MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohammed Gharib Bilal Desemba 10, 2014, amewahutubia wawakilishi wa Afrika katika Mkutano wa Mazingira Duniani (Cop20) unaofanyika jijini Lima, nchini Peru. Mheshimiwa Makamu wa Rais anahudhuria mkutano huu akimuwakilisha Rais Jakaya Kikwete ambaye ni Kiongozi wa Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabia Nchi. Mkutano huo wa jana ulikuwa na dhima ya Afrika baada ya mwaka 2015: Makubaliano Mapya kuhusu Mabadiliko ya Tabia Nchi.
Awali Mheshimiwa Dk. Bilal aliwaambia wawakilishi wa Afrika katika mkutano uliojumuisha Mawaziri wa Afrika wanaoshughulikia masuala ya Mazingira katika nchi zao kuwa, Afrika licha ya unyonge wake bado inalo jukumu la kusimama kidete katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na ili kufanikiwa katika jambo hilo ni muhimu kwa Bara hili kuwa na sauti ya pamoja.
Makamu wa Rais aliendelea kusema kuwa, Bara la Afrika lina kila sababu ya kuwa na mipango yake ambayo itatumika kushirikisha nchi za nje ya Afrika ili kwa pamoja Dunia iweze kuwa na kauli inayofanana yenye kulenga kukabiliana na majanga yanayotokana na mabadiliko ya Tabia Nchi licha ya kuwepo tofauti za kimaendeleo kati ya Afrika na nchi za mabara mengine.
Awali akizungumza kabla ya Makamu wa Rais, Waziri wa Mazingira wa Sudan ambaye ni Mwenyekiti wa kundi hili la Afrika Dk. Hassan Albdelgadir Hillal alisema, kundi la Afrika linapongeza uongozi wa Tanzania kupitia kwa Rais Jakaya Kikwete kwa namna unavyosimamia agenda hizi za mabadiliko ya Tabia Nchi na kusimamia upatikanaji wa sauti moja kutoka kwa nchi za Afrika. Dk. Abdelgadir aliendelea kusema kuwa, Afrika inatakiwa kutumia mkutano huu wa Lima kwa umakini ili kuhakikisha mipango inayofikiwa inapata kutambulika na kuonekana mwakani wakati mkutano kama huu utakapofanyika jijini Paris.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Dk. Binilith Mahenge ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mawaziri wa Mazingira kwa nchi za Afrika yeye alibainisha kuwa, viongozi wa nchi za Afrika wamekuwa mstari wa mbele kabisa kuhakikisha kuwa Afrika inasikika na kwamba anatarajia ushirikiano katika ngazi ya Mawaziri kuendelea hata pale atakapokuwa anakabidhi nafasi hiyo kwa Waziri wa Mazingira wa Misri.
Katika mkutano mwingine ambao pia ulikuwa mwendelezo wa Siku ya Afrika katika COP20, Mheshimiwa Makamu wa Rais Dk. Bilal alisisitiza kuwa Afrika inatakiwa kuhakikisha vijana na akina mama wanakuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na hali hii ya mabadiliko ya tabia nchi.
“Makundi haya ni muhimu sana kwa kuwa ndiyo yanayohusika moja kwa moja na shughuli za kila siku. Hatutaweza kufanikiwa kama tutayaacha makundi haya nyuma,” alisema Makamu wa Rais katika Mkutano huo ambao pia ulihutubiwa na Dk. Fatima Denton, Mkurugenzi wa Harakati Maalum kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kamishenbi ya Uchumi kwqa Afrika (UNECA).
Imetolewa na: Ofisi ya Makamu wa Rais Tanzania, Lima, Peru