Watanzania Wamuomba Pinda Ofisi ya Ubalozi Qatar

Waziri Mkuu wa Tanzania,  Mizengo Pinda.

Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda.


 
WATANZANIA wanaoishi nchini Qatar wameiomba Serikali iangalie uwezekano wa kufungua ofisi ya ubalozi nchini humo ili iwe rahisi kwao kufikisha matatizo yao na pia wawe na uhakika wa masuala yao kushughulikiwa kikamilifu. Wametoa ombi hilo kwa nyakati tofauti Desemba 20, 2014 wakati wakitoa hoja na amatizo yao mbele ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye yuko nchini Qatar kwa ziara ya kiserikali ya siku tatu.
 
Akizungumza kwa niaba ya Watanzania waishio Qatar katika mkutano uliofanyika kwenye hoteli ya Sheraton jijini Doha, Mwenyekiti wa Umoja wa Watanzania wanaoishi Qatar, Bw. Said Ahmed Said alisema ubalozi wanaoutegemea kwa sasa hivi uko Saudi Arabia ambako ni mbali na kwamba inakuwa vigumu kuwasilisha shida zote zinazowakabili Watanzania.
 
“Kwa mfano kuna suala la fursa za watoto wetu kusomeshwa elimu ya juu na kulipiwa na Serikali ya hapa. Inakuwa vigumu kupata hiyo fursa kwa sababu hakuna mtu wa kutusemea,” alisema Bw. Said na kushangiliwa na wenzake.
 
“Watoto wetu waliozaliwa hapa wakimaliza sekondari hawawezi kwenda Chuo Kikuu chochote kwa sababu mfumo wa hapa hauwaruhusu. Hata wale tuliowaacha nyumbani huwezi kuwaleta wakasomea hapa kwa sababu ya huo mfumo. Lakini wenzetu kutoka nchi nyingine wanapata hizo fursa kwa sababu wana quota yao. Tunaamini tukiwa na ubalozi hapa nchini, tutaweza kupata fursa kama wenzetu,” alisema.
 
Watanzania wengine waliochangia hoja ya kuwa na ofisi ni Bw. Abdallah Sima Abdalla (kutoka Zanziabar), Bw. Hersi Mohammed Adam (kutoka Singida) na Bw. Iddi Ali Ameir ambaye pia anatoka Zanzibar.
 
Hata hivyo, Bw. Hersi Mohammed Adam ambaye amefanya kazi kwenye kamouni ya Al Mazrui Oil Industries kwa miaka tisa, alisema kuna haja ya kuwaleta Watanzania wengi  wajifunze kazi ndogondogo zinazohusu uchimbaji mafuta kwani wana fursa ya kufundishwa wakiwa kazini. “Kuna kazi ambazo hazihitaji vyeti vya juu sana kama kusafisha mabomba ya gesi lakini pia ni za muhimu na zitawasaidia wengi kupata ajira wakati kazi kama hizo zikianza nchini Tanzania,” alisema.
 
Akizungumzia suala la kuwa na ubalozi, Waziri Mkuu alisema wazo lao ni la msingi ikizingatiwa kwamba kuna Watanzania zaidi ya 300 wanaoishi Qatar. “Hili suala ni la Serikali na mimi naona jibu la msingi ni kuwa na ofisi ya ubalozi hapa Doha kwa sababu mko wengi na tuna mahusiano ya karibu sana na wenzetu,” alisema na kuahidi kulifuatilia kwa sababu amekwishajadiliana na  Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk. Mahadhi Maalim ambaye yuko kwenye msafara wa Waziri Mkuu.
 
Akizungumzia suala la ajira, Waziri Mkuu aliwahakikishia Watanzania hao kwamba Serikali ya Qatar imesharidhia mkataba wa kuruhusu raia wa Tanzania waje kufanya kazi Qatar. “Sisi tulianzisha huu mkataba na wenzetu hawa wameuridhia mwezi uliopita… naamini utatusaidia sana kwenye suala la ajira za watu wetu lakini itabidi tuangalie ninyi ambao mlikuwepo zamani kabla mkataba haujasainiwa tunawafaya nini,” alisema.
 
Wakati huo huo, Waziri Mkuu Pinda alitoa nakala zipatazo 30 za Katiba Inayopendekezwa kwa Watanzania waishio Qatar na kuwataka waisome na kutoa mapendekezo yao hasa katika eneo la uraia pacha. “Hakikisheni mnaisoma na kujadili kwa kina eneo hili na kisha mtupe majibu yenu kwa sababu suala hilo liliibua mjadala mkubwa ndani ya Bunge Maalum la Katiba wakati likijadiliwa,” alisema.
 
Waziri Mkuu amefuatana na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Titus Kimani; Waziri wa Kilimo na Maliasili wa Zanzibar, Dk. Sira Ubwa Mamboya; Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk. Mahadhi Maalim; Naibu Waziri wa Nishati, Bw. Charles Kitwanga; Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Bw. Godfrey Zambi.
 
Wengine ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Bw. Abbas Kandoro, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Bi. Halima Dendego, wabunge wawili Bi. Amina Makilagi na Bw. Aeshy Hilali, Dk. Gideon Kaunda wa TPSF na Bw. Shigela Malocha kutoka TPDC.