RAIS wa Tanzania, Jakaya Kikwete ametuma salamu za rambirambi kuomboleza kifo cha Balozi na Mwanasiasa George Nhigula ambaye aliaga dunia usiku wa kuamkia Agosti 13, 2011 katika Hospitali ya Mikumi, Magomeni, Dar es Salaam kwa matatizo ya figo.
Mzee George Maige Nhigula ambaye alizaliwa Aprili 3, mwaka 1929, Wilaya ya Kwimba, Mkoa wa Mwanza, ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 82. Katika salamu ambazo ameitumia familia ya marehemu, Mheshimiwa Rais Kikwete amesema kuwa amestushwa na kuhuzunishwa na kifo cha Mzee Nhigula ambaye amemwelezea kama mzalendo halisi na wa kuigwa, na mtumishi hodari wa umma aliyeitumikia nchi yetu kwa moyo wa dhati na usiokuwa na kifani.”
“Nilipata nafasi ya kumjua Marehemu Nhigula katika uhai wake. Nilipata pia nafasi ya kufanya naye kazi kwa karibu wakati tukiwa wote Bungeni. Katika nafasi zote alizozishikilia akiwa mtumishi wa Serikali, akiwa Balozi wa Tanzania katika nchi mbali, akiwa mbunge mwakilishi wa wananchi wa Kwimba na akiwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mzee Nhigula alionyesha uzalendo usiopimika na moyo wa kuwatumikia wananchi usiokuwa na mipaka wala kifani.”
Ameongeza Rais Kikwete katika salamu zake hizo: “Taifa letu limepoteza Mzee mwingine ambaye kisima chake cha busara kilikuwa kinahitajiwa sana na wananchi wetu katika kipindi cha sasa. Tumepoteza mpiganaji mwingine shujaa wa Taifa la Tanzania.”
Amesema Rais Kikwete: “Nawatumieni salamu za dhati ya moyo wangu na pole nyingi kufuatia kifo cha Mzee wenu na Mzee wetu. Nawaombeni nyote wana-familia kuanzia kwa mama mjane, watoto, wajukuu, jamaa na ndugu wote mpokee salamu zangu hizi. Napenda kuwahakikishieni kuwa natambua machungu yenu katika kipindi cha sasa cha maombolezo.
Niko nanyi katika machungu yenu haya. Namwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Subira, awajalie subira na moyo wa uvumilivu katika kipindi hiki kwani yote ni Mapenzi yake. Aidha, namwomba Mwenyeji Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke peponi pema roho ya marehemu. Amen.”
Katika uhai wake, Marehemu Nhigula alikuwa ofisa mwandamizi katika Balozi za Tanzania katika Uingereza na Washington, Marekani, akaanzisha Ubalozi wa Tanzania katika Sweden mwaka 1962, akawa Katibu Mkuu wa Kwanza Mwafrika wa Wizara ya Kazi, na akawa Balozi wa Tanzania katika nchi za Misri, Uingereza, Japan na India.
Baada ya kustaafu utumishi wa umma, mwaka 1985 aligombea na kushinda Ubunge wa Jimbo la Kwimba, Mkoani Mwanza na akawa Mbunge kwa vipindi viwili hadi 1995. Wakati akiwa Mbunge pia alichaguliwa Naibu Spika wa Bunge.