TTCL na Kampuni ya MS Huawei Technologies ya China imeingia mkataba ambao unalenga kujenga, kupanua na kuboresha mtandao wa TTCL wa simu za mezani, mkononi pamoja na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambapo miradi hiyo itagharimu zaidi ya kiasi cha Dola za Kimarekani 182.
Akizungumza katika hafla fupi ya kusaini mkataba huo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL- Dk. Kamugisha Kazaura, alisema awamu ya kwanza ya mradi huo inategemea kukamilika ifikapo mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu, 2015.
Alisema miradi ambayo iko kwenye mkataba itahusisha ujenzi wa mtandao wa teknolojia ya kisasa ya 4G Long Term Evolution (LTE), 3G – UMTS pamoja na 2G- GSM, teknolojia hizi zitasaidia Kampuni kupanua na kuboresha huduma zake nchi nzima na katika ubora wa hali ya juu. Teknolojia hizi zitatoa huduma bora ya sauti na intaneti (data) yenye kasi zaidi.
“…Mkataba huu pia unahusisha ununuzi wa mitambo kwa ajili ya kupeleka mawasiliano vijijini chini ya mpango wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF). TTCL imeshinda zabuni ya kupeleka mawasiliano katika kata 69 zinazojumuisha vijiji zaidi ya 400 vyenye wakaazi zaidi ya laki tano. Chini ya mradi huo UCSAF itaipatia TTCL Dola za Marekani milioni kumi kujenga miundo mbinu ya mawasiliano katika Kata hizo,” alisema Ofisa Mtendaji huyo wa TTCL.
Dk. Kamugisha Kazaura, aliongeza kuwa mkataba wa TTCL na Huawei ni moja ya juhudi zinazofanywa na Kampuni katika kutekeleza mikakati endelevu ili kuboresha na kupanua upatikanaji wa huduma nafuu za mawasiliano ya simu na intaneti nchi nzima.
Aidha, mikakati hii inaunga mkono juhudi za serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha huduma za simu na intaneti zinawafikia watanzania waliopo vijijini na mjini.
Hivyo, tunapenda kuwahakikisha watanzania na wateja wetu kuwa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) iko imara, na imejipanga kimkakati katika kuhakikisha inaendelea kutoa huduma endelevu, bora na nafuu kwa wateja wetu wa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.
Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) ni kampuni inayotoa huduma bora kwa makampuni makubwa ndani na nje ya Tanzania, pia imeunganisha nchi yetu na nchi za jirani Rwanda, Burundi, Malawi, Kenya, Uganda na Zambia kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano. Nchi hizo zimeungwa kupitia TTCL kwenda kwenye mikongo ya baharini ya SEACOM na EASSy pamoja na Kituo cha Mawasiliano ya Intaneti (IP PoP) cha TTCL.
Pia, inaunganisha taasisi za fedha, taasisi za afya na hospital, Wizara na taasisi zake, watoa huduma za intaneti (ISPs), watoa huduma za simu (telecom operators) ni baadhi ya wateja wetu wanaonufaika na huduma zetu mbalimbali tunazozitoa. Na hii inatokana na kuwa TTCL ni Kampuni pekee yenye miundombinu ya kuaminika, uhakika, yenye ubora na iliyosambaa nchi nzima.
Ili kupanua wigo wa matumizi ya mawasiliano ya simu na TEHAMA nchini nzima, Kampuni iko kwenye utekelezaji wa miradi mikubwa ya mageuzi ya kibiashara, kiufundi, masoko na mauzo. Utekelezaji wa miradi hii ulianza mwaka 2014 na unatekelezwa kwa awamu, hii ikiwa ni awamu ya kwanza na tunategemea kumaliza awamu zote mwaka 2017.
Kukamilika kwa miradi hii, italeta mabadiliko makubwa katika utoaji huduma kwa wananchi ambapo itaiwezesha TTCL kuwa kampuni inayotoa huduma bora zaidi na kwa bei nafuu. Katika eneo la ufundi tuna miradi ambayo inalengo la kuboresha mitandao yetu na huduma zinazotokana na mitandao, kupanua mitandao na kuhakikisha huduma za TTCL zinapatikana nchi nzima na kwa bei nafuu. Maboresho hayo, yatawezesha upatikanaji wa huduma za simu za mezani, mkononi pamoja na huduma za intaneti zenye ubora na kasi ya hali ya juu kwa wateja wetu nchi nzima.