Na Silas Severe
“NDUGU zangu wa Watanzania ninatambua kabisa kuwa hili si jukwaa la siasa ila nimeona ni heri niwaletee niliyopata kuyaona katika jukwaa la siasa- kwamba; Kwanini Lowassa anafaa kuwa Rais wa Tanzania?
Kila mtu ana haki ya kutoa maoni yake kwa mujibu wa mawazo yake kwakuwa ana utashi wake binafsi hivyo naomba nitoa mtizamo wangu, na sitatoa maoni ili kumfurahisha mtu ndani ya ‘Forum’ ni maoni yangu na nina haki ya kuwa tofauti au sawa kimawazo na mtu yoyote. EL (Edward Lowassa) anaifaa Tanzania kwa sababu zifuatazo:-
Ni Kiongozi shupavu, jasiri na mwenye ushawishi mkubwa ndani ya chama na Serikali kwa upande wa Serikali hili linadhihirika aliposhika nyazifa mbalimbali kama:-
a) Kusimamia Sekta ya Elimu ambayo ndiyo Uti wa mgongo wa maendeleo ya Taifa lolote hapa duniani. Alisimamia kwa ukakamavu kutekeleza Mpango wa Maendeleo kwa Elimu ya Sekondari (MMES) na alihimiza kwa nguvu zake zote ujenzi wa Shule za Kata Nchi nzima ili kuwapa fursa mamilioni ya Watanzania wenzetu waishio Vijijini kupata fursa ya elimu.
Zoezi hili lilihitaji uwekezaji mkubwa sana na tukumbuke kwamba Taifa letu ni masikini sana, changamoto zilizo ikabili Sekta ya elimu kama Ukosefu wa vifaa vya maabara, nyumba za walimu, madarasa ya Kutosha na upungufu wa vitabu si kosa la mtu fulani bali umasikini wa Taifa letu ndio maana Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF) hutoa misaada kwa nchi masikini kusaidia maendeleo ya Elimu kwa kuwa ni Sekta inayohitaji uwekezaji mkubwa kifedha na rasilimali zingine.
EL ni mtu anayeamini katika elimu ndio maana ‘motto’ wake ni tofauti kidogo na ‘Motto’ wa Chama chake na anasema; “ELIMU KABLA, KILIMO KWANZA.” Ni kweli kabisa kwamba hakuna linaloweza kufanikiwa bila elimu, Unaweza kuwaambia watu wasio na elimu ya kutosha walime Kilimo cha Kisasa? ‘Me I agree’ (mi nakubali) kwamba elimu kabla na Kilimo Kwanza.
Mataifa Makubwa yaliondelea leo duniani yalifanya uwekezaji Mkubwa kwanza katika elimu, hasa Elimu ya Msingi (Kwa mfano China, Brazil na Marekani) na baadaye kufanya ‘Mapinduzi Makubwa ya Kilimo’, baadaye viwanda vidogo, na baadaye viwanda vikubwa ambavyo vilichochea kukua kwa kwa Sekta za huduma na kusababisha mfumuko wa nafasi nyingi za ajira kwa vijana!
b) Kuwafukuza bila woga hadi kuwasindikiza Airport wawekezaji wababaishaji wa Kampuni ya City Water hadi kuwapandisha ndege uwanja wa
Taifa: Akiwa Waziri wa Maji na Maendeleo ya Mifugo, EL alitekeleza wajibu wake kwa umahiri mkubwa na bila woga na moja ya mambo ambayo yatakumbukwa ni kufukuzwa kwa wawekezaji wababaishaji wa Kampuni ya Kitapeli ya City Water ambao walishindwa kutekeleza wajibu wao, aliwatimua na kuwasindikiza hadi Airport! EL ni Kiongozi Shupavu sana na asiyeogopa mtu!
c) Kiongozi mwajibikaji na asiyeogopa kufanya uamuzi mgumu hata kama utamuumiza. Kujiuzulu kwake kutoka katika wadhifa wake wa U-waziri Mkuu kufuatia kashfa ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond inachukuliwa na wengi kama kuhusika kwake katika Saga hilo. Napenda kuwakumbusha Watanzania wenzangu kwamba Waziri Mkuu ndiye Mtendaji Mkuu wa Shughuli za Serikali na Mtekelezaji wa Maagizo ya Baraza la Mawaziri, ambacho kimsingi ndicho chombo kikubwa cha Utendaji wa Serikali (Govt. Machine) na hivyo kama kuna kosa linafanyika basi linatosha kuiangusha Serikali nzima. Katika tukio lile ilibidi Serikali nzima akiwemo Rais wajiuzulu, lakini EL alikubali mwenyewe kwa ajili ya kulinda heshima ya Chama chake na Serikali, huu ni mfano mzuri wa kuigwa kwa Waafrika wote.
Siku zote tatizo letu Waafrika ni kukosa kuwajibika pale inapobainika uzembe umefanyika. Ukweli umebaki kuwa wazi hadi leo ndiyo maana ‘NCHI IPO GIZANI’ mgawo ya umeme unaendelea kama kawaida na dada wa Richmond ambaye ni Dowans mitambo yake inawashwa na tumerudi pale pale! Mimi nasema kwa kosa la Richmond, Serikali nzima ilikuwa imeanguka.
d) Mfuatiliaji na asiyechoka kufuatilia kero za wananchi, hakai ofisini kungoja taarifa. Wakati wa baa la njaa lilisababishwa na ukame kwa msimu wa mwaka 2007/08 ni huyu EL alikuwa akishirikiana na Wakuu wa Wilaya zote zenye njaa na wakati mwingine alishiriki yeye mwenyewe kupita nyumba kwa nyumba kusimamia zoezi la ugawaji wa chakula kwenye familia zenye njaa, ili kuhakikisha kwamba azma ya Serikali ya kwamba hakuna mwananchi atakayekufa kwa njaa inatimizwa-ni huyu huyu EL.
Mtu hawezi kukosa mapungufu hata siku moja, nakubali ana mapungufu yake lakini EL ni ’embe dodo’ lililoiva tayari kuvunwa na Watanzania mwaka ukifika 2015.