ENDAPO ratiba ya madaktari wanaomtibu Rais Jakaya Kikwete katika Hospitali ya Johns Hopkins nchini Marekani itakwenda kama ilivyopangwa kiongozi huyo atarejea nchini Tanzania, Novemba 29, 2014.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Taratibu za matibabu ya Rais Kikwete, zimekamilika Novemba 24, 2014. Taarifa hiyo imesema Rais Kikwete ataendelea kupumzika na kuangaliwa kwenye Hoteli Maalum inayohusiana na Hospitali ya Johns Hopkins kwa siku mbili hadi tatu kabla ya kuanza safari ya kurejea nyumbani.
“Kama kila kitu kitakwenda kama ilivyopangwa na madaktari, Rais Kikwete anatarajiwa kurejea nyumbani Jumamosi. Rais Kikwete aliondoka nchini Alhamisi ya Novemba 6, 2014, kwenda kufanyiwa uchunguzi wa afya yake lakini madaktari katika Hospitali ya Johns Hopkins waliamua kumfanyia upasuaji wa tezi dume Jumamosi ya Novemba 8, 2014.”
Taarifa imeeleza kuwa Rais Kikwete anaendelea kuwashukuru Watanzania kwa sala na maombi yao ya kumtakia heri ya kupona haraka na kurejesha afya njema katika kipindi chote cha ugonjwa wake.