WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara atakuwa mgeni rasmi kwenye fainali ya michuano ya Kombe la Taifa Wanawake kati ya Pwani na Temeke itakayochezwa Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam.
Mechi hiyo itakayoanza saa 10.15 jioni itachezeshwa na mwamuzi wa FIFA, Jonesia Rukyaa, na itaonyeshwa moja kwa moja na televisheni ya Azam. Waamuzi wasaidizi ni Hellen Mduma, Agnes Alphonce, na Mwanahamisi Matiku wakati Kamishna ni Ingridy Kimario.
Timu za Ilala na Kigoma zitacheza mechi ya utangulizi kutafuta mshindi wa tatu kuanzia saa 8.00 mchana. Bingwa wa michuano hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya Proin na kufanyika kwa mara ya kwanza nchini atapata kombe na sh. milioni tatu.
Makamu bingwa atapata sh. milioni mbili wakati mshindi wa tatu atapata sh. milioni moja. Kiingilio kwenye mechi hizo ni bure.
FRIENDS RANGERS YAPOTEZA MECHI KWA KUGOMA
Wakati huo huo, Mechi namba 120 ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kundi A kati ya Majimaji na Friends Rangers iliyochezwa jana (Januari 29 mwaka huu) Uwanja wa Majimaji mjini Songea ilivunjika dakika ya 38 baada ya Friends Rangers kugoma kuendelea na mchezo. Kwa kitendo hicho, Friends Rangers imepoteza mchezo huo. Hatua nyingine za kikanuni zitafuata baada ya kamati inayohusika kukutana.
Wakati huo huo, mechi ya FDL kundi A iliyochezwa leo (Januari 30 mwaka huu) Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam kati ya African Lyon na Ashanti United imemalizika kwa sare ya bao 1-1.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)