Gervinho wa Arsenal afungiwa mechi tatu

Gervinho Kouassi

MSHAMBULIAJI wa Arsenal, Gervinho Kouassi amefungiwa mechi tatu kufuatia kutolewa nje kwa kadi nyekundu katika mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu ya soka ya England msimu huu dhidi ya Newcastle. Gervinho alitolewa baada ya kushikana mashati na Joey Barton, ambapo kiungo huyo wa Newcastle alianguka uwanjani.

Arsenal walikata rufaa kupinga kufungiwa kwa mechi tatu kutokana na sheria zinavyosema mchezaji akioneshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja kuwa ni adhabu kali mno. Lakini Chama cha Soka cha England kimetupilia mbali rufaa hiyo, hali inayomfanya Gervinho atumikie adhabu hiyo.

Gervinho aliyejiunga na Arsenal msimu huu akitokea klabu ya Lille ya Ufaransa kwa kitita cha paundi milioni 10.5, atakosa mechi dhidi ya Liverpool, Manchester United na Swansea.

Kiungo mwenye utata wa Newcastle Barton, ambaye alioneshwa kadi ya njano tu kutokana na kuwemo katika sakata hilo, alikiri katika mtandao wa Twitter kwamba “alianguka kirahisi” baada ya kuzabwa kofi na Gervinho.

Timu zote mbili Arsenal na Newcastle zimeshtakiwa na FA kwa kushindwa kuwadhibiti wachezaji wao huku kiungo wa Gunners Alex Song akikabiliwa na adhabu tofauti ya vurugu baada ya kumkanyaga Barton, tukio ambalo mwamuzi hakuliona.

-BBC