Kikwete: Hakuna Mtanzania ataekufa kwa njaa

Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete.

Na Mwandishi Maalumu, Shinyanga

RAIS wa Tanzania, Jakaya Kikwete amewataka wakuu wa wilaya nchini kwa maeneo yanayoonesha dalili za uhaba wa chakula kutoa taarifa haraka ili ziweze kupatiwa chakula kwani taifa lina chakula cha kutosha, hivyo kuwataka Watanzania wasiwe na hofu.
Rais Kikwete amewahakikishia Watanzania kuwa hakuna Mtanzania yoyote ambaye atapoteza maisha kwa njaa kwani Tanzania kwa sasa ina chakula cha kutosha.
Rais Kikwete ametoa agizo hilo hivi karibuni mjini Shinyanga alipozungumza katika hafla ya futuru aliyowaandalia viongozi na wananchi wa Mkoa wa Shinyanga Ikulu ndogo ya mkoani Shinyanga.
Aidha amewasili mkoani Shinyanga mchana wa leo kwa ziara ya siku mbili mkoani humo na miongoni mwa mambo mengine ameshiriki katika mazishi ya Luteni Jenerali Silas Peter Mayunga kwenye Makaburi ya Wasabato ya Unyanyembe mjini Maswa.
Akijibu shukurani za Sheikh Mkuu wa Mkoa, Sheikh Ismail, Rais Kikwete amesema kuwa amepata habari na kujionea mwenyewe wakati anasafiri kwa gari kwenda Maswa kumzika Jenerali Mayunga kuwa zipo dalili za waziwazi za ukame ambao unaambatana na ukosefu wa chakula.
Amesema Mheshimiwa Rais: “Nimejionea mwenyewe hali ya ukame wakati wa safari yangu kwenda Maswa. Sikuona dalili yoyote ya vifurushi vya akiba ya chakula ambayo kwa kawaida ni dalili ya akiba ya chakula cha kutosha katika mkoa huu. Leo sikuona.”
“ Lakini napenda kuhakikishieni ndugu zangu kuwa tunacho chakula cha kutosha kabisa kuhudhumia kila eneo lenye uhaba wa chakula nchini. Hakuna Mtanzania ambaye atakufa kwa njaa kwa sababu chakula kiko cha kutosha kabisa,” Rais amewaambia viongozi hao wa Shinyanga.
Hata hivyo, Rais anasema kuwa ili Serikali iweze kujua haraka mahitaji halisi ya maeneo yenye dalili za uhaba wa chakula ama tayari upo uhaba, ni lazima wakuu wa wilaya watoe taarifa haraka kwa mamlaka husika ili wananchi waweze kupelekewa chakula mara moja.
“Nataka kuwaambieni wakuu wa wilaya kuwa hakuna aibu yoyote kwa nyie kusema kuwa maeneo yenu yanalo tatizo la njaa. Aibu itakuwa mkuu wa wilaya akikaa kimya kiasi cha wananchi katika eneo lake kuanza kupoteza maisha kwa sababu ya uhaba wa chakula. Hili hatutalivumilia. Mkuu yoyote ambaye ataona aibu kusema eneo lake lina njaa na watu wetu wakapoteza maisha, huyu tutamshughulikia,” amesema Rais.