*TFF Yataja Kiingilio katika mchezo huo
MECHI ya Nani Mtani Jembe 2 kati ya Simba na Yanga zinazodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itachezwa Jumamosi, Disemba 13, 2014 saa kumi kamili jioni kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Meneja Udhamini wa TBL, George Kavishe amesema kwamba “Tayari Simba na Yanga zimesaini makubaliano ya kucheza mechi ya Nani Mtani Jembe 2 (Nani Mtani Jembe 2 Match). Pambano hili ni zawadi ya kufungia mwaka kwa mashabiki na kila timu imetia saini makubaliano kwamba itachezesha kikosi cha kwanza ili kuwapa mashabiki burudani ya uhakika.”
Kavishe aliongeza kuwa mechi hii ni maalumu kwa ajili ya kuhitimisha kampeni ya Nani Mtani Jembe 2 ambayo imeendeshwa kwa zaidi ya miezi miwili ikiwapa fursa mashabiki wa timu hizi kuchangia timu zao kila wanapoburudika na bia ya Kilimanjaro Premium Lager.
Alisema Nani Mtani Jembe 2 inahusisha mashabiki wa klabu za Simba na Yanga ambapo zawadi ya shilingi milioni 100 itatolewa na kugawanywa ifuatavyo.
• Shilingi Milioni 20 ni zawadi ya mechi ya Nani Mtani Jembe ambapo timu itakayoshinda itapata sh milioni 15 na timu itakayofungwa itapata shilingi milioni 5.
• Kampeni hii inaendeshwa kwa njia ya sms ambapo mashabiki wanapiga kura kwa njia ya sms na shilingi milioni 80 zimegawanywa kati ya timu hizo mbili ambapo kila timu ilianza na shillingi milioni 40 kwenye benki maalumu mtandaoni.
Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Pamela Kikuli alisema mashabiki wa Simba na Yanga wanaweza kushiriki kwa kununua bia ya Kilimanjaro Premium Lager yenye ujazo wa mililita 500 ambapo mteja atabandua ganda la kizibo cha bia ya Kilimanjaro Premium Lager na kuona namba maalumu. Ataandika jina la timu yake (SIMBA au YANGA) ikifuatiwa na namba hiyo ya kwenye kizibo ambayo anatuma kwenda namba 15415 na kwa kufanya hivyo anakuwa amepunguza pesa taslimu shilingi 10,000 kutoka timu pinzani na kuichangia timu yake.
Kikuli pia alizikabidhi timu hizo jezi maalumu itakayovaliwa mahususi kwa ajili ya mechi hiyo na kuwahimiza mashabiki waendelee kuzipigia kura timu zao na kikubwa kuhakikisha wanafika uwanja wa taifa na kujionea wenyewe pambano hilo ambalo lazima mshindi apatikane.
Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura aliwakaribisha mashabiki na kuwaomba wajitokeze kwa wingi kwani hivi sasa timu hizo ziko kambini zikijiandaa na mtanage huo wa kukata na shoka unaotarajiwa kuwa na msisimko mkubwa.
Alitaja viingilio vya mechi hiyo kuwa ni shilingi 30,000 kwa VIP B, 20,000/= VIP C, 15,000/= kwa viti vya rangi ya chungwa kiingilio kitakuwa ni sh 15,000 huku viti vya bluu na kijani tiketi zikiuzwa kwa sh. 7,000/=.
Wambura alisema pambano hilo litakalosimamiwa na TFF litaanza saa kumi kamili na litachezwa kwa dakika 90 tu ambapo kama muda huo timu hizo hazitafungana basi mikwaju ya penati itapigwa ili mshindi apatikane.
Taji la Nani Mtani Jembe linashikiliwa na Simba ambao waliwafunga mahasimu wao 3-1 katika mechi iliyochezwa Disemba 21, 2013.