RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, amemteua Dk. James P. Mataragio kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC). Kulingana na, Katibu Mkuu Kiongozi (KMK), Balozi Ombeni Sefue uteuzi huo ulianza tarehe 15 Desemba, 2014.
Dk. James P. Mataragio ni Mtanzania ambaye hivi sasa anaishi na kufanya kazi nchini Marekani akiwa Senior Geoscientist wa Kampuni ya Bell Geospace, Houston, Marekani. Wasifu wake ni kama ifuatavyo:-
ELIMU:-
• Masters in Business Development (MBA), Chuo Kikuu cha Charlotte, North Caroline, Marekani (2008)
• PhD (Geochemistry, Mineralogy, Structural Geology and Petroleum Geology), Chuo Kikuu cha Missouri – Rolla, Missouri, Marekani (2005)
• MSc (Geochemistry and Petrology), Chuo Kikuu cha Okinawa, Japan (1997)
• BSc(Hons) (Geology), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, 1994
UZOEFU WA KAZI:-
• Mwaka 2004 – hadi sasa, Senior Geoscientist, Bell Geospace Inc, Houston, Texas, USA
• 2001 – 2004, Mhadhiri Msaidizi, Chuo Kikuu cha Missouri, wakati akisoma Shahada ya Uzamivu
• 2000 – 2001, Mhadhiri Msaidizi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
• 1999 – 2000, Meneja Mradi, Anglo Gold (Buzwagi)
• 1994 – 1999 -, Exploration Geologist, Anglo America Corporation.
Miongoni mwa makampuni makubwa ya kimataifa ya mafuta na gesi aliyofanya nayo kazi kwa niaba ya mwajiri wake Bell Geospace ni pamoja na Petrobras (Brazil); BP; Anadarko; Tullow; Pemex (Mexico); ANP (Brazil), Ecopetrol (Colombia); Petronas, (Malaysia) na Vale Rio Doce.
Aidha, Dk. James P. Mataragio ni mmoja wa wataalam wa sekta ya madini, mafuta na gesi asilia waishio Marekani (Diaspora) ambao walijitolea kuishauri Serikali kuhusu sekta hiyo bila malipo.
Kwa kuzingatia elimu yake, uzoefu wake na uzalendo wake, Rais ana matumiani makubwa kuwa Dk. James P. Mataragio ataleta nguvu mpya na uzoefu mkubwa wa kimataifa katika kuiongoza TPDC ili iwe kampuni kubwa ya kitaifa ya mafuta na gesi asilia kama yalivyo makampuni mengine ya kitaifa ya mafuta na gesi asilia duniani.
Ateuliwa Msaidizi wa Rais
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Willy Kitima kuwa Msaidizi wa Rais – Nyaraka (Documentation) kuanzia Alhamisi iliyopita, Desemba 11, 2014. Kabla ya uteuzi wake, Kitima alikuwa Mratibu wa Taasisi ya Kupambana na Rushwa ya Biashara nchini ya Business Action Against Corruption (BAAC) Tanzania.
Taasisi hiyo inaendeshwa kwa ushirikiano kati ya Jumuiya ya Madola na Serikali ya Tanzania kupitia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (PCCB) na Taasisi ya Uendelezaji Sekta Binafsi nchini ya PPSF. Kitima pia amewahi kuwa Mkrugenzi Mtendaji wa Shirika la Kufutilia Nyendo za Rushwa Kimataifa la Transparency International (TI) nchini. Aidha, ana ujuzi wa shughuli za benki na vyombo vya habari.