Na Mwandishi Wetu
KILA timu inayoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania inatarajia kupewa jumla ya sh. milioni 26.3, fedha zitakazotumika kama gharama ya klabu katika mashindano hayo.
Akizungumza na vyombo vya habari jana Dar es Salaam, Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema fedha hizo zitatolewa kwa awamu tano tofauti kuanzia mwezi huu.
Aidha Wambura alisema kwa Agosti kila timu itapata sh. 4,732,142, Septemba (sh. 4,732,142), Oktoba (sh. 5,622,321), Januari (sh. 5,622,321) na Machi (sh. 5,622,321). Jumla ya fedha kutoka kwa mdhamini wa ligi, Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom ambazo zitatumika kwa ajili ya nauli kwa timu zote katika msimu mzima ni sh. 368,637,458.
Wakati huo huo; TFF imesema imeiandikia barua Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuomba iruhusu mechi ya mchujo ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika mwakani Equatorial Guinea na Gabon, kati ya Taifa Stars na Algeria (Desert Warriors) ichezwe Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
“Ombi letu limetokana na ukweli kuwa tulishaliarifu Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) miezi mitatu iliyopita kuwa mechi hiyo itachezwa katika uwanja huo. Taarifa hiyo pia tuliipa Algeria ambayo imeshatuma ujumbe wake kukagua hoteli ambayo timu yao itafikia,” alisema Wambura.
Aliongeza kuwa kwa upande wa CAF uamuzi wa kubadili uwanja hivi sasa utaigharimu TFF, kwani itapigwa faini, na vilevile TFF kulazimika kuingia gharama za kusafirisha timu zote mbili kwa ndege pamoja na waamuzi kwenda Mwanza kwa ajili ya mechi hiyo.