Na Mwandishi Wetu, Dodoma.
HATIMAYE Bunge limepitisha bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini baada ya kuifanyia marekebisho na kuwasilisha mpango wa dharura wa kuondoa tatizo la mgawo wa umeme unaolikabili Taifa kwa sasa.
Bajeti hiyo ilipitishwa jana kwa mbinde baada ya wabunge kupongea mpango wa dharura kisha kuichambua kabla ya kuridhia mpango mzima.
Aliyekuwa na kazi kubwa jana mjini hapa ni Waziri wa wizara hiyo, William Ngeleja ambaye alipata wakati mgumu wa kuwashawishi wabunge ili kukubali kupitisha mapendekezo waliokuja nayo.
Akizungumzia mikakati waliyoiibua Ngeleja alisema ili kuondoa mgawo wa umeme na tatizo zima la upungufu wa nishati hiyo, Serikali itatumia sh. bilioni 523 kwa ajili ya kuzalisha umeme kutoka kwa wawekezaji anuai wanaofanya kazi hiyo nchini.
Aliongeza kuwa Serikali pia imefuta kodi kwa mafuta ya aina zote yatakayoingizwa nchini kwa uzalishaji nishati ya umeme. Ngeleja alisema hiyo yote itakuwa ni moja ya mikakati ya Serikali kuhakikisha wananchi hasa wa kawaida wanapata umeme usiokuwa na gharama kubwa.
Alisema gharama za uzalishaji wa umeme ni kubwa tofauti na mapato ya shirika la TANESCO hivyo kudai Serikali inalazimika kubeba mzigo wa kiwango kinachozidi. “…Mauzo ya TANESCO ni sh. bilioni 115…kuna upungufu wa sh. bilioni 408…Serikali itabeba mzigo huu,” alisema Ngeleja alipokuwa akihitimisha mpango huo.
Aidha aliongeza kuwa iwapo mpango huo utafanikiwa na kupatikana uhakikia wa umeme nchini, gharama za umeme zitafanyiwa marekebisho kwa wafanyabiashara wakubwa na si kwa watumiaji wa majumbani.
Alisema gharama za umeme zinazotozwa kwa sasa nchini ni za chini sana ukilinganisha na zinazotozwa katika nchi zote za Afrika Mashariki.
Hata hivyo, akifafanua zaidi mpango wa dharura wa Serikali amesema ndani ya kipindi cha Julai na Desemba mwaka huu, mkakati huo utaiwezesha TANESCO kutoa megawati 572 kutoka kwa wawekezaji anuai wa nishati hiyo.
Alizitaja kampuni zingine zilizoongeza uzalishaji umeme mbali na Symbion ni IPTL kutoka Megawati 20 za awali hadi Megawati 100 sasa hali ambayo imetokana na Serikali kupata fedha za kununulia mafuta ya uzalishaji.
Alisema mradi mwingine ni wa kampuni ya Aggreko ambayo imeingia mkataba na TANESCO na tayari mitambo imewasili nchini na kufikia mwishoni mwa Agosti mitambo hiyo itaanza kuzalisha megawati 100.
Ngeleja, aliongeza pia TANESCO imekubaliana na Shirika la Hifadhi ya Jamii nchini (NSSF) kuwa linunue mtambo wa kuzalisha megawati 150 na utekelezaji utanza Septemba, ambapo mtambo wa megawati 50 utafungwa na kufuatiwa na mwingine Oktoba wa megawati 50, kabla ya kuhitimisha na mwingine Novemba utaokuwa na megawati 50 tena.