Na Anna Titus na Happiness Tesha, MAELEZO-Dar-es-Salaam
RAIS mstaafu Ali Hassani Mwinyi ameyataka mashirika, taasisi za kijamii na makundi mengine kujitokeza na kuwasaidia watu wasiojiweza katika jamii ikiwemo ya walemavu wa ngozi (albino) na yatima.
Mwinyi ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam wakati wa halfa ya kukabidhi msaada wa chakula kwa watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) na yatima kilichotolewa na Jumuiya ya Kiislamu Tanzania na taasisi ya Rehema.
Rais Mwinyi alisema miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na changamoto kubwa katika utoaji wa huduma za kijamii kwa watu wasiojiweza, hatua inapelekea watu hao kujiona kwamba wamesahaulika na Serikali.
Aliongeza kuwa katika miaka ya 1980, Serikali ilifanya mabadiliko sera zake za kiuchumi ambapo fursa zilitolewa kwa taasisi, mashirika na wafanyabiashara kuwasaidia makundi mbalimbali ya kijamii.
Kwa mujibu wa Rais Mwinyi alisema makundi yanayohitaji misaada ya kijamii ni mengi, hivyo jukumu hilo halina budi kuungwa mkono na taasisi na mashirika mengine hapa nchini.
“Juhudi zilizoonyeshwa na kituo cha rehema na Tampro zinaungwa mkono na Serikali kwani kushindana katika jambo la kheri kama hili la kusaidia walemavu wa ngozi ni rehema kubwa kwa Mwenyezi Mungu,”
Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Alshaymaa Kweir alisema jamii ya watu wenye ulemavu wanakabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwemo maradhi ya kansa yanayotokana na athari za jua wakati wanapokuwa wakijitafutia riziki zao.
Alisema msaada huo wa chakula katika mwezi mtukufu wa ramadhani kutoka taasisi ya rehema na Tampro hauna budi kuungwa mkono na mashirika mengine ya kijamii kwani jukumu la kuwasaidia walemavu ni suala la kila mwanajamii.
“Ulemavu huu wa ngozi tulionao sisi jamii ya albino si uwezo wetu bali ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu, hivyo basi jamii haina budi kuwasaidia watu wenye matatizo mbalimbali ili nao wajione kuwa ni sawa na binadamu wengine,”
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Rehema, Abdi Adamu alisema msaada huo ni maalum kwa ajili ya kuzisaidia jamii za walemavu wa ngozi kuondokana na tatizo la vyakula katika kipindi hiki cha mfungo wa Mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Alisema msaada ulitolewa na taasisi yake ni unga wa ngano, maharage, mchele, chumvi, sukari, mafuta ya kupikia, nyanya za makopo, tambi, amira na dawa ya mbu, ambavyo vyote kwa pamoja thamani yake ni sh. milioni 15.
“Shughuli kubwa za taasisi yetu ni pamoja na kutoa huduma za kijamii ikiwemo elimu, maji, chakula. Katika elimu tayari tuna Chuo cha Ualimu cha Safina kilichopo tabata chenye jumla ya wanafunzi 114 na kinachotoa mafunzo ya ualimu na kinawelenga watu wasio na uwezo mkubwa wa kulipa ada,” alisema Adam
Aidha Adam aliiomba Serikali kuwasaidia eneo la ardhi kwa ajili ya ujenzi wa chuo cha ualimu ili kuondokana na uhaba wa walimu uliopo kwa sasa nchini.