Na Mwandishi Wetu
SHIRIKA la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limeingia mkataba na klabu maarufu duniani ya Real Madrid ya Hispania wa kujenga kituo cha michezo kwa ajili ya kuzalisha vipaji.
Akizungumza katika hafla ya kusaini mkataba huo wa miaka 18, Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk Ramadhani Dau alisema ujenzi huo utagharimu Sh bilioni 16 na unatarajiwa kuanza kujengwa Mei mwaka huu na kwamba utakamilika baada ya miezi 18.
Dk Dau alisema kituo hicho ambacho kitajengwa kwenye kijiji cha michezo cha shirika hilo (NSSF Sports City), kitakuwa eneo la Mwasoga, Kigamboni, Dar es Salaam.
“Tuna eneo la zaidi ya ekari 400 ambapo tutajenga viwanja, shule ya michezo, nyumba za kuishi na maduka. Lengo letu tuzalishe na kuuza wachezaji. Tunakusudia kuwa na timu ya vijana chini ya umri wa miaka 13, 18, 20, timu B na timu ya wakubwa,” alisema Dk Dau.
Alisema utekelezaji wa kituo hicho utaanza hivi karibuni kwa kutumia majengo ya kukodi wakati wakisubiri ujenzi kukamilika.
“Hivi hapa baada ya kusaini mkataba, utekelezaji utaanza kwa kutumia majengo ya kukodi ambayo tunadhani yatakuwa maeneo ya Temeke na tutakuwa tukitumia viwanja vya Karume na Uhuru,” alisema.
Mkurugenzi Mkuu huyo wa NSSF alisema katika kuendesha kituo hicho, kila kitu kitafanywa na Real Madrid kuanzia masuala yote ya ufundi, kuwatambua wachezaji, chakula, wataalamu wa saikolojia na wataalamu wa viungo na kwamba wajibu wa shirika lake utakuwa kwenye kujenga tu.
“Sisi tunachukulia huu mradi ni uwekezaji na hatufanyi hisani, itazingatia misingi ya biashara na faida kubwa ni kwamba NSSF itaongeza kipato, lakini pia kituo kitatumika kuitangaza Tanzania kwa sababu yatakayofanyika yataoneshwa kwenye televisheni ya Real Madrid,” alifafanua Dk Dau.
“Lakini pia wakati umefika sasa kwa Tanzania kushiriki Kombe la Dunia Qatar 2022, kama unaandaa vizuri vijana wa miaka 13 sasa mpaka mwaka 2020 wanaweza kuwakilisha vizuri kwenye mechi za kufuzu na mwaka 2022 wakashiriki Kombe la Dunia, wakikosa la Qatar, basi hata hizo zinazokuja, hiyo pia ni moja ya madhumuni ya kituo hicho.”
Akizungumzia namna walivyofikia uamuzi wa kujenga kituo, Dk Dau alisema wazo hilo lilipatikana Agosti mwaka jana na kisha likapelekwa kwenye Mkutano wa Wanachama uliofanyika Arusha ambako waliazimia NSSF iwekeze rasmi kwenye michezo kabla ya kuwasilishwa kwenye bodi na utekelezaji kuanza kufanyika.
“Tulitembelea sehemu nyingi kuona wenzetu wanafanyaje. Binafsi nilitembelea nchi kadhaa za Ulaya, nilienda kituo cha Manchester United, Sunderland, Real Madrid kwa hapa Afrika nilikwenda Asec Mimosas (Ivory Coast) na TP Mazembe (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC) kuona wanafanyaje, ziara ikazaa matunda kwani tulikubaliana na Madrid na ndio wamekuja kusaini mkataba leo (jana),” alifafanua Dk Dau.
Naye Mkuu wa Vituo vya Michezo wa Real Madrid, Rayco Garcia aliishukuru NSSF wa kuwa na mpango huo na kuahidi kufanya kazi ili kuipatia Tanzania mafanikio. “Tukifanikiwa kuwatoa vijana hao, Tanzania itaweza kushiriki kwenye michuano mikubwa kama alivyosema Dk Dau, inabidi tufanye kazi ili vijana wafanikiwe, wafike mbali,” alisema Garcia.
Mbali na Garcia ambaye pia ni kocha wa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 18 ya Madrid, wengine walioambatana kwenye msafara huo ni Mkurugenzi wa Ufundi wa Klabu hiyo, Ruben de la Red, Kocha Mkuu wa timu za vijana, Francisco Martin Ramos na Juan Jose San Roman Milla. Mwaka jana, wachezaji wa zamani wa Real Madrid walifanya ziara nchini.