Na Mwandishi Wetu
BENKI ya Posta Tanzania (TPB) Tawi la Mwanza, imetoa msaada wa madawati 40, meza 5 na viti 10 yenye thamani ya Sh milioni 5 kwa Shule ya Msingi Gedeli iliyopowilaya ya Nyakato, Mwanza. Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya Posta, Regina Semakafu, alikabidhi msaada huo jana kwa Kaimu Afisa Elimu Kizito Bahati wa Wilaya hiyo kwa niaba ya shule hiyo.
Mkurugenzi huyo alisema fedha za utengenezaji wa vifaa hivyo, zimetokana na faida wanayoipata kutokana na huduma mbalimbali wanazozitoa kwa wateja wao. Aliongeza uongozi wa benki, umeguswa baada ya kupata historia fupi ya shule hiyo, kuwa na uhaba wa madawati, viti, meza na makabati na kwa kuona hali halisi ya shule kwa wanafunzi wengi wao kuketi sakafuni wakiwa madarasani.
“Uongozi wa Benki ya Posta inatambua umuhimu wa elimu katika jamii yetu, na madawati haya yatasaidia sana kuongeza chachu ya elimu kwenyejamii,” alisema Mkurugenzi huyo.
Alisema licha ya kutoa huduma za kibenki, Benki ya Posta imeedelea kuwa karibu na jamii siku zote kwa kusaidia masuala mbalimbali ya kijamii, ikiwemo sekta ya elimu na huduma mbalimbali ambazo zinatolewa na benki hiyo, ikiwemo ongezeko la ATM mashine, idadi ya matawi na mikopo mbalimbali.
Kwa upande wake, baada ya kupokea msaada huo, Kaimu Afisa Elimu Kizito Bahati aliishukuru Benki ya Posta kwa msaada wa vifaa hivyo. “Tunasihi taasisi nyingine ziige mfano huu wa Benki ya Posta, maana bado kuna mahitaji mengi katika shule nyingi zilizopo wilayani hapa, aliongeza Kaimu Afisa Elimu. Naye Mwalimu Mkuu, Elly John aliushukuru uongozi wa Benki ya Posta kwa msaada huo, na kuhahidi watatunza vifaa hivyo ili viweze kutumika kwa muda mrefu.
Mwanafunzi wa darasa la saba, Alphaxard Nkongo alishukuru sana kwa msaada huo uliotolewa na Benki ya Posta, na kuongeza kuwa kwa sasa watakuwa wanakuja nakuondoka shule bila sare zao za shule kupata vumbi kama zamani walivyokuwa wanaketi kwenye sakafu.