EXECUTIVE Chef Issa Kipande anayefahamika kama ‘Chef Issa’ (aliyeshika kombe) wiki hii amefanya makubwa kwa kuwa mmoja wa ma-Chef wa timu ya Stockholm, Sweden, kushiriki na hatimaye kushika nafasi ya kwanza kwenye kipengele cha timu za kanda kwenye mashindano ya Kombe la Dunia la Mapishi 2014 ‘Villeroy & Boch Culinary World Cup 2014’ yaliyofanyika nchini Luxemborg. Katika mashindano hayo ushindi wa jumla umechukuliwa na taifa la Singapore.
Kitendo cha kushinda kombe la dunia katika tasnia yoyote ni cha kijasiri hivyo haina budi kumpongeza Chef Issa kwa kuwakilisha vyema Watanzania na Waafrika kwa jumla. Mtanzania huyu anayefanya kazi nchini Sweden na Mtwara ambako amefungua hoteli yake hivi karibuni, ameshiriki katika mashindano hayo makubwa yanayofanyika kila baada ya miaka minne na yaliyoshirikisha ma-Chef zaidi ya 3000 kutoka nchi 56 za mabara yote matano ya dunia.
Mpaka sasa Chef Issa Kapande mbali ya kushinda tuzo nyingi tofauti katika fani yake ya upishi pia anashikilia rekodi ya kuwa Chef Mtanzania Msomi na mdogo kuliko wote aliyewahi kufungua na kuongoza hotel ya nyota tano akiwa Internationally Certified Executive Chef akiwa na umri wa miaka 25 tu. Hili ni jambo la kujivunia sana.
Chef Issa anasema kuwa Mola ajaliapo anatamani sana mwaka 2018 aipeleke Timu ya Taifa ya Tanzania mashindano haya. “Na nina imani tutafanya vizuri tu kwani kuna wapishi wazuri sana nyumbani Tanzania ingawa wamekosa nafasi au muongozo wa kuweza kuonyesha uwezo wao. Mungu ibariki Tanzania”, anasema.
Executive Chef Issa alipata pia heshima kubwa sana ya kuhudhuria executive lunch kwa watu maalumu tu iliofanyika wakati wa kutoa kombe la dunia kushoto ni Rais wa mashindano hayo na kulia ni mtoto wa mfalme wa nchi ya Luxembourg Crown Prince Guillaum.