UKIFIKA Wilaya ya Newala Mkoa wa Mtwara jitahidi utembelee eneo maarufu linalojulikana kama shimo la Mungu. Ni shimo kubwa la kuvutia huku likiwa linatisha pia kimuonekano. Ndani ya shimo ni kama eneo la mbuga ndogo na inaaminika kuna baadhi ya wanyama wakali pia. Wenyeji wameamua kuliita jina shimo la Mungu kutoana na maajabu wanayodai hutokea katika shimo hilo.
Kwa muonekano ni kama mmomonyoko wa udogo uliosababisha kutokea kwa shimo kubwa huku likidaiwa kuwa na maajabu na wakazi wanaozunguka eneo hilo. Kimtazamo linavutia na laweza kuwa sehemu ya utalii. Shimo hilo refu na la kitambo kidogo kwa sasa linazidi kuongezeka kiukubwa na kusogelea eneo la makazi lenye majengo jambo ambalo laweza kuwa hatari kiusalama.
Baadhi ya wakazi wa eneo hilo wanasema sehemu hiyo inaogopwa na kuheshimiwa kutokana na imani walizonazo juu ya matukio, muonekano na mazingira ya shimo hilo. Wanasema ndani ya shimo hilo kuna ishara na mambo ya kutisha. Wanasema kuna kipindi ndani ya shimo huonekana moto unaowaa bila kuchoma misitu iliyomo ndani ya shimo hilo. Pia unapolisogelea muda wote kuna mvuke mkali wenye ishara ya joto kubwa kutokea ndani la shimo hilo na mara nyingi unapokuja nyakati za asubuhi na usiku eneo hilo la shimo huonekana kama tambalale.
Wengi wanaoangukia au kuingia ndani kabisa ya shimo hilo hawatoki salama. “…Shimo hili ni hatari sana huwezi kuingia humu na ukatoka salama lazima upotee kimiujiza na hata mwili wako hauwezi kupatikana tena…kama huamini jaribu kuingia humo uone,” anasema mkazi mmoja ambaye nilimkuta jirani na eneo hilo.
Anasema kwa sasa shimo hilo kubwa linazidi kuongezeka kiasi cha kutishia usalama wa wananchi wanaokaa umbali mfupi na lilipo shimo hilo. Baadhi ya wakazi wameanza kujaribu kutupia takataka pembezoni mwa shimo hilo ili kupunguza kasi ya mmomonyoko wake unaozidi kuongeza ukubwa wa shimo hilo siku hadi siku.
Hata hivyo, pembeni ya Shimo la Mungu lipo jengo la Kituo cha Redio Newala (Newala FM) kinachomilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Wenyeji wa eneo hilo wanaamini na kituo hicho cha matangazo nacho kwa sasa kipo hatarini kutokana na kuendelea kuongezeka kwa ukumbwa wa Shimo la Mungu.
Simulizi zaidi juu ya maajabu ya shimo hili na nini kimo ndani ya shimo kukujia hivi punde hapahapa; www.thehabari.com.