Waziri Mkuu Mizengo Pinda akizungumza bungeni.
HOTUBA YA MHESHIMIWA MIZENGO P. PINDA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA KUHITIMISHA SHUGHULI ZA MKUTANO WA 18 WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA TAREHE 7 FEBRUARI, 2015 I: UTANGULIZI (a) Masuala ya jumla Mheshimiwa Spika, 1. Tumekuwepo hapa kwa takriban siku 12 katika shughuli za Mkutano wa 18 wa Bunge lako Tukufu. Ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa Rehema kwa kutufikisha salama siku ya leo. 2. Lakini tumekutana hapa tukiwa tumeshuhudia mabadiliko katika Baraza la Mawaziri na Wenyeviti wa baadhi ya Kamati za Kudumu za Bunge. Niruhusu nitumie nafasi hii ya awali kuwapongeza Mawaziri na Naibu Mawaziri wote ambao wameteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali katika mabadiliko hayo. Aidha, napenda niwapongeze Wenyeviti watatu pamoja na Makamu mmoja kwa kuchaguliwa kuongoza Kamati za Kudumu za Bunge ikiwemo Kamati ya Bajeti, Kamati ya Nishati na Madini na Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala. Tunawatakia afya njema Mawaziri, Naibu Mawaziri na Wenyeviti wote katika kutekeleza majukumu yao mapya. Mheshimiwa Spika, 3. Tangu tulipomaliza Mkutano wa 16 na 17 wa Bunge lako Tukufu, kumetokea majanga katika sehemu mbalimbali Nchini ikiwemo mafuriko na mapigano ya Wakulima na Wafugaji kule Morogoro, pamoja na ajali za barabarani. Naomba nitumie nafasi hii kuwapa pole wote walioathirika na majanga, maafa na ajali za barabarani. Kwa wale waliopoteza maisha tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahala pema peponi Amina. b) Maswali Mheshimiwa Spika, 4. Katika Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge wamepata fursa ya kuuliza maswali ya kawaida na yale ya papo papo kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu. Jumla ya maswali 122 ya msingi na 313 ya nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Serikali. Aidha, Maswali 15 ya msingi na 13 ya nyongeza yaliulizwa na kujibiwa kwa utaratibu wa maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu. (c) Miswada na Taarifa Mbalimbali Mheshimiwa Spika, 5. Tunahitimisha Mkutano huu tukiwa tumekamilisha kazi kubwa ya kusoma na kujadili taarifa mbalimbli za Kamati za Bunge za Kisekta na zisizo za Kisekta. Kamati za Kisekta ambazo Taarifa zake zimewasilishwa na kujadiliwa na Waheshimiwa Wabunge ni zifuatazo: i) Kamati ya Miundombinu; ii) Kamati ya Nishati na Madini; iii) Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira; iv) Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji; v) Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala; vi) Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; vii) Kamati ya Masuala ya UKIMWI; viii) Kamati ya Ulinzi na Usalama; ix) Kamati ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa; x) Kamati ya Huduma na Jamii; na xi) Kamati ya Maendeleo ya Jamii. 6. Aidha, Bunge Lako Tukufu lilipokea na kujadili Taarifa za Kamati zisizo za Kisekta zinazosimamia Fedha za Umma zifuatazo: i) Kamati ya Hesabu za Serikali; ii) Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa; na iii) Kamati za Bajeti. Mheshimiwa Spika, 7. Vilevile, tumepokea na kujadili taarifa ya Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa kuchunguza sababu za migogoro baina ya Wakulima, Wafugaji Wawekezaji na Watumiaji wengine na Ardhi Nchini. Mheshimiwa Spika, 8. Katika Mkutano huu, tulipanga na tulitarajia kujadili Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Kodi wa mwaka 2014 (The Tax Administration Bill. 2014); Muswada wa Sheria ya Takwimu wa mwaka 2013 (The Statistics Bill, 2013); na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali (Na. 2) wa mwaka 2014, (The Written Laws Miscellaneous Amendments (No. 2) Bill, 2014) ambao ndio pia ulihusu Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Kiislamu Sura 375. (The Islamic Law (Restatement) Act) unaotambua Mahakama ya Kadhi. Mheshimiwa Spika, 9. Hata hivyo, hatukuweza kuijadili Miswada hiyo katika Mkutano huu, ili Kamati husika zipate nafasi na muda wa kupitia na kutoa ushauri kwa Bunge lako Tukufu. Ni matumaini yangu kwamba Miswada hii itapata nafasi ya kuwasilishwa na kujadiliwa katika Mkutano ujao wa 19 wa Bunge lako Tukufu. d) Hoja za Wabunge na Kauli za Mawaziri Mheshimiwa Spika, 10. Pamoja na shughuli zilizopangwa katika Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge walipata pia fursa ya kupokea na kujadili Hoja ya Mheshimiwa James Mbatia kuhusu kukamatwa na Polisi kwa Mwenyekiti wa Chama cha CUF Profesa Ibrahim Lipumba kutokana na maandamano ya Wafuasi wa Chama hicho yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam kiyume cha Sheria. Aidha, Serikali kupitia Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika ilipata nafasi ya kutoa kauli ya Serikali kuhusu kutatua changamoto za soko la Sukari Nchini. Mheshimiwa Spika, 11. Nitumie nafasi hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kushiriki kupokea na kujadili taarifa mbalimbali zilizowasilishwa. Napenda kuliahidi Bunge lako Tukufu kwamba michango ya Waheshimiwa Wabunge, maoni na mapendekezo ya Kamati zote kwa ujumla yatazingatiwa na Serikali kwa utekelezaji.
II: KILIMO a) Hali ya Uzalishaji na Upatikanaji wa Chakula Mheshimiwa Spika, 12. Hali ya uzalishaji na upatikanaji wa chakula nchini kwa ujumla imeendelea kuwa ya kuridhisha katika maeneo mengi kufuatia mavuno mazuri katika msimu wa kilimo wa 2013/2014. Tathmini ya awali ya uzalishaji wa mazao ya chakula Nchini hadi mwezi Septemba, 2014 inaonesha kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula katika msimu wa kilimo wa 2013/2014 ulifikia jumla ya Tani Milioni 16.0 zikiwemo Tani Milioni 9.8 za mazao ya nafaka na Tani Milioni 6.2 za mazao yasiyo ya nafaka. 13. Katika kipindi hicho, makadirio ya mahitaji ya chakula Nchini kwa mwaka 2014/2015 zilionesha kuwa tunahitaji Tani Milioni 12.8. Hivyo, kutokana na uzalishaji huu, Nchi ina ziada ya Tani Milioni 3.2 za chakula, na tumewezesha kujitosheleza kwa chakula kwa Asilimia 125. Napenda kutumia fursa hii kuwapongeza Wananchi na hasa Wakulima wote Nchini kwa kuitikia wito wa Serikali wa Mpango wa “KILIMO KWANZA”, na kuongeza tija katika uzalishaji, ambao umetuwezesha kupata mavuno mengi na kupata ziada hii ya chakula. Serikali itaendelea kuweka juhudi zaidi katika uzalishaji wa mazao ya Chakula ili kulihakikishia Taifa letu kuondokana na njaa na aibu ya kuomba chakula kutoka nje ya Nchi. Mheshimiwa Spika, 14. Tathmini hii pia imeonesha kuwa, uzalishaji wa nafaka kwa ujumla umeongezeka kutoka Tani Milioni 7.6 msimu wa 2012/2013 hadi Tani Milioni 9.8 msimu wa 2013/2014. Kati ya Tani hizo Milioni 9.8, Tani Milioni 6.7 ni za mahindi, Tani Milioni 1.7 ni za mchele na Tani Milioni 1.4 mtama. Kutokana na mahitaji ya nafaka kwa msimu wa 2014/2015 kuwa Tani Milioni 8.1; Taifa lina ziada ya Tani Milioni 1.4 za nafaka. Uzalishaji wa mahindi ambayo ni chakula kikuu umeongezeka kutoka Tani Milioni 5.2 katika msimu wa 2012/2013 hadi kufikia Tani Milioni 6.7 katika msimu wa 2013/2014. Kutokana na mahitaji ya mahindi kwa mwaka 2014/2015 kukadiriwa kuwa Tani Milioni 5.2, Taifa lina ziada ya Tani Milioni 1.5 za Mahindi sawa na Asilimia 29.7. Vilevile, uzalishaji wa mchele umeongezeka kutoka Tani Milioni 1.3 msimu wa 2012/2013 hadi Tani Milioni 1.7 katika msimu wa 2013/2014. Kwa vile makadirio ya mahitaji ya mchele kwa mwaka 2014/2015 ni Tani 900,000, Taifa lina ziada ya Tani 800,000 za mchele, sawa na Asilimia 89. b) Hali ya Akiba ya Chakula Mheshimiwa Spika, 15. Wakala wa Hifadhi ya Chakula wa Taifa (NFRA) walianza ununuzi wa nafaka katika msimu wa 2014/2015 wakiwa na akiba ya chakula ya Tani 189,493.7. Hadi kufikia tarehe 29 Januari, 2015 NFRA ilikuwa imeshanunua jumla ya Tani 298,122.3 za nafaka sawa na Asilimia 107.1 ya lengo la ununuzi. Aidha, kiasi cha chakula kilichochukuliwa katika maghala hadi tarehe 29 Januari, 2015 kilikuwa Tani 29,290.5. Jumla ya Tani 1,117.5 ziko njiani kutoka vituo vya Vijijini kwenda katika maghala ya Wakala wa Hifadhi ya Chakula wa Taifa katika Kanda mbalimbali. Hivyo hadi tarehe 29 Januari, 2015, akiba ya chakula katika maghala ya Wakala wa Hifadhi ya Chakula wa Taifa ilikuwa Tani 460,175.5 zikiwepo Tani 451,589.1 za mahindi; Tani 3,939.6 za mpunga; na Tani 4,646.8 za mtama. c) Changamoto ya Hifadhi ya Nafaka Mheshimiwa Spika, 16. Pamoja na mvua nzuri zilizonyesha katika msimu wa 2013/2014, ongezeko hili la uzalishaji wa chakula limechangiwa na juhudi za Serikali za kuhimiza Wananchi kuongeza matumizi ya zana kubwa za kilimo (Matrekta) pamoja na kutoa pembejeo za ruzuku kwa wakulima. Aidha, bei nzuri ya kununulia mahindi ya Shilingi 500 kwa kilo iliyotumiwa na Wakala wa Hifadhi ya Chakula wa Taifa iliwavutia wakulima wengi kupeleka mahindi yao katika vituo vya ununuzi vya Wakala jambo lililowafanya Wakala kushindwa kununua nafaka za ziada kutoka kwa wakulima na hivyo kusababisha kuwepo kwa malalamiko mengi kutoka kwa wakulima. Hadi kufikia tarehe 11 Novemba 2014, uwezo wa Wakala wa kuhifadhi nafaka katika maghala yake ulikuwa ni Tani 246,000 tu, hivyo kutokana na akiba kubwa iliyopo sasa ya Tani 460,175.5, imewalazimu Wakala kuhifadhi sehemu ya akiba hiyo katika maghala mengine Vijijini, katika Taasisi za Serikali na Sekta Binafsi; na nje ya maghala ya Wakala kwa kufunikwa na maturubai. d) Mpango wa kuongeza maghala ya Hifadhi ya Taifa Mheshimiwa Spika, 17. Makadirio ya mahitaji ya hifadhi Kitaifa kwa kipindi cha muda mfupi ni tani 400,000; kwa kipindi cha muda wa kati ni tani 700,000; na tani 1,000,000 kwa kipindi cha muda mrefu. Katika jitihada za kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa maghala ya kutosha ya kuhifadhi nafaka katika maghala ya Wakala wa Hifadhi ya Chakula wa Taifa, Serikali imeandaa mpango maalum unaotarajiwa kugharimu takriban Shilingi Bilioni 212 wa kuongeza uwezo wa NFRA wa kuhifadhi nafaka hadi kufikia Tani 400,000 ifikapo mwaka 2015/2016. Chini ya mpango huo, Serikali itajenga maghala au vihenge vya kisasa (Silos) katika maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa nafaka. e) Ujenzi wa Vihenge vya Kisasa (Silos) Mheshimiwa Spika, 18. Kutokana na kuwepo kwa changamoto ya ujenzi wa Silos, nilipokuwa Nchini Poland mwezi Oktoba 2014 nilipata fursa ya kukutana na Viongozi wa Serikali ya Poland pamoja na kutembelea Kampuni ya Mtynpol inayohusika na ujenzi wa Silos, kuhifadhi na kusindika nafaka kwa kutumia teknolojia za kisasa. Nilitumia fursa hiyo, kumwomba Makamu wa Rais wa Chama cha Wafanyabiashara cha Poland, Bwana Witold Karczewski ambaye pia ndiye Mwekezaji wa maghala (Silos) na Viwanda vya usindikaji Nchini Poland kutembelea Tanzania ili kuona uwezekano wa kujenga Silos zitakazotumia teknolojia inayoendana na mazingira ya Tanzania. Mheshimiwa Spika, 19. Tarehe 4 hadi 5 Oktoba, 2014; Bwana Witold alifika hapa nchini na kwa pamoja tulitembelea maghala ya Wakala wa Hifadhi ya Chakula wa Taifa yaliyopo Kizota – Dodoma. Baada ya ziara hiyo, mwezi Novemba, 2014 Serikali ya Tanzania imewasilisha maombi ya kupata Mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya Poland. Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa tayari Serikali ya Poland imepokea na kuyapitia maombi yetu; na mwishoni mwa mwezi huu wa Februari, 2015; Wizara ya Fedha inatarajia kukamilisha mazungumzo ya kupata mkopo huo wa masharti nafuu. Ni matumaini yangu kuwa utekelezaji wa mradi huo utaanza mapema mwaka huu baada ya Serikali ya Poland kuridhia maombi hayo. f) Hali ya Usambazaji wa Pembejeo ya Ruzuku Nchini Mheshimiwa Spika, 20. Kuanzia mwaka 2003/2004 hadi mwaka 2007/2008, Serikali imekuwa ikitoa ruzuku ya pembejeo za kilimo kwa wakulima kama fidia za gharama za usafiri ili pembejeo hizo ziuzwe kwa bei moja Nchi nzima. Kutokana na changamoto mbalimbali za kiutendaji, Mfumo huo ulibadilishwa na kuanzisha utaratibu wa kutumia Vocha kati ya mwaka 2008/2009 hadi msimu wa 2013/2014. Mheshimiwa Spika, 21. Mpango huo katika kipindi hiki cha miaka kumi umewezesha uzalishaji wa mazao ya chakula kuongezeka kutoka Tani Milioni 7.7 mwaka 2003/2004 hadi kufikia Tani Milioni 16 mwaka 2013/2014. Ongezeko hili limechangia ongezeko la viwango vya utoshelevu wa chakula Nchini kutoka Asilimia 88 mwaka 2003/2004 hadi kufikia Asilimia 125 mwaka 2013/2014. Aidha, uzalishaji wa zao la mahindi umeongezeka kutoka Tani Milioni 3.2 mwaka 2003/2004 hadi Tani Milioni 6.7 mwaka 2013/2014. Uzalishaji wa mchele umeongezeka kutoka Tani 600,000 mwaka 2003/2004 hadi Tani Milioni 1.7 mwaka 2013/2014. Mheshimiwa Spika, 22. Ongezeko la uzalishaji wa mazao hayo pamoja na sababu nyingine limechangiwa na ongezeko la matumizi ya pembejeo zilizotokana na mpango wa ruzuku. Pamoja na mafanikio ya mpango wa ruzuku ya pembejeo za kilimo kupitia utaratibu wa Vocha, pamekuwepo na changamoto katika ngazi mbalimbali za utekelezaji, ikiwemo ubadhirifu, upotevu wa Vocha na ucheleweshaji wa Vocha, hali iliyosababisha wakulima wengi kushindwa kupata pembejeo kama ilivyokusudiwa. g) Mfumo mpya wa usambazaji wa pembejeo Mwaka 2014/2015 Mheshimiwa Spika, 23. Katika kukabiliana na changamoto zilizopo katika Mpango wa Ruzuku ya Pembejeo kwa kutumia vocha; na katika jitihada za kutekeleza azma ya kuwapelekea wakulima pembejeo kwa ufanisi zaidi, Serikali katika msimu wa 2014/2015 imebuni utaratibu mpya wa majaribio ambao lengo lake ni kuviwezesha vikundi na Vyama vya Ushirika kuchukua mikopo ya pembejeo za kilimo kutoka Taasisi za za fedha; na vikundi vya wakulima, VICOBA na Vyama vya Ushirika moja kwa moja kutoka katika Makampuni ya Pembejeo. h) Hatua za Utekelezaji wa Mfumo mpya wa Ruzuku za Pembejeo Mheshimiwa Spika, 24. Jumla ya Kaya 946,000 zinatarajiwa kunufaika na Mpango wa Ruzuku ya Pembejeo za Kilimo kutoka Taasisi za Fedha na Makampuni ya pembejeo. Hadi sasa AMCOS 247 katika Mikoa ya Tabora, Kigoma, Mbeya (Chunya) Katavi, Singida, Iringa na Shinyanga zimepata mikopo ya pembejeo ya jumla ya Shilingi 74,737,708 kupitia Benki za CRDB. Benki ya NMB imetoa mikopo kwa vikundi sita (6) vinavyojishughulisha na kilimo cha mpunga yenye thamani ya Shilingi Milioni 600. Kupitia Benki za Wananchi, vikundi vya wakulima 147 katika Wilaya za Mbinga, Njombe, Mufindi, Kagera na Tandahimba vyenye wanachama 3,242 vilipata mikopo ya pembejeo yenye thamani ya Shilingi Milioni 844.4. 25. Kwa vile Halmashauri za Wilaya zitahusika moja kwa moja katika suala la usimamizi wa mpango huu, na kwa vile Kamati za pembejeo za Wilaya zitakuwa chini ya usimamizi wa Mkuu wa Wilaya, ninawaagiza Viongozi wa Mikoa na Wilaya kusimamia kwa karibu zoezi la kuhamasisha vikundi kuchukua mikopo katika Taasisi za fedha na vyombo vingine na kuhakikisha kuwa usambazaji wa pembejeo hizi unafanyika ipasavyo ili tuongeze idadi ya wanufaika wa mfumo huu na kuufanya kuleta mafanikio yaliyotarajiwa kwa manufaa ya Wananchi na Taifa kwa ujumla. i) Mwenendo wa Malipo ya Madeni ya Ununuzi wa Mahindi kwa Msimu wa 2014/2015 Mheshimiwa Spika, 26. Kama nilivyoeleza hapo awali, Wakala wa Hifadhi ya Chakula wa Taifa ilikuwa na kazi kubwa ya kununua nafaka kutoka kwa wakulima; vikundi vya wakulima na wafanyabishara. Kutokana na wakulima kupewa bei nzuri; na kutokana na wakulima kwa hiyari yao kuomba mazao yao yanunuliwe na Wakala kwa mkopo kuepuka kuharibika, wakulima walifika kwa wingi katika vituo vya mauzo tofauti na kiasi cha fedha ambacho Wakala walikuwa wametenga kwa ununuzi hivyo kuliwasababishia wakulima adha kubwa. Mheshimiwa Spika, 27. Hadi kufikia Mwezi Desemba 2014 Serikali ilikuwa inadaiwa kiasi cha Shilingi Bilioni 89 za Wakulima waliouzia Wakala mahindi. Aidha, hadi kufikia tarehe 29 Januari, 2015, Serikali ilikuwa imelipa wakulima hao kiasi cha Shilingi Bilioni 15 na kubakiza deni la Shilingi Bilioni 74. Katika juhudi za Serikali za kutatua changamogo ya deni hili, Mwezi Februari 2015 Serikali inatengemea kulipa kiasi cha Shilingi Bilioni 40 na kubakia na deni la Shilingi Bilioni 34 ambazo tunategemea zitalipwa kutokana na mkopo wa CRDB wa Shilingi Bilioni 15 na Bajeti ya Serikali. Aidha, Serikali pia imepanga kuuza kiasi cha Tani 175,000 kutoka katika akiba yake ya chakula kwa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na wafanyabishara. Nichukue fursa hii kuwapa pole wakulima wanaoidai Serikali kwa usumbufu wanaopata. Hata hivyo, ninapenda kuwahakikishia kuwa wote watalipwa stahili zao katika kipindi kifupi kijacho.
III. ELIMU (a) Jitihada za Utengenezaji wa Madawati Mheshimiwa Spika, 28. Moja ya changamoto tulizonazo katika kipindi hiki kwenye Sekta ya Elimu ni pamoja na suala la madawati katika Shule za Msingi na Sekondari Nchini. Taarifa nilizo nazo ni kuwa, hadi sasa mahitaji yetu kama Nchi ni madawati Milioni 3.3 kwa Shule za Msingi, na tayari tunayo Madawati Milioni 2.1 sawa na Asilimia 63 ya mahitaji. Kwa maana hiyo, tuna upungufu wa madawati Milioni 1.2 sawa na Asilimia 37. Kwa upande wa Shule za Sekondari tunayo madawati Milioni 1.4 kati ya madawati 1.5 yanayohitajika au Asilimia 92 ya mahitaji. Kuna upungufu wa madawati takriban 120,000 sawa na Asilimia Nane ya mahitaji. Upungufu huo ni kwa idadi ya wanafunzi walioko Shule za Msingi na Sekondari kwa sasa. 29. Wakati tunazungumzia upungufu huo wa madawati idadi ya Wanafunzi wa Shule ya Msingi na Sekondari inaendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka kadiri idadi ya watu inavyoongezeka. Hivyo, kasi yetu ya kuondoa upungufu wa madawati inatakiwa kuwa kubwa kuliko kasi ya ongezeko la wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari kwa mwaka. Ni jukumu letu wote Serikali, Sekta Binafsi pamoja na Wananchi kwa ujumla kuondoa upungufu huo hususan katika Shule za Msingi. Mheshimiwa Spika, 30. Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuondoa tatizo hili la madawati. Hatua hizo ni pamoja na kupeleka fedha za ununuzi wa madawati kutoka Serikali Kuu kwenda kwenye Serikali za Mitaa. Aidha, kiasi cha Shilingi Bilioni 12.3 zilizotokana na fedha za fidia ya Rada zilielekezwa kwenye Halmashauri kwa ajili ya kununulia madawati. Hadi sasa madawati ya plastiki 30,996 yameshasambazwa Nchini. Usambazaji wa madawati 61,468 ya mbao utaanza hivi karibuni. Vilevile, Serikali imekamilisha mikataba ya kusambaza madawati mengine ya plastiki 75,699. Tunatarajia kuwa fedha hizo za Rada zitapunguza uhaba wa madawati kwa asilimia 5.1. Katika mwaka 2014/2015, kiasi cha Shilingi Bilioni 1.1 kimetengwa na Halmashauri kwa ajili ya kununua madawati 152,000. Mheshimiwa Spika, 31. Serikali imekuwa ikishirikiana na Taasisi za Umma, Wahisani, Sekta Binafsi na Mwananchi mmoja mmoja katika kupunguza uhaba madawati Nchini, Nitumie nafasi hii kuwashukuru, wote ambao wamekuwa wakichangia Sekta ya Elimu hasa katika tatizo hili la upungufu wa madawati. a) Ujenzi wa Maabara katika Shule za Sekondari. Mheshimiwa Spika, 32. Mtakumbuka kuwa Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipokuwa kwenye ziara Mkoani Singida mwaka 2012 alielekeza kila Shule ya Sekondari Nchini iwe ina vyumba vitatu vya maabara ifikapo tarehe 30 Novemba 2014. Tangu wakati huo hadi sasa Viongozi wa Serikali Mitaa na Tawala za Mikoa wamekuwa wakitekeleza maelekezo hayo. Hali ya ujenzi wa vyumba vya maabara Nchini inaonesha kuwa hadi mwezi Desemba 2014 vyumba 3,607 sawa na Asilimia 34 ya mahitaji ya vyumba 10,653 vya maabara Nchini vilikuwa vimejengwa. Aidha, Vyumba 6,249 sawa na Asilimia 59 ya mahitaji vilikuwa vinaendelea kujengwa na Asilimia 7 bado vilikuwa havijaanza kujengwa. Mheshimiwa Spika, 33. Mkoa uliofanya vizuri katika kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais hadi kufikia Desemba 2014 ni Mkoa wa Njombe ambao ulifanikiwa kukamilisha ujenzi wa vyumba vya maabara kwa Asilimia 96 ya shule za sekondari zilizopo Mkoani humo. Mkoa wa Ruvuma nao ulikamilisha ujenzi kwa Asilimia 81, ukiwa ni Mkoa wa pili Kitaifa. Napenda kutumia fursa hii kuipongeza Mikoa hii miwili kwa kutekeleza vizuri maelekezo ya Mheshimiwa Rais. Imeonesha mfano mzuri katika kutekeleza maelekezo ya Kiongozi wetu wa Nchi. Mheshimiwa Spika, 34. Katika zoezi hili Mkoa wa Morogoro ulikuwa Mkoa wa tatu ambao ulijitahidi kujenga vyumba vya madarasa kwa kufikia kwa asilimia 53 ya mahitaji. Mikoa 22 iliyobaki haikuweza kufikia asilimia 50 ya lengo kwa kipindi chote cha mwaka 2012 – 2014. Kati ya Mikoa hiyo ambayo haikuweza kufika hata robo ya lengo (Asilimia 25) katika kipindi tajwa cha takribani miaka mitatu ni Mikoa sita; nayo ni Mtwara (Asilimia 21), Lindi (Asilimia 20), Tabora (Asilimia 17), Dodoma (Asilimia 12), Rukwa (Asilimia 11) na Kigoma (Asilimia 10). Tunaweza kusema hii ndiyo Mikoa ya mwisho katika kutekeleza agizo la Rais. Mikoa 16 ambayo sikuitaja hapa iko katika kundi la Asilimia kati ya 26 hadi 49. Mheshimiwa Spika, 35. Mheshimiwa Rais katika hotuba yake kwa Wananchi ya tarehe 31 Desemba 2014 aliongeza miezi sita zaidi hadi Juni 2015 kwa wale ambao hawajakamilisha ujenzi wa maabara hizo ili waweze kukamilisha. Ni matarajio ya Mheshimiwa Rais kuwa muda huo unatosha kwa kila Sekondari iliyopo Nchini kuwa na vyumba vitatu vya maabara na aliweka bayana kuwa hakusudii kuongeza tena muda baada ya muda huo kupita yaani Juni 2014. Hivyo, ninawataka Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Mameya, Wenyeviti na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Wilaya na Miji Nchini kuhakikisha maagizo haya yanatekelezwa. Aidha, ninatoa rai kwa Waheshimiwa Wabunge na Madiwani kutoa msukumo stahiki katika utekelezaji wa maagizo haya kwa maslahi ya Taifa letu. 36. Kwa upande wa Serikali, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI haina budi kuhakikisha agizo hili la Mheshimiwa Rais linatekelezwa ndani ya muda uliotolewa. Aidha, katika kufanya hivyo wahakikishe kuwa vyumba vya maabara vinavyojengwa vina ubora stahiki na vinalingana na thamani ya fedha zilizotumika. Ubadhirifu wa aina yoyote usipewe nafasi na watakaobainika kuhusika wachukuliwe hatua za kisheria mapema. Nitapenda OWM – TAMISEMI waendelee kufuatilia suala hili na kunipa taarifa mara kwa mara.
IV: SEKTA YA NISHATI a) Hatua iliyofikiwa ya Upatikanaji wa Nishati Vijijini (Miradi ya REA) Mheshimiwa Spika, 37. Serikali imedhamiria kuimarisha na kuongeza kiwango cha huduma za upatikanaji wa Nishati ya Umeme Vijijini ili kujenga msingi wa uchumi imara na wa kisasa wa Taifa linalojitegemea. Moja ya hatua zinazochukuliwa ni utekelezaji wa Mpango Kabambe wa usambazaji Umeme Vijijini. Mheshimiwa Spika, 38. Ili kufikia azma hiyo, Wakala wa Nishati Vijijini umeanza kutekeleza Mradi Kabambe wa Awamu ya Pili unaohusisha usambazaji wa umeme Vijijini katika Mikoa yote ya Tanzania Bara. Mradi huu unahusisha ujenzi wa Vituo 6 vya kupoozea umeme na njia ya kusambaza umeme kwenye maeneo yenye msongo wa 33kV yenye urefu wa Kilomita 15,000. Vilevile, utahusisha ujenzi wa njia za kusambaza umeme yenye msongo wa kilo-Volti 400 zenye urefu wa Kilomita 8,000 na ufungaji wa Vipooza Umeme 3,300. Mradi huu utakapokamilika utakuwa umeunganisha Wateja wa awali takriban 250,000 katika Vijiji 1,142. Mradi huu unafuatia baada ya kukamilika kwa zaidi ya Asilimia 80 ya Mradi Kabambe wa Awamu ya Kwanza ambapo Wateja 17,688 wameunganishwa kwenye miundombinu ya usambazaji wa umeme Nchini. Mheshimiwa Spika, 39. Mradi Kabambe wa Awamu ya Pili unakadiriwa kugharimu Shilingi Bilioni 881. Hadi sasa takriban Shilingi Bilioni 278 zimelipwa kwa Wakandarasi ikiwa ni malipo ya awali ya Asilimia 10 na gharama za kununua vifaa na hati za dhamana zenye jumla ya Shilingi Bilioni 439 kwa Miradi yote 35 zimefunguliwa. Mheshimiwa Spika, 40. Kutokana na juhudi za Serikali za kuongeza kasi ya kuunganisha umeme Vijijini ambazo zimechochewa na kupunguza gharama za kuunganisha umeme kwa wananchi hasa waishio Vijijini idadi ya Watanzania waliounganishiwa umeme imeongezeka kutoka Asilimia 2.5 kwa Mwaka 2007 hadi Asilimia 18.4 kwa Mwaka 2010 na kufikia Asilimia 24 kwa Mwaka 2014. b) Utekelezaji wa Mradi wa ujenzi wa Bomba la Gesi Mheshimiwa Spika, 41. Kuanzia mwaka 2013 Serikali ilianza kutekeleza Mradi wa ujenzi wa Bomba la Gesi kutoka Mtwara na mitambo ya kuchakata na kusafisha gesi unaendelea vizuri. Mpaka kufikia mwezi Oktoba, 2014 ujenzi wa bomba ulikuwa umefikia Asilimia 97 na ule wa mitambo ulikuwa umefikia Asilimia 84. Kwa wastani mradi mzima sasa umekamilika kwa Asilimia 92. Matarajio ni kumalizika kwa ufungaji wa mitambo yote na kuanza majaribio ya awali. Mara majaribio yote ya miundombinu yatakapokamilika, miundombinu hii itakabidhiwa kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) kwa uendeshaji. Zoezi hilo linatarajiwa kufanyika mwezi Juni, 2015. Mheshimiwa Spika, 42. Ili kujiandaa kunufaika na upatikanaji wa Gesi Asilia, TPDC imeanzisha Kampuni yake Tanzu (GASCO) ambayo imepewa majukumu yote ya kumiliki miundombinu yote ya usafishaji, usafirishaji na usambazaji wa gesi asilia hapa nchini pamoja na kukusanya gesi kutoka vyanzo mbalimbali. Ili kufanikisha azma hii ya Serikali, tayari GASCO kupitia TPDC imeajiri Wafanyakazi wapya wapatao 120 kwa ajili ya mitambo ya kusafisha gesi na wengine 50 kwa ajili ya kuendesha bomba la gesi. Mheshimiwa Spika, 43. Manufaa mengine yatakayopatikana kutokana na upatikanaji wa Gesi Asilia ni kupata umeme wa uhakika na matumizi viwandani, magari na majumbani. Aidha, Nchi itaokoa Dola za Marekani Bilioni Moja (sawa na Shilingi za Tanzania Trilioni 1.6) kwa mwaka kutokana na mitambo iliyopo nchini kutumia gesi asilia badala ya mafuta. Faida nyingine za mradi mpya ni pamoja na ajira katika mitambo itakayojengwa Madimba na Songo Songo kwani kila mtambo utahitaji wastani wa Wafanyakazi 60. Pia, mradi utatoa ajira katika Sekta zote na hususan za Afya, Elimu, Maji, Usafiri pamoja na huduma nyingine za Kijamii zitakazohitajika katika maeneo husika. Natoa wito kwa Wananchi wote kulinda miundombinu ya Gesi Asilia ambayo inajengwa kwa gharama kubwa. Aidha, nawahimiza Wakandarasi wa Mradi wa Bomba la Gesi kukamilisha ujenzi kwa muda uliopangwa.
V: UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA a) Matokeo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Mheshimiwa Spika, 44. Uchaguzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa uliofanyika Nchini tarehe14 Desemba 2014 ulihusisha uchaguzi wa Wenyeviti wa Vijiji 12,261, Wenyeviti wa Vitongoji 63,319, Wenyeviti wa Mitaa Mijini 3,884, Wajumbe wa Serikali za Vijiji/Mitaa na Wajumbe wa Viti Maalum. Jumla ya watu 8,137,974 sawa na asilimia 69 ya watu waliojiandikisha kupiga kura walijitokeza kupiga kura. Vyama vya Siasa 17 sawa na asilimia 81 ya Vyama vyote vyenye usajili wa kudumu vilishiriki kwenye uchaguzi huu. 45. Taarifa ya matokeo inaonesha kwamba katika nafasi ya Wenyeviti wa Vijiji, CCM kilishinda kwa asilimia 79.4, CHADEMA asilimia 15.1 na CUF asilimia 4.6. Vyama vingine kwa ujumla vilipata asilimia 0.9. Matokeo ya Wenyeviti wa Vitongoji yanaonesha kuwa CCM imeshinda kwa asilimia 79.3, CHADEMA asilimia 15.6, CUF asilimia 4.3 na vyama vingine vilipata asilimia 0.8. Nafasi za Wenyeviti wa Mitaa CCM kilishinda kwa asilimia 66.5, CHADEMA asilimia 25.4, CUF asilimia 6.8 na vyama vingine vilipata kwa asilimia 1.3. Matokeo ya Wajumbe wa Serikali za Vijiji/Mitaa ni kuwa CCM ilipata asilimia 79.3, CHADEMA asilimia 15.7, CUF asilimia 4.3 na Vyama vingine vilipata asilimia 0.7. Kuhusu matokeo ya Wajumbe wa Viti Maalum ni kuwa CCM walipata asilimia 82.1, CHADEMA asilimia 13.7, CUF asilimia 3.5 na Vyama vilivyobaki navyo vilipata asilimia 0.7. b) Changamoto Zilizojitokeza Mheshimiwa Spika, 46. Pamoja na mafanikio yaliyopatikana wakati wa uchaguzi huo, zipo changamoto zilizojitokeza katika mchakato mzima wa upigaji kura. Hii ni pamoja na kuwepo kwa vurugu siku za uchaguzi, wagombea kufariki au kujitoa, ukosefu wa umakini katika usimamizi na ucheleweshaji wa vifaa vya kupigia kura. Kutokana na kasoro hizo asilimia 1.2 ya maeneo yaliyostahili kupiga kura bado hawajapiga kura. Hata hivyo, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI wamejipanga vizuri kuhakikisha kwamba uchaguzi wa maeneo yaliyobaki na tathmini yake unakamilika mapema iwezekanavyo. 47. Aidha, kutokana na baadhi ya Wakurugenzi wa Halmashauri kuonesha udhaifu katika kusimamia uchaguzi huo, Serikali ilichukua hatua ya kutengua uteuzi wa Wakurugenzi sita (6) ambao ni Mkurugenzi wa Mkuranga, Kaliua, Kasulu, Serengeti, Sengerema na Bunda. Vilevile, wapo Wakurugenzi waliosimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi wa makosa yao wakiwemo Wakurugenzi wa Hanang’, Mbulu, Ulanga, Kwimba na Manispaa ya Sumbawanga. Wapo pia, Wakurugenzi waliopewa “ONYO KALI” ambao ni Wakurugenzi wa Rombo, Busega na Muheza. Wakurugenzi waliopewa “ONYO” pekee ni wa Manispaa ya Ilala, Hai, na Mvomero. Watumishi wa ngazi za chini pia walichukuliwa hatua na Halmashauri ambazo ni mamlaka zao za nidhamu. Utekelezaji wa hatua hizi utasaidia kupeleka ujumbe kwa wale wote ambao watashindwa kutoa usimamizi thabiti kwenye chaguzi zijazo. c) Pongezi na Shukurani kwa Wananchi Mheshimiwa Spika, 48. Kwa kuzingatia mchakato mzima wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2014, naomba uniruhusu nitumie fursa hii kushukuru na kuwapongeza Wananchi wote walioshiriki na hivyo kufanikisha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2014. Nipongeze pia Vyama vyote vya Siasa vilivyojitokeza kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo. Kipekee kabisa niwapongeze Viongozi na Wanachama wote wa Chama cha Mapinduzi kwa ushindi mkubwa na wa kishindo katika maeneo yote kuanzia nafasi za Vijiji, Vitongoji, Mitaa, Wajumbe wa Serikali za Mitaa/Vijiji na Viti Maalum.
VI: HALI YA MAENDELEO YA ZANZIBAR Mheshimiwa Spika 49. Tarehe 10 Januari, 2015 nilibahatika kuhudhuria katika sherehe ya uwekaji jiwe la msingi katika Shule ya Sekondari ya Kibuteni Mkoa wa Kusini Unguja. Ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar. Shule ya Sekondari ya Kibuteni (Unguja) ambayo nilikwenda kuiwekea jiwe la msingi pamoja na shule nyingine ya Mkanyageni – Pemba zinajengwa kwa ushirikiano na Benki ya Kiarabu kwa Maendeleo ya Afrika (BADEA) ambapo BADEA imetoa mkopo wa Dola za Kimarekani Milioni Sita na Serikali ya Zanzibar imatoa Dola 600,000 ambazo ni Asilimia 10 ya gharama zote. Gharama za ujenzi kwa fedha za kitanzania inatarajiwa kufikia Shilingi Bilioni 3.0. 50. Ujenzi wa Shule hiyo ya kisasa ni mwendelezo wa juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya kusukuma maendeleo ya Elimu katika sehemu zote za Zanzibar. Aidha, Shule hii ni miongoni mwa Shule za Sekondari 27 zilizojengwa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Saba inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein ambapo Shule 19 zimekamilika na 18 kati ya hizo zimekwisha funguliwa. Mheshimiwa Spika, 51. Chini ya mkopo wa Benki Kuu ya Dunia Skuli tatu za Sekondari zimefanyiwa ukarabati mkubwa, kampasi mpya ya Chuo cha Ualimu cha Benjamini William Mkapa huko Pemba imejengwa, madawati na vitabu vya ziada na kiada, vifaa vya maabara na kompyuta vimenunuliwa. Pia, mafunzo ya Ualimu kazini yameendeshwa kwa muda wa miaka mitano. Mradi huo umegharimu Dola Milioni 48 ambapo Dola Milioni 42 zimetolewa na Benki ya Dunia na Dola Milioni sita ni mchango wa Serikali. Mheshimiwa Spika, 52. Wakati tunaadhimisha miaka 51 ya Mapinduzi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein alieleza mafanikio yaliyopatikana Zanzibar baada ya utekelezaji wa Dira 2020, MKUZA II, Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2010 – 2015 na Malengo ya Milenia. Miongoni mwa mafanikio muhimu yaliyopatikana ni kukua kwa uchumi ambapo kuanzia mwaka 2010 hadi 2014 Pato la Taifa limeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 942.3 mwaka 2010 hadi Shilingi Bilioni 1,442.8 mwaka 2013 sawa na Asilimia 53.0. Aidha, katika kipindi hicho uchumi wa Zanzibar ulikua kutoka Asilimia 6.4 mwaka 2010 hadi kufikia Asilimia 7.4 mwaka 2013. Pato la Mtu Binafsi nalo limeongezeka kwa wastani wa Asilimia 38 kutoka Shilingi 778,000 mwaka 2010 na kufikia Shilingi milioni 1.1. mwaka 2013. Kwa mwaka 2014 kasi ya kupanda kwa bei za bidhaa na huduma (Mfumuko wa Bei) ilibaki katika wastani wa tarakimu moja ya Asilimia 5.6, ikilinganishwa na 6.1 kwa mwaka 2010. Mheshimiwa Spika, 53. Mafanikio yanaonekana pia katika ukusanyaji wa mapato ambapo, katika miaka minne 2006/2007 hadi 2009/2010, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilikusanya mapato ya Shilingi Bilioni 484, ikilinganishwa na Shilingi Bilioni 997 zilizokusanywa katika kipindi cha 2010/2011 mpaka 2013/2014. Takwmu hizi zinaonesha ongezeko la Asilimia 106. Mheshimiwa Spika, 54. Katika kuimarisha mazingira ya biashara kwa kushirikiana na Sekta Binafsi, Zanzibar imeweza kusafirisha bidhaa zenye thamani ya Shilingi Milioni 94,235.8 kwa mwaka 2014 kutoka bidhaa zenye thamani ya Shilingi 87,799.6 kwa mwaka 2013, sawa na ongezeko la Asilimia 7.3. 55. Kwa upande wa Sekta ya Utalii, idadi ya Watalii imeongezeka kutoka Watalii 132,836 mwaka 2010 na kufikia Watalii 274,619 mwaka 2014. Hili ni ongezeko la Asilimia 107. Katika elimu idadi ya Shule za maandalizi imeongezeka kutoka Shule 238 mwaka 2010 hadi 279 mwaka 2014, ongezeko hili ni sawa na Asilimia 17. Shule za Msingi zimeongezeka kutoka 299 mwaka 2010 hadi 359 mwaka 2014 ongezeko la Asilimia 20. Shule za Sekondari zimeongezeka kutoka 194 mwaka 2010 hadi Shule 210 mwaka 2014. Ongezeko hili ni sawa na Asilimia Nane (8%). Idadi ya Wanafunzi katika Vyuo Vikuu imeongezeka kutoka 3,624 mwaka 2010 hadi 6,038 mwaka 2014. Ongezeko hili ni sawa na Asilimia 67. Mheshimiwa Spika, 56. Katika Seka ya Afya, idadi ya Wataalam wa Afya imeongezeka kutoka 3,634 mwaka 2010 hadi kufikia 4,618 mwaka 2014. Katika kutoa huduma za maji safi na salama, baadhi ya maeneo yamefikisha Asilimia 87.7 ya mahitaji halisi katika Mkoa wa Mjini Magharibi Kaskazini Unguja Asilimia 71.7, Kusini Unguja 76.4 Kaskazini Pemba, Asilimia 56.4 na Kusini Pemba Asilimia 74.1. 57. Mafanikio yapo pia na yanajionesha katika Sekta zingine zote kama vile Barabara, usafirishaji na uimarishaji wa Miundombinu ya Bandari, Viwanja vya Ndege, Kilimo, Ardhi, Upatikanaji wa Umeme, Sekta ya Mifugo na Uvuvi. Mheshimiwa Spika, 58. Nimeamua kuyasema mafanikio haya kuonesha hatua iliyofikiwa kutokana na juhudi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kujenga uchumi imara wa watu wake. Napenda nichukue nafasi hii kumpongeza kwa dhati Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein na Wananchi wote wa Zanzibar kwa jinsi wanavyoshirikiana katika kuhakikisha wanapiga hatua ya maendeleo ya kukuza uchumi wa Zanzibar. Pamoja na pongezi hizi ni matumaini yangu kwamba Wananchi wa Zanzibar wataendeleza ushirikiano uliopo chini ya uongozi wa Dkt, Ali Mohamed Shein katika kukuza uchumi wa Nchi yao.
VII: HITIMISHO Mheshimiwa Spika, 59. Kama ilivyo ada, naomba nitumie nafasi hii kuwashukuru wote waliosaidia kufanikisha mkutano huu. Nikushukuru wewe Mheshimiwa Spika, kwa kutuongoza vizuri na kwa busara kubwa. Niwashukuru Wenyeviti wa Bunge kwa kazi nzuri ya kuongoza vikao vya Bunge lako Tukufu. Kipekee niwatambue Mheshimiwa Lediana Mng’ong’o na Mheshimiwa Kidawa Salehe ambao wamekalia kiti kwa mara ya kwanza lakini kwa weledi mkubwa Hongereni sana!!. 60. Niwashukuru tena Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge za Kisekta na zisizo za Kisekta kwa kuwasilisha taarifa za Kamati zao vizuri. Aidha, niwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge kwa kazi nzuri ya kujadili taarifa hizo na kwa michango mbalimbali wakati wa Mkutano huu. Mapendekezo ya Kamati zote tuliyokubaliana tumeyaweka pamoja ili kupata urahisi wa kuyatekeleza. Tunaomba Waheshimiwa Wabunge wote wawe na nakala ya mapendekezo hayo kwa ajili ya ufuatiliaji. Mheshimiwa Spika, 61. Nitumie nafasi hii pia kumshukuru Katibu wa Bunge na Wasaidizi wake wote kwa kazi nzuri ya kuhakikisha mkutano huu unakamilisha shughuli zake kama ilivyopangwa. Niwashukuru Wataalam wote wa Serikali na Taasisi zake ikijumuisha Taasisi za Sekta Binafsi, kwa misaada ya Kitaalam na huduma mbalimbali za kufanikisha Mkutano huu. 62. Niwashukuru pia Waandishi wa Habari kwa kazi nzuri walizofanya kuhakikisha kuwa taarifa za majadiliano na maamuzi mbalimbali ya hapa Bungeni zinawafikia Wananchi. Niwashukuru Madereva kwa kazi nzuri waliyofanya ya kuwasafirisha kwa usalama Waheshimiwa Wabunge, Viongozi mbalimbali,
Wataalam na Wasaidizi wote walioshiriki katika Mkutano huu. Mheshimiwa Spika, 63. Nimalizie kwa kuwatakia wote safari njema mnaporejea kwenye maeneo yenu ya kazi na katika majimbo yenu. Ninaamini kwamba, Mwenyezi Mungu atatulinda na kutuweka salama sote kama tulivyo hadi kukutana tena katika Mkutano ujao. 64. Baada ya kusema hayo, naomba sasa kutoa Hoja kwamba, Bunge lako Tukufu liahirishwe hadi tarehe 17 Machi, 2015 saa 3:00 Asubuhi litakapokutana katika Mkutano wa 19 kwenye Ukumbi huu hapa Dodoma. Mheshimiwa Spika, 65. Naomba kutoa Hoja.