Mkuu wa zamani wa Jeshi Zimbabwe afa kwa moto

Jenerali mstaafu, Solomon Mujuru

MKUU wa zamani wa Jeshi la Zimbabwe amefariki dunia akiwa ndani ya shamba lake, hii ni kwa mujibu wa taarifa rasmi ilizozipata BBC. Taarifa zaidi zinasema Mujuru (62) aliyekuwa mwanasiasa mwandamizi na mume wa Makamu wa Rais wa Zimbabwe, Bi. Joice Mujuru, inaelezwa kuwa amekufa baada ya kuungua kwa moto uliozuka katika shamba lake lililopo eneo la Beatrice.
Ofisa mmoja ameiambia BBC kuwa Jenerali Mujuru alikufa kwa moto uliotokea shambani kwake eneo hilo ikiwa ni kilometa 80, Kusini mwa Mji Mkuu wa Harare Siku ya Jumanne.
Hata hivyo haijulikani iwapo alikuwa peke yake wakati huo au kama alipewa ulinzi wa jeshi. Wachambuzi wa mambo wanasema kifo hicho huenda kikazidisha mkanganyiko ndani ya chama cha Rais Robert Mugabe (87), kuhusu nani atakayemrithi kiongozi huyo mwenye umri wa miaka.
Mujuru aliyejulikana kama ‘Rex Nhongo’ wakati wa vita vya msituni, alikuwa Mkurugenzi wa Vikosi vya Mugabe wakati wa vita vya kupigania uhuru miaka ya 1970s’. Wakati wa uhuru mwaka 1980 aliongoza kikosi cha jeshi kabla ya kustaafu na kuingia katika biashara miaka 10 baadaye.
Rais Mugabe anatarajiwa kutoa tamko rasmi kuthibitisha kifo cha Jenerali Mujuru baadaye leo kwa mujibu wa itifaki za Chama Cha Zanu-PF. Mwandishi wa BBC, Brian Hungwe wa mjini Harare anasema Jenerali Mujuru alikuwa mwanachama mwandamizi wa Zanu-PF na anaelezwa alikuwa mwenye msimamo wa kadri na mpanga mikakati akiwa na ushawishi mkubwa wa kuweka viongozi wenye nguvu katika siasa za Zanu-PF.
“Kifo chake kimeacha pengo na kumuuacha mkewe bila nguzo ambaye ni mmoja kati ya makamu wawili wa Rais,” wachambuzi wa mambo wanasema.
Wakati wa vita dhidi ya utawala wa Rhodesia katika miaka ya 1970s, Jenerali Mujuru aliongoza mapambano ya silaha pamoja na marehemu Josiah Tongogora. Mwandishi wa BBC anasema alikuwa Jenerali Mujuru aliyewahamasha wapigania uhuru wa Msumbiji wakati wa mgogoro kumkubali Bw Mugabe kama kiongozi wa vikosi vya vuguvugu la waasi wa Zanla baada ya kuachiliwa kutoka kizuizini mwaka 1974.
Mkuu huyo wa zamani wa Jeshi akiwa kiongozi wa wapigania ukombozi dhidi ya utawala wa kikoloni, Jenerali Mujuru anatarajiwa kuzikwa kwa heshma ya kitaifa, katika makaburi ya mashujaa baadaye wiki hii.
-BBC