Rais Kikwete Amtumia Rambirambi Rais Mpya wa Mozambique, Nyusi

Rais Jaaya Kikwete

Rais Jaaya Kikwete


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Rais mpya wa Mozambique, Filipe Jacinto Nyusi salamu za rambirambi kuomboleza vifo vya watu 79 waliopoteza maisha yao kutokana na kunywa pombe yenye sumu.
Aidha, Rais Kikwete amewatakia watu wengine 174 ambao wamepata madhara ya viwango mbali mbali katika tukio hilo, baadhi yao bado wamelazwa hospitali, kupata nafuu ya haraka, ili waweze kurejea katika shughuli za maendeleo ya nchi yao na ya maisha yao.
Watu hao walipoteza maisha yao na wengine kuathirika afya zao wiki iliyopita wakati walipokunywa pombe inayodhaniwa ilitiwa sumu ya nyongo ya Mamba katika kijiji cha Chitima, Wilaya ya Cahora Basa, Jimbo la Tete.
Serikali ya Mozambique imetangaza siku tatu za maombolezo ya taifa na kuamuru bendera zote kupepea nusu mlingoti. Siku hizo zinamalizika kesho, Alhamisi, Januari 15, 2015.
Amesema Rais Kikwete katika salamu zake: “Nimesikitishwa na kuhuzunishwa na taarifa za vifo vya watu 79 ambao wamepoteza maisha yao kwa kunywa pombe yenye sumu katika Jimbo la Tete nchini mwako. Nakutumia Mheshimiwa Rais salamu zangu za rambirambi na naungana nawe kuomboleza vifo vya ndugu zetu hawa.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Nakuomba pia unifikishie salamu zangu kwa ndugu na jamaa wote ambao wamepoteza wapendwa wao katika tukio hili. Aidha, kupitia kwako, nawatakia wote ambao wameathirika katika ajali hiyo kupata ahueni ya haraka na kurudia maisha yao ya kawaida.”
Rais Kikwete vile vile ametoa pole nyingi kwa Rais Nyusi na Serikali yake kutokana na madhara ambayo yanasababishwa na mvua kubwa zinazonyesha nchini Mozambique ambazo pamoja na mambo mengine zilizoa madaraja makubwa matatu na kukata mawasiliano kati ya eneo la Kaskazini na la Kusini mwa Mozambique.