KITENDO cha baadhi ya wazazi kuendekeza unywaji wa pombe za kienyeji katika baadhi ya vijiji vilivyopo Kata ya Tembela Wilaya ya Mbeya Vijijini kimesababisha wazazi hao kushindwa kuwasimamia vizuri watoto wao hasa wanafunzi jambo ambalo limesababisha kupoteza mwelekeo.
Kauli hizo zilitolewa na baadhi ya viongozi wa vijiji mwishoni mwa mwaka jana walipokuwa wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi. Mwenyekiti wa Kijiji cha Usoa Njiapanda, Willson Mwamunyila akizungumza alisema baadhi ya wazazi wameshindwa kuzilea familia zao na kuendekeza ulevi jamboa ambalo ni changamoto kijijini hapo.
Alisema zipo baadhi ya familia zimetelekezwa na wanaume ambapo zimekuwa zikiishi kwa shida jambo ambalo linachangia hata baadhi ya watoto kushindwa kuendelea na shule na kubaki vijijini huku wakifanya vibarua kwenye mashamba ya watu.
Alisema akina mama ndiyo wameachiwa mzigo wa kuangaika na familia (watoto) huku akina baba wakiendekeza unyaji wa pombe siku hadi siku. “…Nimepokea malalamiko mengi sana juu ya baadhi ya wanaume kutelekeza familia na kuendekeza pombe hapa kijijini, unakuta mama ndiye anayeangaika na watoto baba anafanya vibarua mashambani akipata hela inaishia vilabuni,” alisema Mwamunyila akizungumza na mwandishi wa habari hizi.
Alisema vitendo vya baadhi ya wazazi kuendekeza pombe vimefanya baadhi ya watoto wanafunzi katika familia hizo kushindwa kuendelea na shule kwa kile kukosa mahitaji ya msingi hivyo wasichana kuamua kuacha shule wenyewe na kujiingiza katika shughuli za vibarua kujitafutia chochote.
Akizungumzia suala hilo, Kaimu Mtendaji wa Kijiji cha Usoha Njiapanda, Christopher Mwaryoyo alisema zipo taarifa za baadhi ya wanafunzi wa ie kupewa mimba na kukatishwa masomo, jambo ambalo pia uchangiwa na baadhi ya wazazi kuwatelekeza watoto wao katika kutimiza mahitaji nao kurubuniwa kirahisi.
Alisema suala la ulevi sasa wanapambana nalo kwa kuhakikisha vilabu vinafunguliwa kuanzia saa tisa muda ambao wananchi wanakuwa wamerudi kutoka katika shughuli za kilimo. Alisema hata hivyo Serikali ya kijiji inawashughulikia watu wote wanaosababisha mimba kwa wanafunzi na kuwakatisha masomo. “…Japokuwa ipo changamoto lakini Serikali ya kijiji sasa tunajitahidi kuwafuatilia wazazi wanaotelekeza familia na pia watu wanaotuhumiwa kuhusika kuwatia mimba wanafunzi…changamoto ni ushirikiano ubovu kutoka kwa wazazi wenyewe na wanafunzi wanaotiwa mimba,” alisema Mwaryoyo.