Na Eleuteri Mangi
Wanafunzi wa shule ya sekondari ya Jangwani wameaswa kutumia muda wao vema wakiwa shuleni kwa kuwekeza kwenye elimu ambayo inasaidia kumbadilisha mtu na hatimaye kubadilisha jamii nzima.
Kauli hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi Mtendaji wa Tausi Dreams Foundation Tausi Likokola alipokuwa mgeni rasmi wakati wa mahafali ya wanafunzi wa kidato cha sita katika shule ya sekondari Jangwani iliyopo manispaa ya Ilala Jijini Dare s salaam.
“Ukizaliwa mwanamke, tambua kuwa wewe ni kiongozi wa kwanza katika jamii, hivyo tumia vipaji vyako kama ulivyojaliwa na Mwenyezi Mungu ukizingatia suala la nidhamu ambayo ndiyo msingi wa mafanikio yote yatakayowasaidia katika maisha yenu ndani ya jamii” alisema Tausi.
Tausi alisisitiza kuwa watu wengi duniani wanaofanikiwa wanaongozwa na nidhamu bora waliyonayo ambayo imewasaidia kufikia malengo yao waliyojiwekea, wanafunzi hao wametakiwa kuiga mfano huo ili waweze kufanikiwa maisha yao kwa manufaa yao binafsi, jamii na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya sekondari Jangwani Geraldine Mwanisenga alipokuwa akitoa taarifa fupi ya shule kwa mgeni rasmi wakati wa mahafali hayo alisema kuwa shule yake ni miongoni mwa shule kongwe nchini ambazo zinazofanya vizuri kitaaluma na masuala mengine yasiyo ya kitaaluma.
Kuhusu taaluma, Mkuu huyo alisema kuwa shule yake imeendelea kufanya vizuri na kushika nafasi ya juu katika matokeo ya mitihani ya taifa ambapo mwaka huu imeshika nafasi ya kwanza kwenye matokeo ya kidato cha nne miongoni mwa shule za sekondari za serikali katika Mkoa wa Dar es salaam.
Mkuu huyo wa shule alisema kuwa siri kubwa ya mafanikio yao inatokana na kujiweka malengo, mikakati na kuhakikisha vyote inatekelezwa kwa wakati.
Miongoni mwa mikakati hiyo ni kufundisha masomo ya ziada na rekebishi, kutoa motisha kwa walimu na wanafunzi wanaofanya vizuri katika masomo, ushirikiano baina ya Bodi ya shule, wazazi, wafanyakazi wanafunzi na wadau wengine wa elimu ikiwa ni chachu ya mafanikio ya shule.
Aidha, Mkuu wa shule mwalimu Geraldine amewaasa wahitimu hao watumie elimu waliyoipata wakiwa shuleni hapo kama silaha ya ukombozi kwenye jamii, maana jamii inahitaji wasomi ili kuikomboa kifikra, kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Naye mwanafunzi aliyepata vyeti mbalimbali vya taaluma takribani saba kwa kufanya vizuri katika masomo ya Kemia, Biyolojia, Fizikia, Hesabu, cheti cha kuwa mwanafunzi bora katika masomo, uongozi, uongozi bora pamoja na zawadi Rosemary Mushi alibainisha kuwa ilikuwa ndoto yake kuja kuwa mwanafunzi bora maana alipokuwa kidato cha nne zawadi hiyo ilienda kwa mwanafunzi mwingine ambapo hatua hiyo ilimpa hamasa ya kusimamia azma yake kwa moyo wote.
“Leo ninafuraha sana maana ilikuwa ndoto yangu kuja kuchukua vyeti vyote ambapo ilinilazimu kusoma sana na kufaulu vizuri ili nifikie ndoto yangu ya maisha ya kuwa daktari wa watoto” alisema Rosemary.
Rosemary aliushukuru uongozi wa shule, walimu, wafanyakazi wasio walimu na wanafunzi wenzake kwa ushirikiano mzuri alioupta kutoka kwao wakati wote alipohitaji masaada wao ili kufikia malengo yake ya kufaulu vizuri masomo yake na kumuwezesha kusonga mbele katika hatua nyingine ya elimu.
Shule ya sekondari Jangwani ilianzishwa kwa historia ya kuwekwa jiwe la msingi liliwekwa mnamo Mei 28, mwaka 1928 na Kiongozi Mkuu wa ukoloni wa Mwingereza wakati huo Sir Donald Cameroon na kuifanya shule hiyo kuwa na umri wa miaka 87 ambapo kwa sasa ina jumla ya walimu 102, wafanyakazi wasi walimu 21, wanafunzi 1150 miongoni mwao wanafunzi 70 ni wenye mahitaji maalum kulingana na mahitaji ya sera ya elimu chini ya mtaala wa elimu jumuishi uliohimiza kusomesha wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Mwisho.