RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amepokea Ripoti, nyaraka na ushauri wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu Akaunti ya Tegeta Escrow na atavifanyia maamuzi katika wiki moja ijayo.
Rais Kikwete ambaye alianza kazi rasmi Desemba 8, 2014 baada ya mapumziko ya kufuatia upasuaji aliofanyiwa mwezi uliopita, amepokea Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Umma (PAC) na Maazimio ya Bunge kuhusu Akaunti ya Tegeta Escrow.
Kufuatia kupokea nyaraka hizo, Rais Kikwete ameelekeza kuwa Ripoti ya CAG iwekwe hadharani kwa ajili ya umma kuweza kuisoma na kujua nini hasa kimesemwa na kupendekezwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Rais Kikwete ameelekeza kuwa Ripoti hiyo itangazwe kwenye magazeti yanayosomwa na watu wengi na kwenye mitandao ya kijamii, ili Ripoti hiyo iweze kupatikana kwa Watanzania wengi.
Rais Kikwete ameanza kupitia na kusoma nyaraka hizo na katika wiki moja ijayo atazitolea maamuzi kwa maana ya kwamba yale mambo yanayomhusu yeye moja kwa moja atayatolea maamuzi yeye, yale yanayohusu Serikali atayatolea maagizo na maelekezo ya namna ya kuyashughulikia.
Wakati huo huo, Rais Kikwete jana, Jumatatu, Desemba 8, 2014, alianza kazi rasmi baada ya afya yake kuimarika kufuatia upasuaji aliofanyiwa mwezi uliopita.
Mhe. Rais alianza kazi rasmi kwa kumwapisha Mkuu mpya wa Mkoa wa Arusha, Mheshimiwa Daudi Felix Ntibenda katika shughuli fupi iliyofanyika Ikulu, Dar Es Salaam.
Kwa kuanzia Mhe. Rais atakuwa anafanya kazi za ofisini na kwa muda mchache. Muda na kasi ya kufanya kazi ya Mhe. Rais vitaongezeka kwa kadri afya yake inavyozidi kuimarika.
Na kwa sababu sasa ameanza kazi, Mhe. Rais ataanza kushughulikia mambo yale ambayo yamekuwa yanasubiri maamuzi yake.
Rais Kikwete alifanyiwa upasuaji wa tezi dume katika Hospitali ya Johns Hopkins ya Baltimore, Maryland, Marekani Novemba 8, mwaka huu na alirejea nyumbani Novemba 29, mwaka huu.
Tokea awasili nyumbani, Mhe. Rais amekuwa anafanya mazoezi asubuhi na jioni kuimarisha afya yake kama alivyoshauriwa na madaktari.