Na Kibada Kibada – Katavi
MAKAMU Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania, Profesa Tolly Mbwete ametoa msaada wa shs milioni 45 kwa ajili ya kununulia eneo lenye ukubwa wa ekari 85 kwa ajili ya ujenzi wa Koleji ya chuo tawi la Mkoa wa Katavi. Prof. Mbwette alieleza kuwa katika kuhakikisha suala la maendeleo ya elimu linakuwa ameamua kusaidia kununua eneo litakalotumika kujengwa chuo kwa ajili ya wanajumiya ya chuo hicho mkoani Katavi.
Akizungumza na wanajumuiya chuo hicho katika hotuba yake aliyoaitoa mwishoni mwa wiki katika hafla fupi iliyoandaliwa na wanajumuiya ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania tawi la Mkoa kwa ajili ya kumuaga baada ya kumaliza muda wake alisema amefurahishwa na ushirikiano uliooneshwa na wana Katavi kwa jinsi walivyomkarimu na kumzawadia zawadi ambazo zilimfurahisha na kusema amefurahishwa na zawadi hizo.
Akaeleza kuwa eneo hilo litatumika kwa ajili ya ujenzi wa Chuo litaweza kutumika kujenga majengo ya kisasa ya chuo, nyumba za wahadhili wafanyakazi, makitaba ya kisasa, kumbi nzuri za mikutano ambazo wanafunzi watazitumia kuwafanyia semina, makongamano, pia wananchi watakuwa wanakodishiwa hivyo kukiingizia chuo mapato.
Aidha Profesa Mbwette alieleza kuwa Chuo Kikuu Huria kimeanzisha College za Mikoa na Vituo Wilayani ili kusaidia kuwapatia elimu wananchi walio wengi, na kwa upande wa Mkoa wa Katavi ni moja ya mikoa inayofanya vizuri hususani katika darasa la TEHAMA Kwani kila mwaka wanafunzi wanaongezeka kwa kasi tofauti na Mikoa mingine.
Pia alipongeza juhudi zinazofanywa na uongozi wa tawi la Katavi la kuwa na wanafunzi wengi wanaosoma katika tawi hilo tofauti na sumbawanga Mkoa wa Rukwa ambapo kwa tawi la Mkoa wa Katavi wapo wanafunzi wapatao karibu 300 wa fani mbalimbali hayo ni mafanikio makubwa ya kujivunia.
Prof. Mbwete akizungumzia nafasi nyingine aliyoipata alisema kuwa kwa sasa anaenda kutumikia wananchi wengine wa Afrika katika nchi ya Cameruni. Alisema kuwa kiongozi katika Chuo Kikuu cha Umoja wa Afrika Pan Afrikanism makao yake yako Yaoundé Cameroon hivyo atakuwa huko baada ya kupata nafasi hiyo, na alipata nafasi hiyo baada ya kuchaguliwa pale waliposhindanishwa na Maprofesa wenzie watano kutoka Afrika nay eye kuibuka mshindi hivyo atakuwa kiongozi huko tena.
Naye Mkurugenzi huyo wa Chuo Kikuu Huria tawi la Katavi Kyando alieleza kuwa Profesa Mbwette hakuna namna bora ya kumuaga zaidi ya kushukuru kwa kazi nzuri aliyoitendea jamii ya waTanzania na wanazuoni wenzio kuendeleza elimu ya juu na kuifikia jamii ya Pembezoni kwa namna ambayo isingeweza kudhaniwa miaka ishirini iliyopita.
Kwa upande wao wanafunzi wa chuo hicho katika risala yao iliyosomwa na Rais wa Wanachuo Pius Yaschitu ilieleza kuwa Makamu wa Chuo Prof. Mbwette ni mfano wa kuigwa kwa jinsi alivyo mbunifu kiongozi hodari, mchapakazi na anayependa kusikiliza na kuendelea kujifunza na anayependa kupokea ushauri kuondoka kwake ni pengo ambalo litachukua muda kuliziba.