TGNP Kufanya Mjadala wa Wazi Maadhimisho ya Siku 16 Kupinga Ukatili

Lilian Liundi TGNP, Mtandao.

Lilian Liundi TGNP, Mtandao.

TGNP Mtandao ni asasi ya kiraia isiyokuwa na mrengo wa kidini iliyoanzishwa na kusajiliwa zaidi ya miaka 20 iliyopita ikijihusisha na mapambano ya kuleta usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake na makundi mengine yalioko pembezoni kwa njia ya ushawishi na utetezi, machapisho na mafunzo kwa njia mbalimbali kupinga ukatili wa kijinsia na kuleta mabadiliko ya kijamii kama sehemu ya haki za binadamu.

Pia TGNP Mtandao hushirikiana na asasi na mashirika mengine ya ndani na nje ya nchi kila mwaka katika kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia. Licha ya juhudi mbalimbali za kupambana na ukatili wa kijinsia nchini, bado hali ni mbaya, ambapo takwimu za wizara ya afya zinaonesha, katika mwaka 2013 asilimia 23% ya wasichana wenye umri kati ya miaka 15 na 19 walikuwa na mimba au walikuwa na watoto huku zikionesha kuwa asilimia 18% ya wasichana wa umri huo huolewa utotoni.

Takwimu hizo pia zinaonesha kuwa bado ukeketaji ni tatizo kubwa likiwa bado linatendeka kwa asilimia 15%. Katika kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia mwaka huu, TGNP Mtandao imeandaa mjadala wa wazi utakaofanyika Desemba 3, 2014 kuanzia saa 3 asubuhi katika viwanja vya TGNP Mtandao, Mabibo Dar es salaam.

Kauli mbiu ya kitaifa mwaka 2014 katika kuadhimisha siku hizo ni “Funguka! Fichua Ukatili kwa maendeleo ya jamii”. Katika kuadhimisha siku hizo, TGNP Mtandao itafanya mjadala wa wazi utakaoshirikisha zaidi ya watu 500 kutoka katika makundi mbalimbali ya kijamii wakiwemo wanachi kutoka vituo vya TGNP Mtandao vya taarifa na maarifa kutoka mikoa mbalimbali nchini, makundi yalioko pembezoni, mashirika ya kiraia, wadau wa maendeleo, wasanii na viongozi wa taasisi mbalimbali za umma.

Aidha kauli mbiu itakayoongoza mjadala huo ni “Siyumbishwi, Najilinda, Mnilinde” unaojikita kwa vijana hasa wa kike ikiwahimiza wasiyumbishwe, wajiepushe au wajilinde na mambo au mazingira hatarishi na kuitaka jamii iwajibike kuwalinda na kuwakinga vijana dhidi ya ukatili wa kijnsia unaotokea katika mazingira mbalimbali katika nchi yetu.

Mgeni rasmi katika mjadala huo, atakuwa Katibu Mjendaji wa Tume ya Haki za Binadamu Tanzania Bi. Mary Massey. Wageni wengine mashuhuri ni pamoja na wasaanii nyota nchini wakiwemo Vanessa Mdee, Christian Bella na wengineo. Msanii Christian Bella na wasanii wengine kutoka ngazi ya Jamii ambao atapata nafasi ya kutoa burudani za kufundisha na ujumbe maalum kwa siku hiyo.

Malengo ya mjadala huo ni kujadili na kuwezesha uelewa juu ya umuhimu wa mgawanyo wa rasilimali katika kupambana na ukatili wa kijinsia na kuboresha afya ya jamii na kuondokana na madhara yatokanayo na tohara kwa wanawake na mimba za utotoni. Mjadala huo pia ni nafasi kwa washiriki kuonesha mafanikio, kutoa shuhuda na kueleza changamoto wanazokumbana nazo katika kupambana na ukatili wa kijinsia na hivyo kujiimarisha katika kukabiliana na changamoto hizo.

Vijana watapata fursa ya kufunguka kuhusu rushwa ya ngono inavyoukwa kikwazo katika maendeleo yao shuleni, vyuoni na hata kazini. Pia kutakuwa na wasaha wa zulia jekundu ambapo vijana watakula kiapo cha kutojihusisha na ukatili wa kijinsia katika maisha yao yote.

Imetolewa na; Lilian Liundi,
Kaimu Mkurugenzi, TGNP Mtandao