Dodoma,
SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) lina mpango wa kuondoa nyumba ndogo katika maeneo yenye thamani kubwa yaliyojengwa holela mijini na badala yake kujenga maghorofa kukidhi mahitaji ya makazi.
Taarifa hiyo imetolewa juzi mjini hapa na Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu alipokuwa akimkaribisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuzindua ujenzi wa nyumba za makazi eneo la Medeli mjini Dodoma. Mchechu alisema mpango huo utaanzia eneo la Mikocheni “A” jijini Dar es Salaam.
Alisema watakaokutwa kwenye maeneo watapata haki ya kumilikishwa baadhi ya nyumba katika maghorofa yatakayojengwa na nyumba nyingine za ziada zitakazobaki Shirika litaziuza kwa wateja wengine, alisema.
“Kwa hivi sasa tunajadiliana na Manispaa na Wizara ili kutekeleza mpango huo ambao ni sehemu ya mkakati mkubwa wa Shirika kujenga nyumba nchini kote na kuziuza badala ya kujenga na kupangisha kama ilivyo sasa,” alisema.
Aliongeza kuwa maeneo mengine ya jiji la Dar es Salaam yatakayohusika na mpango huo ni Msasani na Kawe ambayo ni ya thamani kubwa lakini yamevamiwa na kujengwa bila ya mpangilio mzuri.
Kuna Sheria ya Utoaji Miliki za Sehemu ya Majengo (The Unit Tittle) inayowezesha kila mtu kuwa na miliki ya sehemu yake katika nyumba ya ghorofa iliyopitishwa hivi karibuni.
Katika uzinduzi wa jana, Waziri Mkuu aliweka jiwe la msingi kwa maghorofa mawili yenye nyumba 40 ambayo yamekamilika. Kutajengwa maghorofa yatakaokuwa na nyumba 290 hapo Medeli, ambazo kati yake 240 zitapangishwa kwa ajili ya Chuo Kikuu cha Dodoma kilicho jirani na 150 za kuuzwa, ambayo mojawapo imekwishauzwa kwa Sh. Milioni 99.
Hatua nyingine ya mpango wa NHC wa kuendeleza makazi nchini ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010, ni uendelezaji wa majengo yanayomilikiwa na Shirika hilo na kuyaendeleza maeneo mengine mapya. Bw. Mchechu alisema Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu Dodoma (CDA) imeipatia NHC eneo la ekari 264 nje kidogo ya mji wa Dodoma ili kujenga majengo ya makazi.
Akihutubia kwenye uzinduzi huo, Waziri Mkuu aliwataka wakandarasi wa ndani ya nchi ambao ndiyo pekee waliopata kazi ya kujenga nyumba hizo na NHC wasitie aibu kwa kushindwa kutimiza wajibu wao ama sivyo watafukuzwa.
“Msichakachue. Tekelezeni kazi zenu vizuri, watu wawasifie na mjenge uzoefu, vinginevyo itakuwa aibu na Mchechu (Mkurugenzi wa NHC) atawafukuza,” Mhe. Pinda alisema.