*Mpira wa Pete, New Habari Waogelea Magoli 46-2
MASHINDANO ya NSSF Media Cup yameendelea kupamba moto ambapo leo timu ya mpira wa miguu ya NSSF imeichalaza bila huruma timu ya Jambo Leo kwa magoli 3 kwa mtungi. Mchezo huo mkali ambao uliwafanya wachezaji wa timu ya Jambo Leo kukimbia uwanjani kutokana na mvua ya magoli mfululizo ulivunjika dakika ya 69.
Mwamuzi wa mpambano huo alilazimika kumaliza mchezo baada ya kuwasubiri wachezaji wa Jambo Leo kurudi uwanjani kwa dakika 15 bila ya mafanikio kisha kuamua kumaliza pambano na kutoa ushindi kwa timu ya NSSF. Hadi pambano hilo linasimama katika dakika ya 69 NSSF ilikuwa ikiongoza kwa magoli 3 kwa mtungi.
Wachezaji wa Jambo Leo walitoka uwanjani kwa kudai hawawezi kumalizia mchezo huo kutokana na hali ya uwanja ambapo ulikuwa umejaa madimbwi ya maji kwa baadhi ya maeneo kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam. Jambo Leo waliomba pambano hilo lisimamishwe na kuendelea kesho au siku nyingine ambapo uwanja ulikuwa katika hali nzuri tofauti na ilivyokuwa.
Hata hivyo Kamisaa wa Mchezo huo, Majuto Omary alisema mpambano huo hauwezi kurudiwa maana kanuni za mashindano haziruhusu na kuongeza kuwa kama Jambo Leo waliona uwanja ni mbovu wangeligoma tangu awali na sio kusubiri mchezo uchezwe hadi dakika ya 69.
“…Kanuni za mashindano haya haziruhusu wanachotaka Jambo Leo, kwanini wakimbie uwanjani baada ya kufungwa magoli matatu…mbona hawakugoma tangu mchezo haujachezwa hii ni janja yao wameona wamefungwa tena magoli mengi ndio wakimbie uwanja hii haikubaliki, ushindi utaenda kwa aliyeshinda na pambano halirudiwi,” alisema Omary.
Mvua ya magoli nyingine katika mashindano hayo iliwakumba timu ya Mpira wa Pete wasichana ya New Habari ambapo ilichalazwa magoli 46 kwa mawili na timu ya Business Times wasichana katika mchezo wao uliofanyika TTC Chang’ombe. Katika mchezo huo Busuness Timu walionekana kuutawala mchezo kwa muda wote na kuwapeleka puta akinadada wa New Habari kabla ya kuogelea mvua hiyo ya magoli.
Katika mchezo mwingine wa mpira wa miguu, Timu ya Uhuru Media iliichapa Sahara Media kwa magoli 2-1. Timu ya Sahara ndio waliokuwa wa kwanza kupata goli ambapo walipachika bao la kwanza katika dakika 26 kupitia kwa mchezaji wao Deodatus Nkwabi alilofunga kwa kichwa.
Uhuru walikuja juu dakika 46 ambapo mchezaji wao Mussa Gadi alifunga goli kwa mpira wa adhabu na kusawazisha mchezo. Mchezaji wa Uhuru Media, Ayub Malale alicheka na nyavu za Sahara Media katika dakika 87 baada ya kuunganisha crosi na kufanikiwa kufunga bao la pili. Hadi mwisho wa mchezo huo Uhuru 2 na Sahara 1.
Mashindano ya NSSF Media cup yanaendelea katika viwanja vya TCC Chang’ombe na Bandari Jijini Dar es Salaam, yakihusisha mpira wa miguu na mpira wa Pete ambapo vyombo mbalimbali vya Habari vinashiriki michezo hiyo. Mashindano hayo yanaambatana na wiki ya Huduma Kwa wateja ya NSSF ambapo wateja watapata fursa ya kupata elimu kuhusu huduma za NSSF.
Kama wewe ni Mkazi wa Dar es Salaam Tafadhali tembelea banda la NSSF katika viwanja vya TCC Chang’ombe kuanzia Tarehe 20/03/2015 hadi Tarehe 29/03/2015 saa 03:00 asubuhi hadi 11:00 jioni. Mwanachama ataweza kupata taarifa ya michango yake, Kujiandikisha Kwa Wanachama wapya na vile vile watapata elimu kuhusu huduma mbalimbali za NSSF.