Serikali Yatakiwa Kufanyia Kazi Mapungufu Haki za Binadamu

Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez akisoma hotuba kwenye maadhimisho ya siku ya haki za binadamu duniani yaliyoenda sambamba na mkutano wa kujadili utekezaji wa makubaliano ya haki za binadamu nchini na maandalizi ya ripoti ijayo.

Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez akisoma hotuba kwenye maadhimisho ya siku ya haki za binadamu duniani yaliyoenda sambamba na mkutano wa kujadili utekezaji wa makubaliano ya haki za binadamu nchini na maandalizi ya ripoti ijayo.

DSC_0102

Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bibi Mary Massay akitambulisha meza kuu wakati wa maadhimisho ya Siku ya haki za binadamu yaliyoenda sambamba na mkutano wa kujadili utekezaji wa makubaliano ya haki za binadamu nchini na maandalizi ya ripoti ijayo yaliyofanyika jana jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi  Wetu

MRATIBU Mkazi  wa mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez ameitaka serikali ya Tanzania pamoja na mafanikio makubwa katika kufanikisha amani na kutia saini mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu, kufanyia kazi maeneo kadhaa ambayo bado yanatishia sifa nzuri ya taifa hili. Maeneo hayo ni mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, wanawake vikongwe na ukatili kwa watoto.

Alisema taifa hili ambalo limekuwa kimbilio la wakimbizi,kuukubali kuwa makao ya mahakama mbili kubwa za kimataifa zinazoshughulikia haki za binadamu (ICTR na African Court of Human rights) sasa linashuhudia madhila kwa baadhi ya wananchi wake ambao huuawa kwa imani za kijinga.

Akizungumza katika siku ya mataifa ya haki za binadamu mjini hapa, Mratibu huyo pamoja na kutoa ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, alisema ili Tanzania iweze kutekeleza kwa umakini kauli mbiu ya mwaka huu “haki kwa wote  siku zote 365” maeneo yaliyotajwa yanastahili kufanyiwa kazi kwani ni changamoto kubwa.

Alisema Tanzania ambayo imetia saini na kuridhia mikataba ya haki za binadamu kama ya kuwatambua walemavu, kukabili ubaguzi dhidi ya wanawake (CEDAW) na ule wa kulinda haki za watoto (CRC) inaposherehekea siku ya haki za binadamu inakabiliwa na doa hilo la ukatili miongoni mwa watu wake.

Alisema ipo haja ya kuimarisha usalama wa makundi hayo kwa kuhakikisha kwamba mashauri yao mahakamani yanamalizika na haki kuonekana kutendeka . Alisema familia ambazo zimepoteza watu wake kwa namna ya kikatili wanahitaji si tu kuona haki inatendekea bali wahusika wake wakichukuliwa hatua na ulinzi kwa makundi hayo ukiimarishwa.

Aidha alisema kwamba anapata maumivu makubwa anaposikia kuwapo na taarifa nyingi za ukatili kwa watoto na kuendelezwa kwa mila mbaya zinazofunika haki za msingi huku wahusika wakiwa hawachukuliwi hatua au upelelezi ukidaiwa bado kukamilika.

Alisema kitendo cha kuchelewesha haki kutokana na upelelezi kutokamilika au kushindikana  kutokana na kukosekana kwa fedha au familia zenyewe kushindwa kutafuta haki kutokana na kutokuwa na fedha  kunavuruga jina zuri la nchi hii ambayo ina makabila mengi na tamaduni tofauti.

Alisema pamoja na ukweli kuwa matendo hayo kisheria ni haramu kukosekana kwa utashi kwa viongozi kukabiliana na changamoto zilizopo na kuachwa kwa mila mbaya kunawafanya wananchi wabaki katika mazingira ya kutotendewa haki. Alisema mfumo wa sheria lazima uonekane kufanya kazi ili kukabiliana na wavunjaji wa haki za binadamu.

“Ni matumaini yangu kwamba serikali ya Tanzania itaonesha kuwajibika kwake na kuhakikisha inaangalia changamoto hizi na kuziondoa ili kuwezesha kutekeleza haki za binadamu saa 24, siku saba za juma na siku 365 za mwaka” alisema na kuahidi kwamba Umoja wa mataifa katika hilo utaendelea kutoa ushirikiano.

Aidha alisema kwamba UN itaendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania kuimarisha  kamisheni ya haki za binadamu na utawala bora (CHRAGG) na taasisi nyingine za kijamii kuhakikisha kwamba kuna mfumo wa kulinda  haki za biandamu.

Aidha mratibu huyo ameitaka serikali ya Tanzania kukamilisha uongozi wa CHRAGG na pia kuangalia watetezi wa haki za binadamu wanapata ulinzi wa kutosha dhidi ya watu wanaowatishia maisha.

Naye Mkuu wa Balozi za Umoja ya Ulaya (EU) nchini Tanzania na Afrika Mashariki Filiberto Ceriani-Sebregondi  ameitaka serikali ya Tanzania kuangalia  mapendekezo matatu iliyokataa ambayo yanagusa haki za binadamu.

Mapendekezo hayo yalikuwamo katika mfumo wa Umoja wa mataifa wa kupitia mambo mbalimbali yanayohusu haki za binadamu (UPR). Balozi huyo alitaja mapendekezo hayo ni pamoja na kufuta adhabu ya kifo, kuweka umri unaoruhusu ndoa na kuchukua hatua za kulinda waandishi wa habari na kulinda utamaduni wa wananchi wake.

Alisema mambo hayo ni sehemu muhimu ya kutekeleza maazimio ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu. Aidha balozi huyo pia aliitaka serikali kukamilisha kamisheni ya haki za binadamu na utawala bora na kuiwezesha kufanyakazi zake zinazopaswa ikishirikiana na asasi za kiraia na wadau wengine wa haki za binadamu.

Hata hivyo alisema jumuiya hiyo itaendelea kufanyakazi na  serikali katika kuhakikisha kwamba haki za binadamu zinazlindwa. Hata hivyo balozi huyo amesema ni vyema kuendelea kuyafanyia kazi mapendekezo mengine 119 ambayo serikali ilikuwa imeyakubali na kuonesha mafanikio yake katika majadiliano yajayo.

IMG_6732

Pichani juu na chini ni baadhi ya mabalozi, wadau wa haki za binadamu na wageni waalikwa wakifuatilia hotuba mbalimbali zilizokuwa zikitolewa katika maadhimisho ya siku ya haki za binadamu duniani yaliyoenda sambamba na mkutano wa kujadili utekezaji wa makubaliano ya haki za binadamu na maandalizi ripoti ijayo.

DSC_0176

Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya watu duniani (UNFPA), Dk. Natalia Kanem akizungumza kwenye mkutano huo wa kujadili utekezaji wa makubaliano ya haki za binadamu na maandalizi ripoti ijayo.

IMG_6584

 

IMG_6556

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu THRDC Taifa, Bw. Onesmo Olengurumwa akiteta jambo na Balozi wa Sweden nchini Tanzania Lennarth Hjelmaker wakati wa mkutano wa kujadili utekezaji wa makubaliano ya haki za binadamu na maandalizi ripoti ijayo ulioenda sambamba na maadhimisho ya siku ya haki za binadamu duniani.

DSC_0128

Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bibi Mary Massay (kushoto) akiongozana na Mkuu wa Balozi za Umoja wa Ulaya (EU) nchini Tanzania na Afrika Mashariki, Filiberto Ceriani-Sebregondi (katikati) pamoja na Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez kuelekea sehemu maalum kwa ajili ya picha ya pamoja na washiriki wa mkutano wa kujadili utekezaji wa makubaliano ya haki za binadamu na maandalizi ripoti ijayo katika kuadhimisha siku ya haki za binadamu duniani.

DSC_0136

Mgeni rasmi Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Ali Hassan Rajab (wa pili kulia waliokaa) katika picha ya pamoja na wadau waliohudhuria mkutano wa kujadili utekezaji wa makubaliano ya haki za binadamu na maandalizi ripoti ijayo ulioenda sambamba na maadhimisho ya siku ya haki za binadamu duniani. Chanzo: MOblog).