Mimi napenda uigizaji; uwe katika filamu, vichekesho, maigizo n.k. kama vimetengenezwa katika kiwango kinachoridhisha huwa napenda kuangalia bila kujali igizo hilo limetengenezwa na wasanii wa nchi gani. Ninachoangalia je, ipo katika lugha ninayoijua?, Je, inanifurahisha au kunituliza kwa kiwango ambacho mimi nakitaka? Kwa maana hiyo naangalia filamu na maagizo kutoka katika nchi mbalimbali.zikiwemo zile zinazotengenezwa toka katika nchi yangu Tanzania. Natambua sana kwamba katika sanaa hii bado viwango vyetu vipo chini.
Pengine hilo linahitaji kujitokeza kwa watu wenye uwezo wa kutunga hadithi nzuri, kuandaa misuada mizuri na watu wengine wenye weledi katika nafasi mbalimbali za sanaa hiyo. Pamoja na hayo kwa kiwango fulani filamu zetu na wasanii wanakubalika hapa nchini na nchi nyingine za jirani. Hivyo kwangu mimi siwezi kusema kuwa viwango hivyo vya chini vinatudhalilisha. Kinachonisikitisha ni Kiingereza kibovu kinachotumika kutafsiri filamu za kiswahili. Huu ndio naona ni udhalilishaji, na ni udhalilishaji unaoweza kuepukika. Ni kwa nini katika nchi hii iliyo na watu wanaojua lugha ya Kiingereza vizuri iwe na filamu za kiswahili zenye tafsiri ya Kiingereza inayotia aibu kiasi hiki? Mimi najisikia vibaya sana ninapoangalia filamu hizo na kusoma tafsiri hizo zinazodhalilisha.
Najiuliza hivi hawa wasanii wanataka kuyaambia mataifa ya nje kwamba katika nchi hii hakuna watu wanaoijua Kiingereza? Sisemi kutojua Kiingereza ni vibaya la hasha. Kwa nini niwang’ang’anize watu kujua lugha isiyo yao? Ninachokinyooshea kidole ni ile hatua ya kutengeneza lugha ambayo haipo. Kwa kweli niliangalia filamu moja ya Kitanzania na kuangalia ile tafsiri ya Kiingereza iliyokuwa imewekwa kwenye mazungumzo ya Kiswahili kilichokuwa kinatumika kwenye filamu hiyo nikaona mambo ya ajabu. Ilikuwa ni aibu kwa mtengenezaji wa filamu hiyo, Baraza la Sanaa la nchi hii ambao wanaona ni sahihi kwa filamu kama hiyo kurushwa na ni aibu kwa Watanzania wote kwa ujumla. Kiingereza kilikuwa kibovu mno kisichoweza kuvumilika.Mimi nafikiri kama hakuna ulazima wa kuweka tafsiri za lugha nyingine kwenye filamu hizo basi tusiweke kabisa. Kama tunaona kuna ulazima au umuhimu basi Baraza la Sanaa lihakikishe kwamba filamu iliyowekewa tafsiri ya lugha nyingine imetafsiriwa kwa lugha sahihi inayokubalika.
Hivyo kama ni Kiingereza basi kitumike Kiingereza sahihi siyo mkusanyiko tu wa maneno ya Kiingereza. Pengine wasanii wenyewe wanaweza kusema aah si mtu anaangalia vitendo kwenye picha hivyo anaielewa filamu. Wasanii hawa waelewe kwamba wananchi wa Tanzania tayari tumewekwa gredi ya chini katika masuala ya taaluma tukilinganishwa na wenzetu wa nchi nyingine hapa Afrika Mashariki. Kigezo kimoja wanachokitumia ni kushindwa kwetu kumudu lugha ya Kiingereza ambayo wanajua ndiyo inayotumika kufundishia toka shule za sekondari mpaka vyuo vya juu.
Hilo limetuathiri sana katika soko la ajira mpaka katika nchi yetu wenyewe. Wakati tunaendelea kupinga hilo wanajitokeza wasanii na kuuthibitishia ulimwengu kwamba ni kweli hayo wanayoyafikiria. Wanafanya hivyo kwa kukitangaza hicho Kiingereza kibovu kwa watu wote wanaoangalia filamu hizo. Watazamaji hao hawasemi Kiingereza cha wasanii wa filamu hii ni kibovu bali wanasema “Watanzania bwana, kweli ni mbumbumbu hebu angalia hicho kinachopita kwenye ‘screen’. Hii ni kutudhalilisha sisi Watanzania hasa wale ambao wanajua wangeweza kuweka tafsiri za Kiingereza sahihi kwenye filamu hizo.
Pengine kuna wasanii ambao wamezoea kujidhalilisha hivyo hawaoni kama kuna tatizo. Wasanii hawa wa uigizaji wakumbuke kwamba kuna mambo ya msingi ambayo binadamu anayahitaji kwa sababu ya hisia zake za kiubinadamu. Baadhi ya mahitaji hayo ni kuheshimiwa, kukaribishwa, kuwa na utulivu, kueleweka, kujisikia ni wa muhimu n.k. Hakuna mtu mwenye akili timamu anayependa kuyakosa hayo. Mtu mwenye akili zake timamu hawezi kufurahishwa na tendo la yeye kudharaulika, anapenda watu wamuone yeye ni mtu muhimu mwenye heshima zake. Hakuna mtu mwenye akili zake timamu anayependa afanye mambo yatakayoishia kumdhalilisha. Kweli binadamu anafanya mambo mengi ama kwa kudhamiria ama kwa kutojua ambayo yanaishia kumdhalilisha; lakini amini usiamini pale anapotenda hajui kama kuna siku yatakuwa wazi na yatamuumbua na kumdhalilisha.
Kudhalilika kunamfanya mtu akose amani, ajisikie vibaya sana kisaikolojia; wapo wengine wasioweza kuvumilia huwa wanafikia hatua ya kujiua kwa sababu tu wanajiona wamedhalilika. Mimi siungi mkono hatua ya mtu kujiua kwa sababu tu anajisikia amedhalilika bali naweka hadharani kwamba kudhalilika ni jambo baya sana, iwe umedhalilishwa na mtu mwingine kwa jambo ambalo pengine halina hata ukweli au matendo yako mwenyewe yamekufikisha hapo. Hivyo ukiona mtu anafanya vitendo ambavyo hajali kwamba vinamdhalilisha basi ujue kabisa kwamba kuna kasoro katika akili ya mtu huyo. Haijalishi kama mtu huyo yupo Hollywood au Tollywood. Wapo baadhi ya wasanii ambao tayari sisi Watazamaji tumewaweka katika kundi la wao kuwa na asilimia fulani ya upungufu wa akili lakini tumewaacha kwa sababu wanajidhalilisha wenyewe siyo sisi. Ila hili la Kiingereza kibovu tutalipigia kelele kwa sababu linatudhalilisha na sisi.
Pamoja na baraza la sanaa wasanii wenyewe wameanzisha umoja wao; kuna Swahili Films Association na Bongo Movies. Vyombo vyote hivi vinatakiwa kuhakikisha kwamba filamu zilizo chini ya umoja wao zinatengenezwa kwa ubora unaohitajika ikiwemo kupata tafsiri sahihi ya lugha. Watu wanaojua Kiingereza wapo na wanaweza kuifanya kazi hiyo vizuri tu. Sielewi kama wasanii wanashindwa kupata watu sahihi au wanapunguza gharama kwa kutumia watu wasio na weledi. Kama ni kupunguza gharama halafu kuishia kutengeneza kitu hafifu basi wasanii wanakosea. Hii ni karne ya mapokezi ya kilicho bora, wao watafikiriaje vinginevyo? Nao wenye uwezo wa kutoa tafsiri sahihi za Kiingereza wajitokeze ili wasanii wawatambue na kuwatumia.
Kwa pamoja tunaweza kuboresha filamu hizo na kujiondolea kudhalilika.
Chanzo: Mwananchi