Na Mwandishi Wetu, Mbinga
UONGOZI wa Muunganisho wa Ujasiriamali Vijijini (MUVI) umekagua jengo ambalo umepanga kuweka mashine ya usindikaji wa zao la mhogo, wilayani Mbinga itakayotumiwa na kikundi cha MUVI kijiji cha Kilosa. Uongozi huo umefanya kazi hiyo hivi karibuni ulipotembelea kijiji hicho mkoani Ruvuma.
Akizungumza katika ziara hiyo, Kaimu Meneja wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogovidogo (SIDO) mkoani Ruvuma, Athur Ndedya amewataka wana-Kilosa kuutumia mradi huo ambao tayari umeanza kuonesha mafanikio makubwa. Jengo hilo linatarajiwa kufungwa mashine ya kusindika mhogo ambayo inatolewa kwa ushirikiano wa MUVI na SIDO.
“Tuna amini tunao mhogo wa kutosha eneo hili hivyo mfanye kazi kwa bidii na kuondoa tofauti zenu, umoja ndiyo msingi wa mafanikio…inapaswa kufanya kazi kwa umoja kwani hali ya maisha ni ngumu kwa sasa, jengo limekidhi vigezo hivyo wakati wowote mtapokea mashine ya kusindika mhogo.
Alisema zao la mhogo ni moja ya zao la pekee ambalo linamatumizi mengi na kuongeza kwani linaweza kutumika kutengeneza biskuti, mkate, clips, tambi na vitafunwa mbalimbali hivyo kuwataka kulizalisha kwa kiwango kikubwa.
Naye Ofisa Biashara wa SIDO, Ruvuma, Stephano Ndunguru amewataka wanakijiji hicho kuzitumia fursa zinazojitokeza ipasavyo kwa lengo la kukuza uchumi wao na eneo husika jambo ambalo linaweza kuwatambulisha ndani na nje ya nchi.
“Nayasema haya kwani kadri maendeleo yanapoongezeka na ugumu wa maisha unazidi, tusipo jipanga tutakuwa watazamaji na kuruhusu fursa hizo kwenda kwa wageni. Mfano mzuri eneo lenu limebahatika kuwa Makao Makuu ya Wilaya mpya ya Nyasa lakini inasemekana sehemu kubwa ya maeneo yaliyopimwa yamechukuliwa na wageni, hatusemi wageni wasije la hasha…waje lakini watukute tupo pazuri watatuheshimu, wakitukuta hatuna muelekeo wanaweza kutudharau.
Hata hivyo, Ofisa Habari wa Mradi wa MUVI, Ruvuma, Dunstan Mhilu amewataka wanakijiji hao kuondoa hofu juu ya soko la bidhaa zao kwani idara yake ya mawasiliano imejiandaa kuhakikisha bidhaa za mhogo wa Kilosa zinatangazwa ndani na nje ya nchi.
Aliongeza taarifa za soko zitachapishwa magazetini, zitatangazwa redioni, kwenye Jarida la MUVI ‘Nuru Magazine’ (Nuru ya mafanikio) pamoja na gazeti mtandao la dev.kisakuzi.com (www.thehabari.com) na pia tovuti ya www.muvi.go.tz inayomilikiwa na asasi hiyo.
“Changamoto ya soko la mhogo inatambulika lakini mawasiliano katika biashara vijijini ni moja ya silaha ambayo MUVI inaitumia kupambana na ulanguzi wa bidhaa, elimu na kuboresha uelewa wa bei nakuwajengea uwezo ili kuongeza thamani ya bidhaa na soko linalokidhi kiwango cha mlaji.
Mtendaji wa Kijiji hicho, Aidan Nchimbi ameishukuru MUVI na SIDO pamoja na Mbunge wao wa Mbinga Magharibi, John Komba kwa kuwasaidia sh. milioni 4 zilizogawanywa kwa vikundi vine kijijini hapo.
Pichani juu ni Ofisa Habari wa MUVI Ruvuma, Dunstan Mhilu akitoa mafunza kwa wajasiriamali wa Kijiji cha Kilosa, wilayani Mbinga, kulia kwake (mwenye suti) ni Kaimu Meneja wa SIDO, Ruvuma, Athur Ndedya, na anayemfuatia mwenye fulana ya SIDO ni Ofisa Biashara wa SIDO Ruvuma.