Sekretarieti ya Maadili ‘Yamsafisha’ Maswi, Yasema Hakukosea Sakata la Escrow

Eliakim C. Maswi

Eliakim C. Maswi

Na Mwandishi Wetu

UCHUNGUZI wa Awali uliofanywa na Sekretarieti ya Maadili umebaini kuwa Ndugu Eliakim C. Maswi hana makosa yoyote ya kimaadili katika mchakato wa fedha za akaunti ya Tegeta Escrow hivyo umekabidhi taarifa yake kwa Rais Jakaya Kikwete kutoa uamuzi wa mwisho.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu, Uchunguzi wa Awali uliofanywa na Kamati ya Uchunguzi wa Awali iliyoundwa na Katibu Mkuu Kiongozi umebaini kuwa Ndugu Eliakim C. Maswi, hakutenda au kuhusika na jambo lolote linaloashiria vitendo vya jinai au kukiuka Maadili ya Viongozi wa Umma.

“…Ushahidi wa vielelezo uliotolewa kwenye Sekretarieti ya Maadili na kwenye Kamati ya Uchunguzi wa Awali umejitosheleza kuthibitisha kwamba Ndugu Eliakim C. Maswi alitenda kazi yake kwa kiwango kinachoridhisha kwa kufanya mawasiliano na mamlaka mbalimbali na kwa nyakati tofauti kwa lengo la kuhakikisha na kujiridhisha kwamba kufungwa kwa Akaunti ya Tegeta Escrow kunafanyika kwa usahihi,” ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa imebainika hakuna ushahidi wowote kuwa Eliakim C. Maswi alikuwa miongoni mwa waliopata mgao wa fedha au fadhila yoyote kutokana na kufungwa Akaunti ya Tegeta Escrow.

“…Kwa nafasi yake ya mamlaka ya nidhamu Katibu Mkuu Kiongozi, ameridhika kuwa Ndugu Eliakim C. Maswi hana makosa yoyote aliyoyafanya katika mchakato wa akaunti ya Tegeta Escrow yanayostahili adhabu. Hivyo, mchakato wa kinidhamu, kimaadili na kijinai dhidi yake umefikia mwisho wake. Mwenye mamlaka ya uteuzi atatafakari taarifa hizi na kuamua cha kufanya kuhusu ajira yake baadaye,” imebainisha taarifa hiyo.

Katika mapendekezo ya Kamati ya Uchunguzi wa Awali, pia imesema; “…haijabaini kosa lolote ambalo linaweza kusababisha Ndugu Eliakim Chacha Maswi, Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, kufunguliwa mashtaka ya kinidhamu kwa kukiuka Sheria ya Utumishi wa Umma Sura 298 ikisomwa pamoja na Kanuni zake za mwaka 2003 kwa kuruhusu Benki Kuu ya Tanzania kutoa fedha zilizokuwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow.”

Katika mkutano wake wa 16 na 17, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na mambo mengine, lilijadili Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali iliyotokana na Taarifa ya Ukaguzi wa Akaunti ya Tegeta Escrow uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Baada ya majadiliano, Bunge lilipitisha maazimio kadhaa yaliyoelekezwa kwa Serikali kwa ushauri na utekelezaji. Mojawapo ya maazimio hayo yalimtaja Ndugu Eliakim C. Maswi, ambaye ndiye Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, kuwa amehusika kijinai au kimaadili katika miamala iliyotokea katika akaunti ya Tegeta Escrow.