Zambia Yaomba Kununua Gesi Asilia Tanzania

GESI

Zambia imeomba Tanzania kuiuzia nchi hiyo ya jirani gesi asilia kwa madhumuni ya kuzalisha umeme na kupanua wigo wa uzalishaji wa viwandani.
Aidha, Tanzania na Zambia zimekubaliana kuifufua Reli ya TAZARA kati ya nchi hizo mbili kwa kukabiliana ipasavyo na changamoto na matatizo ambayo kwa muda sasa yamekuwa yanakwamisha utendaji bora wa reli hiyo iliyojengwa kwa nia ya kuiwezesha Zambia kupata njia ya kufikia baharini kwa urahisi zaidi na kusafirisha bidhaa zake kwenda nje.
Ombi hilo na makubaliano kuhusu TAZARA yalifikiwa jana, Jumatano, Februari 25, 2015 wakati wa mazungumzo rasmi kati ya nchi hizo mbili ikiwa ni sehemu ya ziara rasmi ya Kiserikali ya siku mbili iliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete katika Zambia kwa mwaliko wa Rais Edgar Chagwa Lungu. Mazungumzo hayo yalifanyika Ikulu ya Zambia, mjini Lusaka.
Katika mazungumzo hayo yaliyochukua muda mrefu, Rais Kikwete na Rais Lungu waliongoza nchi zao katika majadiliano kuhusu masuala mbali mbali ikiwa ni pamoja na ombi la Zambia kutaka kununua gesi kutoka Tanzania na jinsi ya kufufua Reli ya TAZARA.
Wakati wa mazungumzo hayo, Rais Lungu alimwomba Rais Kikwete akubali Tanzania iuzie gesi asilia Zambia, ombi ambalo Rais Kikwete alilikubali bila kusita.
“Hakuna shaka kuwa tuko tayari kuwauzieni gesi asilia ndugu zetu wa Zambia. Linalohitajika ni kwa Zambia kuweza kujenga bomba la kusafirishia gesi hiyo kutoka Tanzania hadi Zambia. Mwambie yoyote ambaye anaweza kutoa mkopo wa ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kuwa Tanzania iko tayari kuwauzieni gesi,” alisema Rais Kikwete wakati wa mazungumzo hayo.
Kuhusu ufufuaji wa Reli ya TAZARA, viongozi hao wawili walikubaliana kuangalia changamoto za kiuongozi na utendaji, changamoto za kiufundi, changamoto za kisheria na changamoto za kimuundo, ambazo zinakwamisha uendeshaji wa ufanisi wa Reli hiyo.
Reli hiyo yenye urefu wa kilomita 1,600 inaunganisha Dar es Salaam na Kapiri Mposhi, Zambia, ilijengwa kwa mkopo wa dola za Marekani milioni 500 kutoka Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China mwishoni mwa miaka ya 1960 na mwanzoni mwa miaka 1970.
Hata hivyo, Reli hiyo ilikabiliwa na changamoto kiasi cha kwamba sasa inachukua muda wa siku 12 kwa treni kusafiri kati ya vituo hivyo viwili vikuu wakati inachukua kiasi cha siku tano tu kwa magari kusafiri kati ya Dar es Salaam na Kapiri Mposhi.
Aidha, Reli hiyo yenye uwezo wa kubeba mizigo tani milioni tano za mizigo, mwaka jana, ilibeba mizigo yenye uzito wa tani 280,000 tu.
Serikali ya China imekubali kimsingi kusaidia kuifufua Reli hiyo lakini baada ya kupokelewa kwa ripoti ya uchunguzi unaofanywa kuhusu chanzo na ukubwa wa matatizo yanayoikabili Reli hiyo.