Samsung, UNESCO Kujenga Kijiji cha Digitali Loliondo

Baadhi ya wafanyakazi wa UNESCO na Samsung wakifuatilia kwa umakini hafla hiyo fupi ya kutiliana saini makubaliano baina ya Samsung Tanzania na UNESCO.

Baadhi ya wafanyakazi wa UNESCO na Samsung wakifuatilia kwa umakini hafla hiyo fupi ya kutiliana saini makubaliano baina ya Samsung Tanzania na UNESCO.


DSC_0062

Mwakilishi mkazi shirika la UNESCO nchini Bi. Zulmira Rodrigues  na Mkurugenzi wa  Samsung Electronics nchini Tanzania, Bw. Mike Seo wakibadilishana nyaraka za makubaliano hayo yaliyofanyika ofisi za UNESCO.

Na Mwandishi wetu

SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni  (UNESCO) limetiliana saini mkataba na kampuni ya elektroniki ya Samsung ya ujenzi wa Kijiji cha Digitali cha Ololosokwan, Loliondo.

Makubaliano hayo yalitiwa saini hivi karibuni kati ya Mwakilishi mkazi Unesco nchini Bi. Zulmira Rodrigues  na Mkurugenzi wa  Samsung Electronics nchini Tanzania, Bw. Mike Seo katika hafla iliyofanyika ofisi za UNESCO.

Kijiji hicho kitakuwa na  shule yenye Tehama ikiwa na maunganisho ya intaneti, kiliniki ya kisasa ikiwa na kituo cha  teknolojia ya mawasiliano yenye kuwezesha utabibu (telemedicine) na  jenereta linalotumia nguvu za jua kwa ajili ya kijiji hicho.

Utiaji saini huo ulioshuhudiwa na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya UNESCO, bi. Leah Kihimbi kutoka wizara ya habari, vijana, utamaduni na michezo na Dkt. N.  Iriya kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) Dar es Salaam na wafanyakazi wa UNESCO.

Katika hafla hiyo Bi. Rodrigues  amesema kwamba mradi huo utawezesha UNESCO kuwapatia vijana wa Kimasai elimu kutokana na ukweli kuwa kwa utamaduni na kazi zao za ufugaji wamekuwa wakipata shida ya kupata elimu.

“Kupitia kijiji hiki vijana wataendelea na masomo hata kama wanachunga mifugo yao”, alisema Bi. Rodrigues.

Naye  Mkurugenzi wa Samsung Electronics nchini Tanzania miongoni mwa manufaa makubwa yatakayopatikana katika mradi huo wa kijiji cha digitali huko Loliondo  ni kuweza kupata nishati  rahisi na iliyo rafiki kwa mazingira.

Alisema kwamba Afrika imekuwa mstari wa mbele katika uanzishaji wa vijiji vya digitali. Aidha kwa kitendo hicho Afrika inaonesha dunia ni kwa namna teknolojia inaweza kutumika kuleta mabadikliko chanya  yanayotakiwa kwa ajili ya maendeleo ya wananchi waliopo vijijini.

Bi Leah Kihimbi ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya habari,vijana, utamaduni na michezo, alisema kupitia vijiji vya digitali  itawezekana kutekeleza program ya elimu  kwa watu wanaoishi Loliondo huku tamaduni zao zikihifadhiwa.

Kijiji hicho cha Loliondo kitakuwa cha nne katika vijiji vya kidigitali barani Afrika. Inatarajiwa kwamba kijiji kingine kitajengwa mjini Zanzibar kwa ushirikiano wa UNESCO na Samsung Electronics mwaka 2015.

Untitled 1

Pichani ni muonekano wa mchoro wa kijiji hicho utakavyokua.