wa mwezi Agosti, MW 50 za kwanza kati ya MW 100 zilizopangwa kuzalishwa na Aggreko, zitakuwa zimeingia kwenye gridi ya Taifa. Ifikapo tarehe 1 Oktoba, 2011 tunatarajia MW 100 zinazokusudiwa kuingia kwenye gridi ya Taifa kutokea Aggreko zitakuwa zinazalishwa zote.

Mheshimiwa Spika, hali hiyo niliyoeleza huko juu ndiyo iliyosababisha ukali wa mgawo wa umeme ukarudi siyo tu kwenye Miji ya Mwanza, Mbeya, Arusha, na maeneo ya Jiji la Dar es Salaam kama alivyoeleza Mheshimiwa Mbunge, bali katika maeneo yote nchini yanayopata umeme wake kutoka gridi ya Taifa.

Mheshimiwa Spika, katika hali ya upungufu mkubwa huu wa upatikanaji wa umeme, Uongozi wa Shirika la TANESCO ulifanya uamuzi wa kuhakikisha huduma ya umeme inapatikana kwenye maeneo muhimu ya huduma za jamii, yakiwemo hospitali, vyuo, mitambo ya kusukuma maji na maeneo mengine muhimu kwa jamii.

Mheshimiwa Spika, kwa Mji wa Mwanza, upatikanaji wa umeme vile vile ilibidi uelekezwe katika maeneo ya hospitali za Bugando na Sekoture, kwenye mitambo ya kusukuma pampu za maji na maeneo mengine muhimu kwa kijamii na hivyo kusababisha baadhi ya maeneo ya Mwanza kukosa umeme kwa kipindi hiki.

Mheshimiwa Spika, hadi ilipofika saa kumi mchana jana, maana ile kazi ya matengenezo ilikuwa inaendelea, katika jumla ya mahitaji ya Mwanza ya MW 42 upatikanaji umeme ulikuwa umefikia MW 20, kutoka MW 5 zilizokuwa zinapatikana katika kipindi hiki ambacho Mheshimiwa Mbunge alikuwa ameelekeza.
Mheshimiwa Spika, naomba nitumie muda huu pia kusema kwamba katika muda huu wa saa kumi jioni ya leo uzalishaji Mwanza umetoka kwenye MW 20 zile masaa 24 iliyopita na hivi sasa iko kwenye MW 32 mpaka 34 kati ya kiwango cha mahitaji ya MW 42 ambazo ndiyo mahitaji ya juu ya Mwanza.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hali pia ya upatikanaji wa umeme inaendelea kuboreka katika miji ya Dar es Salaam, Mbeya, Arusha na miji mingine nchini inayopata umeme kutoka kwenye gridi ya Taifa kadri upatikanaji wa umeme unavyokuwa unazidi kuongezeka.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Mji wa Kigoma, kwa taarifa nilizokuwa nazo, jana kulikuwa hakuna tatizo la kutokuwepo kwa huduma ya umeme kama alivyoeleza Mheshimiwa Mbunge. Ninafahamu kwamba matatizo yaliyokuwepo Kigoma ni ya kipindi tofauti na hiki alichoeleza Mbunge. Matatizo yaliyotokea Kigoma ni ya wiki iliyopita, kati ya tarehe 05 na 13 Agosti, 2011, na yalitokana na tatizo la upatikanaji wa mafuta lililotokana na mgomo wa wasambazaji wa mafuta. Tatizo hili lilimalizika tarehe 13 Agosti, 2011 mafuta yalipowasili na uzalishaji kurejea katika hali yake ya kawaida.

Kwa maana hiyo, matatizo yaliyokuwepo Kigoma ni matatizo yaliyovikumba vituo vyote vilivyo nje ya Gridi ya Taifa vinavyoendeshwa kwa mafuta, kama vile Mpanda, Songea, Tunduru, Loliondo na vituo vinginevyo ambavyo chimbuko lake ni ule mgogoro uliosababishwa na wasambazaji wa mafuta ndiyo ikatokea ile breakdown ya supply kwenye vituo hivyo. Shirika letu la TANESCO linaendelea na jitihada za kuhakikisha kwamba mafuta ya kuendeshea mitambo yanapatikana kwa wakati ili kuhakikisha huduma hii muhimu inapatikana wakati wote katika vituo hivi.

Mheshimiwa Spika, niseme naomba kwa niaba ya TANESCO kukiri na kuwaomba radhi Watanzania, kwamba ni kweli pamoja na kwamba matukio haya yametokea ghafla, na kwa pamoja, lakini bado nasisitiza kwamba TANESCO, ilikuwa inawajibika kutoa taarifa kwa Umma mapema, ili Watanzania wafahamu kinachoendelea na hatua zinazochukuliwa kukabiliana na matatizo haya.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo baada ya maelezo hayo naomba kuwasilisha.