Azimio la Mtwara – Uwajibikaji Katika Uvunaji wa Maliasili ya Nchi Yetu

"Azimio la Mtwara" tarehe 31-12-2014 Zitto Kabwe na Prof. Ibrahim Lipumba

“Azimio la Mtwara” tarehe 31-12-2014 Zitto Kabwe na Prof. Ibrahim Lipumba


TANZANIA kama zilivyo nchi nyingi za bara la Afrika imejaaliwa kuwa na Rasilimali mbali mbali za asili. Miongoni mwa rasilimali hizo ni pamoja na Madini na Gesi Asilia. Usimamizi wa uvunaji wa rasilimali hizi umegubikwa na manung’uniko makubwa ya wananchi hususan kutokana na usiri mkubwa uliopo kwenye mikataba ya uvunaji wa Maliasili hizi za Taifa.

Mikataba yote 6 ya uvunaji wa Dhahabu bado ni Siri kubwa na vile vile mikataba yote 26 ya utafutaji na uvunaji wa Gesi Asilia na Mafuta. Mikataba miwili imevuja mpaka sasa na yote imeonyesha tofauti kubwa sana na mikataba ya mfano ambayo Serikali imeweka wazi. Mikataba ya mfano hutumika kujadiliana na makampuni ya uwekezaji katika utafutaji na uchimbaji wa Gesi na Mafuta hapa nchini. Mageuzi katika sekta ndogo ya gesi na mafuta yamekuwa hayashirikishi wananchi na hufanywa kwa usiri mkubwa na hivyo kusababisha wananchi kutokuwa na taarifa kabisa na kinachoendelea katika utajiri wao wa asili.

Mwaka 2007 nilitangaza Azimio la Songea lililokuwa na malengo makuu manne
1) kutokuwa na mikataba mipya ya madini mpaka mikataba iliyokuwepo ipitiwe. Mikataba yote ya madini ilipitiwa na Kamati ya Bomani na tangu mwaka 2007 hapajawa na mkataba Mpya wa madini ulioingiwa na Serikali.

2) kufanya mabadiliko ya sheria zote za kodi ambazo ni kikwazo katika kukusanya kodi katika sekta ya madini. Sheria husika zimefanyiwa marekebisho ikiwemo kupandisha mrahaba, kufuta nafuu ya kodi ya ongezeko la thamani kwa kampuni za madini na kuirejesha kodi ya ongezeko la mtaji.

3) Serikali kumiliki sehemu ya hisa katika migodi ya madini. Kwa mujibu wa sera Mpya ya madini ya mwaka 2009 na sheria Mpya ya madini ya mwaka 2010 Serikali itakuwa na hisa katika kila mgodi Mpya unaoanza nchini.

4) Halmashauri za Wilaya zenye migodi kupata mgawo wa theluthi ya mrahaba unaokusanywa katika madini yanayovunwa nchini. Pamoja na kwamba hivi sasa Halmashauri zinakusanya kodi ya ‘ cess’ lakini bado Serikali Kuu inabeba fedha yote ya mrahaba.

Malengo haya yaliongoza mjadala wa masuala ya madini mwaka 2007 mpaka 2010 sheria Mpya ya madini ilipotungwa. Utekelezaji wa Azimio la Songea ni wa zaidi ya 75% lakini bado kilio cha wananchi kipo pale pale. Hii inatokana na usiri mkubwa wa mikataba na hususan mikataba ya gesi na miundombinu yake. Usiri huu unasababisha ukosefu mkubwa wa uwajibikaji kwa upande wa watendaji wa Serikali. Usiri hupelekea rushwa na ufisadi.

Moja ya sababu kubwa zinazotolewa na watetezi wa usiri wa mikataba ni kwamba mikataba ile ina Siri za kibiashara na hivyo washindani wa kibiashara wataiba Siri za wenzao. Hoja hii ni nyepesi sana kwani makampuni yote makubwa yanayowekeza nchini yamesajiliwa katika masoko ya hisa kwenye nchi za magharibi na katika masoko hayo mikataba yao hulazimika kuwekwa wazi. Hivyo usiri huo ni kwa wananchi tu na sio kwa hao washindani. Makampuni mengi yaliyopo nchini yanamilikiwa na watu wale wale kupitia masoko ya hisa. Vile vile majirani zetu kama Msumbiji wameweka mikataba yao yote wazi.

Ni dhahiri kwamba moja ya sababu kubwa ya kushamiri kwa rushwa nchini kwetu ni ukosefu wa mfumo thabiti wa uwajibikaji. Ndio maana katika mkutano wa kufunga mwaka 2014 na kuukaribisha mwaka 2015 uliofanyika mjini Mtwara tarehe 31 Desemba 2014, niliwaomba wananchi wa Mtwara kuufanya mwaka 2015 kuwa ni mwaka wa kuwajibishana. Hivyo Azimio la Mtwara ni wito wa kutaka Uwazi na Uwajibikaji katika utafutaji na uvunaji wa mali asili za nchi yetu. Azimio la Mtwara lina malengo yafuatayo

1 kutaka mikataba yote inayohusu uvunaji wa rasilimali za nchi iwekwe wazi kwa wananchi na Bunge liipitie kuidhia kabla ya kuingiwa kwa mikataba hiyo

2 kutaka haki ya wananchi kuruhusu utafutaji wa madini au gesi na mafuta katika maeneo yao ( right of free prior informed consent )

3 kutaka sehemu ya mrahaba unaotokana na uvunaji wa Maliasili ya nchi kugawanywa kwa maeneo yanayovunwa rasimali hizo

4 kutaka mfumo wa mapato na matumizi ya mapato yasiyo ya kikodi ( rents ) yanayotokana na uvunaji wa Maliasili za nchi kuwa wazi kwa wananchi na kushirikisha wananchi katika kupanga matumizi husika kwa faida ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo

Azimio hili ni wito tu utakaotusaidia kuiwajibisha Serikali katika masuala ya utajiri wa Taifa.

Imeandaliwa na Zitto Kabwe, Mb