Rais Kikwete akutana kwa kifungua kinywa na Mzee Kaunda

KAUNDA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete asubuhi ya leo, Alhamisi, Februari 26, 2015, amekutana kwa kifungua kinywa na Mwanzilishi wa Taifa la Zambia na Rais wa Kwanza wa nchi hiyo, Mheshimiwa Kenneth David Kaunda.
Aidha, Rais Kikwete ambaye amemaliza ziara rasmi ya Kiserikali ya siku mbili katika Zambia, ameweka shada la maua kwenye kaburi la Mama Betty Muntikhe Kaunda, hayati mke wa Mzee Kaunda.
Rais Kikwete ambaye amekuwa kiongozi wa kwanza wa nje kualikwa kutembelea Zambia kwa ziara rasmi tokea Rais mpya wa nchi hiyo, Mheshimiwa Edgar Chagwa Lungu kushika madaraka ya kuongoza nchi hiyo mwezi uliopita, amewasili nyumbani kwa Mzee Kaunda katika eneo la State Lodge Area, Leopards Hill, kiasi cha kilomita 26 kutoka mjini Lusaka, kiasi cha saa mbili na dakika 40 asubuhi.
Rais Kikwete na ujumbe wake wa watu wachache amelakiwa na Bwana Kaweche Kaunda, mmoja wa watoto wa Mzee Kaunda ambaye amemwongoza hadi kwenye kaburi la mama yake, Betty Kaunda, ambako Rais Kikwete ameweka shada la maua.
Rais Kikwete amekaribishwa nyumbani kwa Mzee Kaunda na Mzee mwenyewe ambaye kama ilivyo jadi yake alikuwa ameshikilia kitambaa cheupe mkononi.
Baada ya kuweka saini kwenye kitabu cha wageni, Mzee Kaunda na Rais Kikwete walianza mazungumzo wakati wa kifungua kinywa na kwa saa mbili walizungumzia mambo mengi, hasa yale ya kijamii bila kuingiza siasa sana.
Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na watoto wawili wa Mzee Kaunda, Bwana Kaweche Kaunda wa kiume na Bibi Cheswa Kaunda Silwizya ambaye ni mtoto wa mwisho wa Mzee Kaunda na Hayati Betty Kaunda. Aidha, mazungumzo hayo yalihudhuriwa na Balozi wa Tanzania katika Zambia na Balozi wa Zambia katika Tanzania.
Rais Kikwete amemwambia Mzee Kaunda: “Wewe ni mmoja wa mashujaa wetu katika Bara la Afrika. Mzee Kaunda wewe ni nyota wa Bara letu, ambaye umehamasisha na kuwatia moyo watu wengi kukabiliana na changamoto za maendeleo. Tunakushukuru sana kwa mchango wako katika maendeleo ya Bara letu na tutaendelea kukuenzi kwa mchango huu. Tunakutakia maisha marefu na afya njema sana.”
Rais Kaunda amemwambia Rais Kikwete kuwa nyumba hiyo ambayo anaishi kwa sasa iliyoko katika mazingira yenye madhara ya kuvutia ya misitu ilijengwa kwa ajili yake na Rais wa tatu wa Zambia, Hayati Levy Mwanawasa. “Nyumba hii nilijengewe na Serikali ya Rais Mwanawasa.”
“Rais Mwanawasa alifanya jambo zuri, muhimu na la wajibu kabisa kwa sababu unastahili nyumba yenye hadhi ya namna hii kwa mchango wako kwa wananchi wa Zambia na Afrika katika maisha yako,” Rais Kikwete amemjibu Mzee Kaunda.
Rais Kikwete alipotaka kujua siri ya afya yake nzuri kwa umri wake mkubwa, Mzee Kaunda ambaye anafikisha umri wa miaka 91 katika miezi miwili ijayo, amemjibu: “vegetarian life” akiwa na maana ya kuwa ameishi maisha yake yote akila chakula ambacho huliwa na watu wasiokula nyuma katika maisha yao. “Chakula changu kikuu ni ugali na maharage.”
Wakati huo huo, Rais Kikwete ameondoka Lusaka, Zambia kurejea nyumbani baada ya kumaliza ziara rasmi ya Kiserikali ya siku mbili nchini Zambia kwa mwaliko wa Rais Lungu.
Kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kenneth Kaunda, Rais Kikwete ambaye aliandamana na Mama Salma Kikwete, ameagwa kwa heshima zote za kijeshi ikiwa ni pamoja na kupigiwa mizinga 21 kabla ya kupanda ndege kuondoka.