CHADEMA yazuiwa kufanya mikutano

Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willbrod Slaa

Na Janeth Mushi, Arusha

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha imetoa umauzi mdogo wa kuzuia kwa muda mikutano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
kwa kile mikutano hiyo kuwazungumzia madiwani wake watano waliofukuzwa uanachama hivi karibuni.

Mahakama imesema hata kama CHADEMA itapewa kibali cha kufanya mikutano basi kitakuwa na masharti ikiwemo kutolizungumzia suala la madiwani hao na kutotoa lugha chafu na vitisho hadi kesi ya msingi itakapoanza kusikilizwa.

Hakimu wa Mahakama hiyo, Hawa Mguruta ametoa uamuzi huo baada ya madiwani hao kufungua kesi ya msingi ya madai Agosti 10 mwaka huu yenye namba 17/2011 wakipinga hoja mbalimbali.

Kwa mujibu wa Mguruta mahakama hiyo imetoa uamuzi mdogo kutokana na sababu za msingi walizozitoa madiwani hao ambao ni Estomii Mallah Diwani wa Kimandolu (Naibu Meya), John Bayo (Elerai), Ruben Ngowi ( Themi), Rehema Mohamed (Viti Maalum) na Charles Mpanda (Kaloleni).

Alisema viongozi wa CHADEMA wanapokuwa kwenye mikutano yao wasitaje
sababu za madiwani hao kufukuzwa uanachama pamoja na kuwatolea lugha
za matusi zinazolenga kuwadhalilisha, kwani kufanya hivyo kunaweza
kusababisha uvunjifu wa amani kwa mujibu wa sheria.

Mguruta alisema uamuzi huo umetolewa baada ya kupitia madai hayo yaliowasilishwa na umekitaka chama kutokiuka maelekezo hayao kwenye mikutano yake. Na endapo itafanyika basi izungumzie masuala mengine ya wananchi na si suala la madiwani hao ili kuepusha migogoro
ndani ya jamii.

Alisema mahakama imeridhia uamuzi huo mdogo huku ikisubiri kesi ya
msingi kusikilizwa kwa pande zote, ambazo upande mmoja ni
madiwani waliofukuzwa na wa pili ni viongozi wa Chama hicho.

Kwa upande wake Meya wa Jiji la Arusha, Gaudence Lyimo alisema
wamepokea barua ambayo ilipelekwa na viongozi wa CHADEMA juu ya
kuwafukuza uanchama na kutowatambua madiwani wake watano kama
wawakilishi wa chama hicho katika vikao mbalimbali vya madiwani.

Lyimo alisema kuwa baada ya kupokea barua hizo kutoka CHADEMA
wamezituma Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)
wiki moja iliyopita kwa Waziri husika ili azipitie kisha kutoa
uamuzi juu ya suala hilo.