Uporaji Fedha za Escrow Waziri Mkuu Pinda Atakiwa Kujiuzulu

Baadhi ya watu waliopata mgao wa fedha za Escrow.

Baadhi ya watu waliopata mgao wa fedha za Escrow.

*Mwanasheria Mkuu, Waziri wa Nishati na Katibu wake kuwajibishwa

HATIMAYE Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imewasilisha bungeni ripoti ya uchunguzi wa uporaji wa takribani bilioni 306 zinazodaiwa kuchotwa katika akaunti ya Tegeta Escrow zikiwemo fedha za Seriali ya Tanzania, huku ikitoa mapendekezo Waziri Mkuu wa Tanzania ajiuzulu kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake.

Akiwasilisha taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Zitto Kabwe bungeni, alisema kamati hiyo imethibitisha kuwa utaratibu mzima uliyotumika katika utoaji wa fedha hizo umegubikwa na mazingira ya rushwa na mchezo mchafu uliosaidia uchotwaji wa fedha kiasi cha bilioni 306 kuporwa kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT) na kutakatishwa na benki kadhaa nchini na nyingine za nje ya nchi. Fedha hizo zilikuwa ni mali ya Serikali na mbia wake kampuni ya IPTL.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa PAC, Deo Filikunjombe akiwasilisha mapendekezo ya Kamati ya PAC bungeni alisema baada ya kupitia vielelezo vyote vilivyopo kwenye ripoti ya CAG kamati ya bunge imejiridhisha pasipo na shaka kuwa Waziri Mkuu (Mizengo Pinda) alikuwa na taarifa zote kuhusiana na mchakato mzima wa uporaji wa fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow na ndio maana alikuwa akitetea bungeni hazikuwa za Serikali.

Sehemu ya fedha zilizokuwemo katika akaunti hiyo, Tanesco walikuwa na kiasi cha sh. bilioni 142 huku Wizara ya Nishati na Madini ilikuwa na sh. bilioni 40, na kodi ya ongezeko la thamani iliyopotea baada ya fedha kutolewa kiasi cha sh. bilioni 23 mali ya TRA.

“…Ushahidi ulioletwa unaonesha kuwa Waziri Mkuu alikuwa akipata taarifa za jambo hili na kamati imesikitishwa kuona kuwa hakuchukua uamuzi wowote wa kuzuia muamala huu usifanyike maamuzi au maelekezo yoyote ya kuzuia muamala huu usifanyike ilhali ana mamlaka kwa mujibu wa Katiba ya nchi…,” alisema Filikunjombe.

“…Waziri Mkuu atakuwa na madaraka ya juu ya udhibiti na usimamiaji utekelezaji wa siku hadi siku wa kazi na shughuli za Serikali ya Muungano…kamati ilijiuliza ni nini matamko ya mara kwa mara bungeni na nje ya bunge kuhusiana na suala hili kupotosha kwamba hazikuwa fedha za Serikali.

Katika taarifa hiyo kamati imebaini pia Wizara ya Nishati na Madini kupitia kwa Katibu Mkuu wake

(Elihakimu Maswi), haikufanya jitihada za kutosha kuhakiki mauziano ya hisa kama alivyokuwa imeomba hapo awali yamefanyika kitaratibu na muhusika kutambulika kisheria.

“Uongozi wa Wizara ya Nishati na Madini ilishindwa kutimiza wajibu wake ipasavyo kuhakikisha fedha za umma zinalindwa hivyo kufanikisha uchotaji wa fedha katika akaunti hiyo hivyo kuwasaidia wizi wa fedha hizo wahusika. Wahusika katika fedha hizo ni Serikali na IPTL,” ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imebaini kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Elihakimu Maswi aligoma fedha hizo kutolewa lakini ndani ya siku nne baadaye alibadili msimamo na kuruhusu fedha zilizopo katika akaunti ya Escrow kutolewa jambo ambalo linazua mashaka kwa mtumishi huyo wa Serikali.

Taarifa hiyo imebainisha kuwa malipo yote ya shs bilioni 167 na Dola za Kimareani milioni 22 yaliyokuwa katika akaunti hiyo yalilipwa kwa kampuni ya PAP na sio IPTL kupitia banki ya Stabic Novemba 27, 2013.

Walionufaika katika sehemu ya mgao wa fedha uliolipwa wapo viongozi wa siasa, majaji, viongozi wa madhehebu ya dini na watumishi wengine wa Serikali jambo ambalo limeibua mashaka ya uhusiano wa watu hao kulipwa mabilioni ya fedha toka kwa mmiliki wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing, Rugemalira.

Baadhi ya watu walienda kuchukua fedha katika benki tajwa wakiwa na mifuko ya rambo, maboksi, sandarusi na maguni. Na kutokana na muamala uliyofanyika tarehe 6 Februari, 2014 katika benki ya Mkombozi kiasi cha shilingi bilioni 3.3 na muamala wa benki ya Stanbic uliofanywa tarehe 23, Januari 2014 kiasi cha fedha taslimu sh. bilioni 73 ziligawiwa kwa watu kinyume na utaratibu wa Benki Kuu (BoT).

Kamati imependekeza Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya IPTL na PAP, Harbinder Singh Sethi kufikishwa Mahakamani alifanya udanganyifu kwa kushirikiana na viongozi waandamizi wa Serikali na kuwasilisha nyaraka feki za kuonesha kuwa ni mmiliki wa hisa 70 za na kufanikisha kuchota kiasi cha shilingi bilioni 306 kutoka BoT. Seti alikiuka sheria za kodi na kujipatia mali asiyostahili, kutakatisha fedha haramu na kuhujumu uchumi wa nchi.

Kamati imeitaka Takukuru na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Nchini (DCI) kumkamata, Harbinder Singh Sethi na kumfungulia mashtaka mara moja ya ukwepaji wa kodi, utakatishaji fedha haramu na wizi alioufanya katika sakata la uporaji wa fedha hizo. Aidha Kamati imeshauri mamlaka husika kuhakikisha inatumia sheria zilizopo kuhakikisha Singh Sethi anarejesha fedha zilizoporwa BoT.

Kamati pia imewataka waliopata mgao wa fedha wazirejeshe kwa kuwa kiasi hicho ni sehemu ya fedha ya Serikali na walio viongozi wa umma wachunguzwe kama walikiuka sheria ya maadili ya umma ambayo inawataka kutoa taarifa ya zawadi wanazopokea. Imependekeza pia kuvuliwa nyadhifa zao za kuchaguliwa na uteuliwa kutokana na makosa waliyoyafanya ikiwa ni pamoja na kufilisiwa kufidia fedha walizochota na kushtakiwa.

Stanbic banki na Mkombozi Wajumbe wa Bodi Kupitisha Wajumbe wote wa Bodi Tanesco. Naibu wa Nishati wa Madini alisema uongo bungeni na nchi ya Uingereza kutenguliwa uteuzi na kufikishwa mbele ya kamati ya maadili. Mamlaka itengue nafasi ya Waziri wa Nishati na Madini kwa kushindwa utekeleza majukumu yake na kufanikisha uporwaji wa fedha za umma katika akaunti ya Escrow.