JK Atoa Pole Vifo vya Wanafamilia Ajali ya Moto

Waombolezaji katika eneo la msiba Kipunguni A, Ukonga Banana, Wilaya ya Ilala, Mkoa wa Dar es Salaam wakilia kwa uchungu.

Waombolezaji katika eneo la msiba Kipunguni A, Ukonga Banana, Wilaya ya Ilala, Mkoa wa Dar es Salaam wakilia kwa uchungu.


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ametuma salamu za rambirambi za dhati ya moyo wake kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiq kuomboleza vifo vya watu sita wa familia moja waliopoteza maisha kwa moto usiku wa kuamkia, Januari 7, 2015, katika eneo la Kipunguni A, Ukonga Banana, Wilaya ya Ilala, Mkoa wa Dar es Salaam.
Katika salamu zake, Februari 8, 2015, Rais Kikwete amevielezea vifo hivyo kuwa ni vya kusikitisha na kuhuzunisha sana.
“Nimepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa ya vifo vya watu sita wa familia moja kutokana na kuunguzwa na moto. Ni vifo vya kusikitisha na kuhuzunisha sana. Nakutumia wewe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu kuomboleza pamoja nawe, ndugu na jamaa na wanaukonga wote msiba huu mkubwa na wa ghafla,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Naomba uniwakilishie salamu zangu na pole nyingi kwa wanafamilia, wanandugu na jamaa wote ambao wamepoteza wapendwa wao katika tukio hili. Wajulishe kuwa niko nao na naungana nao katika kuomboleza vifo vya wapendwa wetu hawa kwa sababu msiba huu ni wetu sote. Aidha, waambie kuwa naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aziweke pema roho za marehemu.”
Rais Kikwete pia ameongeza kuwa ni matarajio yake kuwa vyombo husika vya Serikali vitafanya uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo kubaini chanzo na mazingira ya moto huo.