Hali ya wakili anayedaiwa ‘kutapeli’ mabilioni bado tete, kesi yaendelea

Na Janeth Mushi, Arusha

WAKILI maarufu mkoani hapa Mediam Mwale, ambaye juzi alisomewa
mashitaka 13 ya kuhujumu uchumi na kughushi nyaraka na kujipatia
fedha sh. bilioni 18 kinyume cha sheria bado anaendelea kusota
wodini katika hospitali ya Mkoa ya Mt.Meru kwa matibabu kutokana na
hali yake kutokuwa nzuri kiafya.

Mwale aliyesomewa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya
Mkoa wa Arusha, Charles Magesa na Mwendesha mashitaka wa Serikali,
Fredrick Manyanda.

Akisoma hati ya mashitaka hayo alidai kuwa mshtakiwa katika kosa la
kwanza na la pili la kughushi alifanya Januari 6 mwaka jana 2010 na
Januari 13 mwaka jana kwa kuhamisha fedha kutoka kampuni za tofauti
ambazo ni kampuni ya Olive Green, Nyamao Mbeche Hollo, Gregg
Motachwa, Ogembo Meetchel, John Adam na Mosoto Haye.

Alidai kuwa kosa la tatu hadi la 13 ni la kuhujumu uchumi ambalo
alifanya Februari 16 mwaka jana, ambapo alihamisha fedha zaidi ya
sh. bilioni 1.9 kutoka kampuni ya Ogembo Chacha na Gregg Motachwa Mwita.

Alidai kuwa katika kosa la nne, mnamo Machi 5 mwaka jana, alihamisha
fedha za kimarekani dola 200,000 na kosa la tano alitenda machi 30,
ambapo alihamisha fedha za kimarekani dola 159,500 na kosa la sita
mnamo Septemba 27 alihamisha fedha za kimarekani dola 5,500.

Mtuhumiwa huyo anadaiwa kutenda kosa la saba Novemba 2 mwaka jana,
ambapo alihamisha fedha za kimarekani dola, 1,246,624.84, kosa la nane
mnamo Desemba 21 mwaka jana, alihamisha fedha za kimarekani dola,
416,000.02 na kosa la tisa mnamo Desemba 24 alihamisha fedha za
kimarekani dola 521,000.

Manyanda aliendelea kutaja kuwa kosa la kumi alitenda mnamo Januari 7
mwaka huu 2011, ambapo alihamisha fedha za kimarekani dola, 808,000.02, kosa la kumina moja mnamo Februari 9 mwaka huu, alihamisha fedha za Kimarekani 527,000.02, kosa la 12 alitenda mnamo Julai 13 mwaka huu, alihamisha fedha zakitanzania sh. milioni 330,000,000 na kosa la 13 alitenda mnamo Julai 14 mwaka huu, kwa kuhamisha sh. milioni 250.

Mashitakiwa huyo alikana mashitaka hayo na wakili upande wa utetezi
unaoongozwa na Loum Ojare, aliomba Mahakama kuruhusu kukabidhiwa vitu
vinavyoshikiliwa na Polisi kwa sababu havipo katika hati ya mashitaka
ambavyo ni magari na simu za kiganjani na mahakama iliruhusu.

Awali mshitakiwa alifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha Agosti 9
mwaka huu na kusomewa mashitaka 13 ya kuhujumu uchumi na kughushi
nyaraka na baada ya hapo mshitakiwa alipatwa na msongo wa mawazo na
kulazwa hospitali ya Mkoa Mount Meru, ambako amelazwa hadi leo.