TAARIFA za uvamizi wa kundi la wahalifu maarufu kama ‘Panya Road’ jijini Dar es Salaam zimezua taharuki kubwa na kusababisha wakazi wa wa jiji sehemu kubwa kufunga shughuli zao na kukimbilia majumbani kuhofia kuporwa na wahalifu hao.
Wananchi maeneo ya Mwananyamala, Kinondoni, Ubungo, Sinza, Buguruni, Tabata, Temeke na maeneo mengine ya jiji walilazimika kufunga maduka, baa na sehemu zingine za biashara na kuanza kukimbilia sehemu walizoona zina usala ili kujinusuru na taharuki hiyo ambayo ilisambaa kwa haraka maeneo mengi ya jiji.
Taarifa ambazo mtandao huu ulizipata kutoka kwa baadhi ya maofisa polisi waliokuwa doria zilisema ni kweli kundi la wahalifu wanaojiita panya road walivamia baadhi ya maduka na baa maeneo ya Mwananyamala na Kinondoni Studio na kufanya uporaji kisha kukimbia kabla ya taarifa kuenea maeneo mengi.
“…Ni kweli baadhi ya maeneo ya Mwananyamala kuanzia Studio walipita wahalifu hao lakini taarifa zimevumishwa zaidi kuwa wapo maeneo yote jambo ambalo limewafanya wananchi kufunga shughuli zao na wengine kukimbia hovyo mitaani…kuna vibaka nao wanatumia fursa hiyo ya woga na kupora,” alisema mmoja wa maofisa aliyekuwa katika gari la doria.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala alisema taarifa zinazoenea kwa sasa ni uvumi kwani hakuna tukio linaloendelea Polisi wa Doria wanazunguka maeneo ya Kinondoni, Sinza, Mwananyamala, Temeke, Tabata, Buguruni hakuna chochote zaidi ya wananchi kuendelea kutimua mbio kutokana na taarifa za uvumi zaidi walizopewa.
“Jamani hakuna cha panyaroad wala panyabuku askari wamezunguka mitaa yote ya Kinondoni, Sinza, Mwananyamala, Temeke, Tabata, Buguruni mambo swari ila watu wanakimbiana tu…” alisema Kamanda Kinondoni akizungumza na chombo kimoja cha habari.
Kwa upande wake Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Sulemani Kova akizungumza na vyombo vya habari usiku huu alisema tukio hilo lilitokea sehemu ndogo lakini baadhi ya watu walivumisha taarifa kana kwamba maeneo yote ya jiji yamevamiwa jambo ambalo limewafanya wananchi kuacha shughuli zao na kuanza kukimbia hovyo kuelekea majumbani. Alisema kutokana na hofu za uvumi wa taarifa na wananchi kutimua mbio hovyo baadhi ya vibaka wanatumia fursa hiyo kuendelea kuwatisha wananchi jambo ambalo alisema sio kweli na kuwataka wananchi waendelee na shughuli zao.
“…Jambo hili ukweli ni asilimia ndogo sana na uvumi ndio asilimia kubwa, mfano uvumi umesambaa kwa asilimia karibu 95 huku ukweli wa tukio ni asilimia kama tano tu…,” alisema Kamanda huyo wa Kanda Maalumu ya Polisi Dar es Salaam akitoa ufafanuzi kwa vyombo vya habari.
Mwandishi wa habari hizi ameshuhudia watu wakitimua mbio hovyo maeneo ya Mabibo, Ubungo, Extenal, Buguruni na Tabata huku sehemu kubwa ya baa na maduka yakiwa yamefungwa kutokana na taharuki ya kuwepo kwa vikundi hivyo karibuni maeneo yote ya jiji. “…Tumeambiwa mbwamwitu wanakuja maeneo ya Tabata ndio maana kila mmoja anakimbia kuelekea kwake,” alisema mmoja wa wanadada aliyekuwa akikimbia na wenzake maeneo ya Tabata Bima.