Ligi kuu ya England Sergio Aguero aanza vyema.

Sergio Aguero akishangilia moja kati ya magori yake

Meneja wa Manchester City Roberto Mancini, amemfananisha Sergio Aguero sawa na mshambuliji wa zamani wa Brazil Romario, baada ya Muargentina huyo kuanza vyema katika mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu ya England dhidi ya Swansea.
Aguero aliyenunuliwa kwa kitita cha paundi milioni 38 alifunga mabao mawili na kusaidia kupatikana kwa jingine, wakati Manchester City ilipoibuka kwa ushindi wa mabao 4-0.
Romario aliyekuwa nyota kwa timu ya Brazil iliyonyakua Kombe la Dunia mwaka 1994, alifunga mabao karibu 1,000 katika muda wake wote wa kusakata kandanda ya kulipwa.
“Sergio ni kivuli cha Romario, ni wachezaji wanaoshabihiana,” alibainisha meneja wa City Mancini aliyejawa na furaha.
“Bado kiwango chake hakijafikia asilimia 100, lakini atakuwa mfungaji mzuri sana wa mabao kwa upande wetu.”
Mwaka 2007 Fifa ilimpongeza Romario baada ya kudai alifunga mabao 1,000, licha ya mabao yake mengine akiwa ameyafunga katika mechi za kirafiki na za vijana.
Mshambuliaji huyo aliyechezea klabu za Vasco da Gama, PSV Eindhoven na Barcelona, pia alipigiwa kura na kuchaguliwa mchezaji bora wa dunia mwaka 1994 na alifunga mabao 55 katika mechi 70 alizoichezea Brazil, akipitwa tu na Pele pamoja na Ronaldo.
Aguero aliingia kipindi cha pili katika mechi ya Jumatatu wakati huo Manchester City ilikuwa ikiongoza kwa bao 1-0, baada ya Mancini kumpumzisha kutokana na uchovu wa mechi za Copa Amerika ambapo mshambuliaji huyo aliiwakilisha timu yake ya taifa ya Argentina.
Lakini ubora wake ulionekana mara moja baada ya kuingia, nusura angefunga bao baada ya kupata mpira wa kwanza, kabla ya kupachika mabao mawili, akatengeneza moja na kuonesha umahiri wa kumiliki mpira na kusaidia wenzake.
“Ulikuwa ni mwanzo mzuri sana,” alisema Mancini.
Wakati huohuo, Manchester City imesema Muargentina mwenzake Aguero, Carlos Tevez atabakia katika klabu hiyo licha ya kuonesha dalili za kutaka kuondoka.
“Bado ni mchezaji wa Manchester City,” alisema mtendaji mkuu wa klabu hiyo Garry Cook.
“Itakuwa raha sana kwa mashabiki wa City kumuona akicheza pamoja na Sergio Aguero.”
-BBC