Na Janeth Mushi, Arusha
MKURUGENZI wa Manispaa ya Arusha, Estomih Chang’a amesema kuwa bado hajapokea barua kutoka katika Chama Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ya kutowatambua madiwani watano waliofukuzwa ndani ya chama hicho.
Chang’a alitoa kauli hiyo jana mjini hapa alipokuwa akitoa taarifa ya kuhairishwa kwa kikao cha Baraza la Madiwani katika Manispaa ya Arusha kilichokuwa kifanyike jana.
Hata hivyo alisema kuahirishwa kwa kikao hicho hakuna uhusiano wowote na mgogoro uliopo CHADEMA. Alisema kikao hicho kimeshindwa kufanyika kutokana na sababu zilizodaiwa ni za kiutawala.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa wameahirisha kikao hicho cha baraza la madiwani kwa sababu za kiutawala ikiwa ni pamoja na maandalizi ya majibu ya maagizo ya vikao vilivyopita ambayo yalikuwa hayajakamilika.
Chang’a alisema kuwa kuahirishwa kwa kikao hicho hakuna maana kuwa wameogopa kauli zilizotolewa juzi katika Viwanja vya NMC na Viongozi wa ngazi ya juu wa Chadema wakiongozwa na Katibu Mkuu, Dk. Wilbroad Slaa kuwa Mkurugenzi huyo anawabeba madiwani hao.
“Kiukweli sijapokea barua yoyote ya kufukuzwa kwa madiwani hao na taratibu lazima zifuatwe na wanaodai mimi au CCM tunawabeba madiwani hao si kweli hayo ni mawazo yao kwani tunafanya kazi kwa kufuata taratibu, kanuni na sheria na kikao kilichokwua kifanyike leo hakijaahirishwa kwa sababu ya Chadema bali ni kwa sababu za kiutawala,” alisema Mkurugenzi huyo.
Mkurugenzi huyo wa Manispaa ya Arusha alisema kuwa kikao hicho cha Baraza la Madiwani kinatarajiwa kufanyika wiki ijayo ingawa hakufafanua kitafanyika siku gani.
Aidha Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema juzi alipokuwa akiwahutubia wakazi wa jiji la Arsuah katika viwanja vya NMC akitoa ufafanuzi juu ya kufukuzwa kwa madiwani hao watano katika mgogoro wa Meya wa jiji hili aliwataka wananchi hao kutokumtambua Meya wa Manispaa hiyo Gaudance Lyimo(CCM)
Lema aliwaeleza wananchi hao kuwa pindi wanapowaona madiwani hao wawazomee kwani chama kimeshatoa barua Manispaa ya Arusha kwa Mkurugenzi ,Changa’h ya kutowatambua madiwani hao pia wasihudhurie vikao ingawa Mkurugenzi anawabeba
Alisema kuwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kama inataka kuwachukua madiwani hao iwachukue na kuwasimamisha wagombee nafasi za udiwani kwa tiketi ya CCM na kudai kwua chama hicho katika uchaguzi huo mdogop itachukua kata zote tano.
Katika mkutano huo madiwani sita wa CHADEMA mbali na wale waliofukuzwa hawatahudhuria vikao hivyo hadi hapo siku 30 walizotoa zitakapoisha kwa makubaliano ndio watahudhuria vikao vya Baraza la Madiwani lakini kama hakutapatikana suluhu watafanya mkutano mkubwa wa hadhara kisha wataandamana hadi Ofisi ya Mkurugenzi na kuifunga.
Madiwani hao wa CHADEMA ambao hawatahudhuria vikao vya halmashauri hadi muafaka utakapopatikana ni Ephata Nanyaro kata ya Levolosi, Elibariki Malley (Engutoto), Viola Lobikoki(Viti Maalum), Doita Harri (Ngarenaro), Crispin Tarimo (Sekei) na Sabina Francis(Viti Maalum).
Madiwani waliofukuzwa uanachama ni Aliyekwua Naibu Meya wa Manispaa ya Arusha Estomii Malla (Kimandolu), John Bayo (Elerai), Charles Mtanda (Kaloleni), Reuben Ngowi ( Themi) pamoja na Rehema Mohamed (Viti Maalum).
Kwa upande wake Meya wa Jiji la Arusha Gaudance Lyimo alisema kuwa Serikali inamtambue yeye kama Meya wa jiji hilo japo Chadema wanasema hawamtambui.