Dotto Mwaibale
ZAIDI ya dola za Marekani sh.bilioni moja zimetumika katika kukamilisha mradi wa ujenzi wa bomba la gesi , kati ya fedha hizo, Benki ya Exim ya China imechangia asilimia 95 na Serikali ya Tanzania asilimia 5.
Aidha, mradi huo umekua kwa asilimia 94 ya mradi mzima, ambapo unatarajiwa kukabidhiwa Juni mwaka huu, ambapo unatarajiwa kuondoa tatizo la mgao wa umeme nchini.
Imeelezwa kuwa kwa sasa jumla ya megawati 300 za umeme kila siku zinazalishwa kwa kutumia gesi asilia.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo asubuhi, Kaimu Meneja Mkuu wa Gas Supply Company Ltd (GASCO), Mhandisi Kapuulya Musomba alisema kiasi hicho cha fedha kinatumika kugharamia mtambo wa kusafisha gesi asilia wa Songosongo na kuwa umetumia dola bilioni 151, 735.
Musomba aliongeza kuwa mtambo wa kusafisha gesi asilia wa Mnazi Bay umetumia dola bilioni 197,877 na mradi wa bomba la kusafirishia gesi asilia umetumia dola bilioni 875,715.
“Kila siku ni lazima tupate taarifa kuwa ni watu wangapi wameajiriwa, ambapo zaidi ya watu 1,000 huajiriwa kupitia mradi huu” alisema Musomba.
Musomba alitaja maeneo ambayo yanatumia gesi asilia kuwa ni viwanda 37, magari 60, nyumba za watu 70, hoteli 1 na taasisi 2 za Mgulani na Gereza la Keko.
Aliongeza kuwa milioni 70 zinahitajika kusambaza miundombinu ya gesi asilia kwa maeneo ya Mtwara na Lindi.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Michael Mwande alisema mradi huo si kwa ajili ya TPDC bali ni wa umma wa Tanzania.
Alisema mradi huo ulitarajiwa kukamilika Desemba mwaka jana, lakini kutokana na ujenzi wa gesi ya Songo Songo na makazi ya waendesha mitambo umesabaisha uchelewe.
Hata hivyo, aliwataka wananchi kuelewa kwa undani kuhusu mradi huo ili uweze kuleta manufaa kwa wananchi na nchi kwa ujumla.
Mwenyekiti huyo alitaja hatua zilizochukuliwa kwa ajili ya usalama wa wananchi wanaoishi maeneo ambayo bomba limepita kuwa ni pamoja na kuangalia namna watakavyochimbia chini bomba hilo ili lisilete athari kwa wananchi wa eneo hilo.
Nyingine ni kuweka helikopta zitakazokuwa zinazunguka eneo la bomba ili kuangalia vitu vitakavyokuwa vinafanywa na wananchi katika eneo hilo sanjari na vibao vyenye namba za simu. (Imeandaliwa na mtandao wa www. habari za jamii.com)