Msimu mpya Ligi Kuu kuanza kesho, timu 10 kupambana

Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura

Na Mwandishi Wetu

MSIMU mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom 2011/12 unaanza kesho, Agosti 20 mwaka huu, ambapo timu 10 kati ya 14 zinazoshiriki katika ligi hiyo zitakuwa viwanjani. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Dar es Salaam na Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura amezitaja mechi za kesho ni pamoja na Coastal Union Vs Mtibwa Sugar (Mkwakwani, Tanga), Kagera Sugar Vs Ruvu Shooting (Kaitaba, Bukoba), Toto Africans Vs Villa Squad (Kirumba, Mwanza) na Polisi Dodoma Vs African Lyon (Jamhuri, Dodoma).

Wambura amesema zngine ni Azam Vs Moro United itakayochezwa Chamazi, Dar es Salaam huku mechi za Jumapili, Agosti 21 mwaka huu ni Oljoro JKT Vs Simba (Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha), na Yanga watakaokuwa wenyeji wa JKT Ruvu.

Ofisa Habari huyo amesema jumla ya waamuzi wa kati 16 wameteuliwa kuchezesha Ligi Kuu. Amewataja waamuzi hao ni Ronald Swai (Arusha), Isihaka Shirikisho (Tanga), Peter Mujaya (Mwanza), Amon Paul (Mara), Mathew Akrama (Mwanza), Ibrahim Kidiwa (Tanga), Dominic Nyamisana (Dodoma), David Paul (Mtwara), Hashim Abdallah (Dar), Martin Saanya (Morogoro), Orden Mbaga (Dar), Kennedy Mapunda (Dar), Israel Mujuni (Dar), Alex Mahagi (Mwanza), Abdallah Kambuzi (Shinyanga) na Thomas Mkombozi (Kilimanjaro).

Aidha aliongeza waamuzi wa akiba sita ambao watatumika wakati wowote watakapohitajika, huku waamuzi wasaidizi walioteuliwa kuchezesha ligi ni 34. Kwa upande wa waamuzi wasaidizi wa akiba walioteuliwa ni kumi, hivyo kufanya jumla ya waamuzi watakaotumika kwenye ligi hiyo kufikia 50.

Hata hivyo amewataja jumla ya makamishna 24 wameoteuliwa kusimamia mechi za ligi hiyo. Kati ya hao 20 wakiwa wa zamani na wanne ni wapya. Makamishna wapya ni Charles Ndagala, Victor Mwandike, Godbless Kimaro na Hamis Tika.

Makamishna wa msimu uliopita walioteuliwa tena ni Hamis Kissiwa, David Lugenge, Abdallah Mitole, Charles Komba, George Komba, Jimmy Lengwe, Amri Kiula, James Mhagama, Fulgence Novatus, Pius Mashera, Michael Bundara, Gabriel Gunda, Mohamed Nyange, Mwijage Rugakingira, Arthur Mambeta, Paul Opiyo, Edward Hiza, Salim Singano, William Chibura na Omary Mwamela.

Uteuzi wa makamishna kama ilivyo kwa waamuzi ulifanyika baada ya kuhudhuria kozi na kufanya mitihani. Kwa upande wa makamishna ambao hawakufanya vizuri, watalazimika kurudia mitihani kabla ya kuteuliwa tena.