Timu ya Kamanda Kova yaingia Daraja la Kwanza

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova

Na Mwandishi wetu’

LIGI ya Taifa ngazi ya Fainali imemalizika jana kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga, huku ikizipa nafasi ya kupanda daraja la kwanza timu za Polisi Central ya Dar es Salaam, Mlale JKT ya Ruvuma na Mgambo Shooting ya Tanga.

Timu zingine zilizofanikiwa kupanda daraja kama washindwa bora ni Samaria ya Singida na Small Kids ya Rukwa.

Taarifa hii imetolewa leo na Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura na kuongeza kuwa usajili kwa ajili ya timu za daraja la kwanza utafanyika kuanzia Agosti 15 mwaka huu hadi Septemba 15 mwaka huu.

Alisema jumla ya timu 18 zitashiriki ligi inayotarajiwa kuanza mwishoni mwa Septemba mwaka huu. Taarifa rasmi ya tarehe ya kuanza ligi hiyo itatolewa baadaye.

Timu nyingine za Daraja la Kwanza ni Temeke United ya Temeke, Polisi (Iringa), Burkina Faso (Morogoro), Polisi (Morogoro), Rhino Rangers (Tabora), Polisi (Tabora), 94 KJ (Green Warriors) ya Kinondoni, Tanzania Prisons (Mbeya), Morani (Manyara), Transit Camp (Temeke), Rhino FC (Mbeya), Majimaji (Songea) na AFC (Arusha).

Manyema Rangers ya Ilala, Nyerere FC ya Kilimanjaro na Mwanza United ya Mwanza ndizo zilizoshuka daraja kurudi Ligi ya Taifa.